Papa:kushindwa kuheshimu maadili ya kidini huleta kutovumiliana duniani!
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Katika hotuba yake Jumamosi tarehe 30 Novemba 2024 , kwa washiriki wa Mkutano wa maadhimisho ya Kumbu kumbu ya miaka 100 ya Kongamano la kwanza la "Dini Zote", lililohamasishwa na ‘Sree Narayana Dharma Sanghom Guru,’ Baba Mtakatifu Franciko alimsalimia Sivagiri Mutt na wote walioshiriki na wa mapokeo mbalimbali ya kidini, ambao wametoka Kerala, nchini India, na kutoka sehemu nyinginezo za dunia ili kusherehekea ukumbusho wa miaka mia moja wa “Kongamano la kwanza la Dini Zote” lililoandaliwa na kiongozi wa kiroho na mwanamageuzi wa kijamii Sree Narayana Guru. Ni furaha ya Papa Francisko kujua kuwa Kongamano hilo pia limeandaliwa kwa ushirikiana na Baraza la Kipapa la Majadiliano ya Kidini ili kuadhimisha tukio hili muhimu katika historia ya mazungumzo ya kidini nchini India na Asia.
Mada iliyochaguliwa kwa ajili ya Mkutano, “Dini Pamoja kwa Ubinadamu Bora, kwa hakika ni muhimu kwa nyakati zetu. Sree Narayana Guru alijitolea maisha yake kukuza mwamko wa kijamii na kidini kwa ujumbe wake wazi kwamba wanadamu wote, bila kujali makabila yao au mila zao za kidini na kitamaduni, ni washiriki wa familia moja ya kibinadamu. Alisisitiza kuwa kusiwe na ubaguzi dhidi ya mtu yeyote kwa njia yoyote na kwa kiwango chochote. Baba Mtakatifu Francisko amesisitiza kwamba ujumbe wake ni muhimu kwa ulimwengu wetu leo, ambapo tunashuhudia visa vinavyoongezeka vya kutovumiliana na chuki kati ya watu na mataifa. Cha kusikitisha ni kwamba maonesho ya ubaguzi na kutengwa, mivutano na unyanyasaji wa tofauti za asili ya kikabila au kijamii, rangi, lugha na dini ni uzoefu wa kila siku wa watu binafsi na jamii nyingi, hasa kati ya maskini, wasio na uwezo na wasio na sauti.
Katika Hati ya Udugu wa Kibinadamu kwa Amani ya Dunia na Kuishi Pamoja ambayo alitia saini pamoja na Imamu Mkuu wa Al-Azhar Ahmad Al-Tayyeb, Papa amesema “tulisema kwamba Mungu “amewaumba wanadamu wote sawa katika haki, wajibu na utu, na amewaita waishi pamoja kama kaka na dada”(Abu Dhabi, 4 Februari 2019). Kwa njia hiyo “Dini zote hufundisha ukweli wa kimsingi kwamba kama watoto wa Mungu mmoja ni lazima tupendane na kuheshimiana, kuheshimu tofauti na tofauti katika roho ya udugu na ushirikishwaji, na kutunza kila mmoja wetu na dunia, makao yetu ya pamoja. Kutofuata mafundisho matukufu ya dini ni mojawapo ya sababu zinazosababisha hali ya taabu ambayo dunia yetu inajipata ndani yake. Watu wa wakati wetu watagundua tena thamani ya mafundisho ya juu ya mapokeo ya kidini ikiwa tu sote tutajitahidi kuyaishi na kusitawisha uhusiano wa kindugu na wa kirafiki na kila mtu, kwa lengo la pekee la kuimarisha umoja kati ya utofauti, kuhakikisha kuwepo kwa uwiano kati ya tofauti, na kuwa wapenda amani licha ya matatizo na changamoto tunazolazimika kukabiliana nazo.”
Kama wafuasi wa mila zetu za kidini, tunapaswa daima kushirikiana na watu wote wenye mapenzi mema katika kukuza “utamaduni wa heshima, utu, huruma, upatanisho na mshikamano wa kindugu”(Tamko la Pamoja la Istiqlal, 5 Septemba 2024). Kwa njia hii, tunaweza kusaidia kushinda utamaduni wa ubinafsi, kutengwa, kutojali na vurugu ambayo kwa huzuni inaenea. Tukichota kutoka katika kweli za kiroho na tunu ambazo tunazo kwa pamoja, lakini zilizokita mizizi ndani na kujitolea kwa imani na imani zetu za kidini, na tutembee pamoja na kufanya kazi pamoja ili kujenga ubinadamu bora! Papa Francisko kwa kuhitimisha amewashukuru kwa uwepo wao na kwa kujitolea kwa mazungumzo na maelewano kati ya wafuasi wa dini mbalimbali. Katika kukuhakikishia maombi yake amependa pia kuwaomba wamkimbuke katik sala zao.