Papa awashukuru maaskari wa Italia kwa kusaidia wanyonge wakati wa vita na majanga!
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko, Alhamisi tarehe 7 Novemba 2024 amekutana na wajumbe Kitengo cha Usafiri na Nyenzo za Kijeshi nchini Italia katika fursa ya miaka 70 tangu kutangazwa kwa MtakatifuChristopher, kuwa Msimamizi wao, mnamo tarehe 4 Novemba 1954 na aliyemtangaza alikuwa ni Mtumishi wa Mungu Papa Pio XII. Papa Francisko ameongeza kusema kuwa “Pia hata mimi nina ibada kwa Mtakatifu Christopher, huwa navaa medali ya Mtakatifu Christopher ili kunisaidia kusonga mbele kidogo.” Baba Mtakatifu Francisko katika hotuba yake amefurahi kwamba kikundi hiki cha wanajeshi walioomba na kupata usimamizi wa Mtakatifu shahidi, ambaye aliacha vita ili kushuhudia Kristo. Awali ya yote hii ina maana ya kutambua kuwa hakuna taaluma na hali ya maisha yoyote ambayo hakuna ulazima wa kuweka katika nanga ya thamani za kina na kutokuwa na haja ya ulinzi wa kimungu. “Kwa hakika, mtu anaweza kusema kwamba, kadri taaluma ya mtu inavyohusisha uwezekano wa kuokoa maisha au kupoteza maisha, kutoa msaada, na ulinzi, ndivyo mtu anavyohitaji kudumisha kanuni za juu za maadili na msukumo unaotoka juu.”
Kuwa na Mtakatifu msimamizi na kumfuata kwa shauku ina maana ya kujibidisha, katika huduma ya Taifa, kufanya kazi kwa mtindo ambao unalazimisha juu ya hadhi ya kila binadamu, ambayo ni mfano wa Muumba na sisi ni sura na ya Mungu. Mtindo ambao unatofautisha kwa kulinda walio wadhaifu zaidi na wale ambao wanajikuta katika hatari, iwe katika vita, iwe katika majanga ya asili na tauni. Kumheshimu Mtakatifu wao Mlinzi pia kunamaanisha kutambua kwamba utaalamu, hisia ya wajibu, kujitolea kwa kila mmoja kwa hakika ni muhimu, lakini kwamba zaidi ya haya yote ni muhimu pia kupata kutoka Mbinguni nyongeza ya Neema, muhimu ya kubeba katika utume ili uwe bora zaidi iwezekanavyo. Inamaanisha, kwa ufupi, kutambua kwamba sisi si waweza wa yote, kwamba si kila kitu kiko mikononi mwetu bali, tunahitaji baraka za kimungu.
Papa Francisko amewapongeza kwa usikivu wao huu, kiukweli wanajua thamani na uzuri wa kazi zao, ambazo hazitakuwa za ajabu kwao wenyewe, lakini zinaweza kuwa hivyo ghafla. Wanajua hili vyema: huwa hivyo wanapoitwa kuingilia kati katika shughuli za ulinzi wa amani, au kukabiliana na matokeo ya majanga ya asili, kutekeleza kazi za ulinzi wa raia na shughuli muhimu za vifaa. Kwa hakika, wametoa kazi yao kwa ajili ya kusaidia wananchi na mamlaka mahalia na wilaya katika nyakati mbalimbali za dharura kama vile matetemeko ya ardhi, mafuriko na magonjwa ya milipuko. Wameweka kambi, hema na hospitali za kambi, wamesafirisha mahitaji ya msingi, vifaa muhimu kwa ujenzi na chanjo, wamekuwepo pia nje ya mipaka ya kitaifa kama sehemu ya misheni ya kulinda amani, kuhakikisha shughuli za usambazaji, kwa vifaa vya kijeshi na kwa usafirishaji na usambazaji wa nyenzo na vifaa mbalimbali kwa madhumuni ya kibinadamu. Utekelezaji wa wakati, ulioratibiwa vyema na wa mara kwa mara wa shughuli hizi zote una jina sahihi liitwalo” huduma.”
Inahitaji kujikita kwa udani juu ya manufaa ya wote, bila kuacha nguvu na jitihada, kutorudi nyuma katika uso wa hatari ili kukamilisha kazi, ambayo mara nyingi husababisha kuokoa maisha ya binadamu na inaweza kuhusisha kujisadaka kwa usalama wa wao wenyewe. “Huduma, utumishi na huduma hutupatia Hadhi. Je hadhi yanini ni nini? Papa ameuliza na kujibu kuwa inapaswa kuwa: “Mimi ni mtumishi.” Na ndiyo heshima kubwa.” Katika suala hilo, ni muhimu kwamba wanaume na wanawake wengi, mwishoni mwa huduma yao ya kazi, hawajitenga mbali na Kikosi cha Usafiri na Vifaa, lakini wanachagua kuwa sehemu ya Chama cha Kitaifa cha Madereva cha Italia. Kama watu wa kujitolea, wanatoa msaada wao kwa jamii, wakishuhudia kwamba tabia ya kutumikia imekuwa tabia ya asili ndani yao, kama tabia ya kawaida ya kuwepo kwao, ambayo haiwezi kuachwa wakati wowote, lakini ambayo badala yake inarekebishwa kulingana na umri na hali ya kila mtu, kwa sababu kila mtu, katika umri wowote, anaweza kutoa mchango wake, akiendelea kuhudumu.
Christopher maana yake ni "aliyembeba Kristo". Wanapofanya kazi kwa bidii kila siku bila kuweka akiba kwa ajili ya utendaji kazi wa idara zao; wanapokwenda kusaidia watu walioathiriwa na majanga ya asili au migogoro ya silaha, wao , wakati mwingine bila kujua, kwa maana fulani wanapeleka mtindo wa Kristo, ambaye alikuja kutumikia na sio kutumikiwa (rej. Mt 10:45); huyu ndiye Yesu aliyepita katika Dunia hii akifaidisha na kuponya kila mtu (rej Matendo 10:38). Papa Francisko amesema wamwombe msimamizi wao Mtakatifu Christopher ili kuwaweka daima katika nia hizo njema. Na, katika suala hilo, Papa amejieleza kwa sala yao ya nembo: “Autiere”, ambayo inasema hivi: “Ee Mwenyezi Mungu na wa milele, linda na kubariki huduma tunayotoa kwa ndugu zetu na kutupatia uwezo wa kutumia mali zetu pia kusaidia na kuokoa wahitaji.” Kwake Maria, Mama wa Mungu, Papa amesema " awalinde na kuwasindikiza; wawe watenda kazi na mafundi wa amani. Na kutoka moyoni mwake Baba Mtakatifu amewabariki wote na kubariki familia zao. Na amewaomba mwamwombee tafadhali.