Tafuta

2024.11.16 Papa amekutana na Washiriki wa Mkutano uliandaliwa na Maktaba ya Kitume ya Vatican. 2024.11.16 Papa amekutana na Washiriki wa Mkutano uliandaliwa na Maktaba ya Kitume ya Vatican.  (Vatican Media)

Papa:maktaba zinapaswa kuwa mahali pa mikutano na amani

Papa amekutana na wawakilishi wa taasisi za sekta kuu duniani,waliofika Roma kushiriki katika mkutano wa kimataifa ulioandaliwa na Maktaba ya Kitume ya Vatican.“Tunaitikia ukoloni wa kiitikadi na kufuta kumbukumbu.Taasisi zao zimeitwa kupitisha urithi wa siku za nyuma kwa njia zenye maana kwa vizazi vipya vilivyozama katika utamaduni wa kimiminika na kuhitaji mazingira dhabiti,yenye uundaji,kukaribisha,kujumuisha na kutumaini siku sijazo."

Na Angella Rwezaula – Vatican.

Jumamosi tarehe 15 Novemba 2024, Baba Mtakatifu Fransisko amekutana na wawakilishi wa taasisi za sekta kuu duniani, waliofika mjini Roma kushiriki katika mkutano wa kimataifa ulioandaliwa  na Maktaba ya Kitume ya Vatican. Akianza hotuba yake Papa alisema kuwa “Nilifurahishwa sana kujifunza kuhusu Mkutano huu, kwa kuongozwa na mada: "Conservata et perlecta aliis tradere, Library in Dialogue", yaani "Imehifadhiwa na kusomwa ili kuwapitishia wengine, Maktaba katika Mazungumzo," ambayo ni ishara ya uwazi wa Maktaba ya Vatican kwa ulimwengu. Ndivyo nilivyomuomba Askofu Mkuu Zani nilipomteua. Nikamwambia, “Uende ufungue.” Baada ya kumaliza kusema hayo Papa amewasalimu Wakutubi na wafadhili wanaochangia kwa ukarimu mahitaji ya Taasisi hiyo. Kwa shukrani nyingi, amewakaribisha pia wawakilishi wa Maktaba ishirini na tatu za hadhi duniani kote ambao wameshiriki katika Mkutano huo. “Maktaba ya Vatican inataka kufanya mazungumzo na taasisi zinazohusiana kuhusu masuala kadhaa muhimu, na imeanzisha vikundi vya mafunzo ambavyo ninaamini vitaendelea na kuzaa matunda kwa ajili ya kutajirishana kwenu.”

Papa wa Maktaba

Baba Mtakatifu amesema kuwa mazungumzo kama haya ya vitendo juu ya mada zilizofafanuliwa vyema hakika yatachangia katika kuimarisha ufikiaji wa kielimu na kiutamaduni wa Maktaba zao katika nyakati hizi zinazobadilika. Taasisi zao zimeitwa kupitisha urithi wa siku za nyuma kwa njia zenye maana kwa vizazi vipya vilivyozama katika utamaduni wa kimiminika na hivyo kuhitaji mazingira dhabiti, yenye uundaji, ya kukaribisha na kujumuisha ambamo wanaweza kuunda mchanganyiko mpya wenye uwezo wa kuelewa mambo ya  sasa ya matumaini kwa siku zijazo. Hakika kazi yao ni ya kusisimua. Katika suala hili, Papa aliibua sura ya Papa Pio XI, Achille Ratti, ambaye baadhi ya wasomi wanamwita “Papa wa maktaba”. Papa Pio alikuwa Mkutubi wa Maktaba yenye Heshima ya Ambrosian huko Milano na baadaye, Maktaba ya Vatican. Mtu wa vitendo, aliyevutiwa na sayansi na mawasiliano ya watu wengi, alikuwa akijua umuhimu mkubwa wa maktaba wakati wa shida sana katika historia, kati ya vita viwili vya ulimwengu.

Juhudi za Papa za kukuza utaratibu wa kuorodhesha

Utamaduni wa Ulaya ulipozidi kuzorota na kuwa mgongano wa itikadi, Papa alipanua sehemu zote za Maktaba ya Vatican, akakuza utaratibu wa kuorodhesha na kufungua shule kwa ajili ya mafunzo ya wasimamizi wa maktaba. Chini ya ulinzi wake, Maktaba ya Vatican ikawa kimbilio salama kwa wasomi wengi, kuweka ndani wale walioteswa na tawala za kiimla ambazo Papa alipinga vikali. Mtazamo wa "Papa huyo wa maktaba", mbunifu, jasiri na mwenye maamuzi, unaweza kutumika kama msukumo tunapojikuta katika ulimwengu wa leo vile vile tunakabiliwa na changamoto kubwa za kitamaduni na kijamii zinazohitaji majibu kwa wakati na mwafaka. Teknolojia imebadilisha sana jinsi wasimamizi wa maktaba wanavyo fanya kazi, na kuifanya iwe tofauti zaidi na isiyochukua wakati mwingi. Vyombo vya habari vya mawasiliano na teknolojia ya habari vimefungua uwezekano usiofikirika miaka michache iliyopita. Mifumo ya kusoma, kuorodhesha na kutumia rasilimali za maktaba imeongezeka. Haya yote yameleta faida nyingi, lakini pia idadi ya hatari: hifadhidata kubwa ni rasilimali tajiri ya kuchimbua, lakini ubora wao umeonekana kuwa mgumu kudhibiti.

Nchi chache tu duniani zinaweza kufanya utafiti

Kutokana na gharama ya juu ya kusimamia makusanyo ya magazeti, hasa ya zamani, ni nchi chache tu duniani zinazoweza kutoa huduma fulani za ushauri na utafiti. Matokeo yake, mataifa yenye faida kidogo yanaweza kukumbwa na si umaskini wa mali tu, bali pia umaskini wa kiakili na kitamaduni. Kuna hatari kubwa kwamba vita vya sasa vya dunia vilivyoganwanyika vipande vipande vitapunguza kasi ya maendeleo ambayo tayari yamepatikana. Hatari ni kwamba mifumo ya gharama kubwa ya silaha inaweza kuzuia ukuaji wa utamaduni na njia zinazohitaji kuendeleza. Au kwamba migogoro inayoharibu shule, vyuo vikuu na miradi ya elimu inaweza kuzuia wanafunzi kujifunza na kufanya utafiti. Taasisi nyingi za kiutamaduni hujikuta hazina ulinzi mbele ya vita, ghasia na uporaji. Ni mara ngapi imekuwa hivyo huko nyuma! Hebu tufanye kazi ili kuhakikisha kwamba haitatokea tena. Tujibu mgongano wa ustaarabu, ukoloni wa kiitikadi na utamaduni wa kufuta, kwa kukuza utamaduni wa kweli. Itakuwa mbaya kama, pamoja na kuta nyingi za kimwili zinazogawanya nchi, kuta za mtandao pia zinajengwa. “Ninyi, kama Wakutubi, mna jukumu muhimu la kuchukua katika suala hili, sio tu katika kutetea urithi wetu wa kihistoria, lakini pia katika kukuza maarifa. Ninawahimiza muendelee kuhakikisha kuwa taasisi zenu ni mahali pa amani, maeneo ya kukutana na majukwaa ya majadiliano ya wazi.”

Kanuni nne katika Waraka wa Evagelii Gaudium

Kama mchango katika jitihada hii, ningependa kupendekeza kwa tafakari yaoenu kanuni nne nilizoziweka katika Waraka wangu wa Kitume Evangelii Gaudium (taz. 222-237). Kwanza, wakati ni mkubwa kuliko nafasi. Nyinyi ni walinzi wa hazina kubwa ya elimu. Na haya yawe mahali ambapo wakati umetengwa kwa ajili ya kutafakari na uwazi kwa mwelekeo wa kiroho na upitao wa maisha yetu. Kwa njia hiyo, unaweza kupendelea mafunzo ya muda mrefu bila kushughulikiwa na matokeo ya haraka na kwa hivyo, kwa kukuza ukimya na kutafakari, kuhimiza maendeleo ya ubinadamu mpya. Pili, umoja unashinda migogoro. Utafiti wa kielimu bila shaka huzua mabishano nyakati fulani, ambayo yanapaswa kuwa mada ya majadiliano mazito, ya uaminifu na yenye heshima. Maktaba lazima ziwe wazi kwa nyanja zote za maarifa na zitoe ushahidi kwa madhumuni ya pamoja huku kukiwa na mbinu tofauti.

Maisha yetu yamejikita katika mahusiano ya kijamii na mitandao

Tatu, ukweli ni muhimu zaidi kuliko mawazo. Ni muhimu kufanya maamuzi madhubuti na ya kweli huku tukidumisha mtazamo wa kiuhakiki na wa kubahatisha, ili kuepusha mgongano wowote wa uwongo kati ya mawazo na uzoefu, ukweli na kanuni, mazoezi na nadharia. Ikiwa tunatafuta ukweli kwa dhati, tafakari yetu inapaswa kuheshimu ukuu wa ukweli kila wakati. Nne, kitu kizima ni kikubwa kuliko sehemu. Kazi yetu inatutaka kupatanisha mvutano kati ya maslahi ya ndani na kimataifa, kwa kutambua kwamba hakuna mtu aliyetengwa. Maisha yetu yamejikita katika mahusiano ya kijamii na mitandao ambayo inahitaji ushiriki wetu wa kuwajibika. Papa amewaomba wasijikuta wanakatishwa  tamaa na ugumu wa ulimwengu ambamo tumeitwa kufanya kazi! Kila jambo ambalo wameshiriki siku hizi liwasaidie wao na washirika wao kuwa kama “mwandishi” mwenye hekima aliyesifiwa na Bwana Yesu, ambaye alikuwa na uwezo wa kuchota kutoka hazina zake mpya na za kale, kwa faida ya wote (rej. Mt. 13:52). Papa amewabariki wote na kazi wanayofanya. Anawaombea na anaomba wamwombee.

Papa kwa Maktaba Vatican
16 November 2024, 13:20