Papa,Siku ya Maskini duniani:Dhiki na matumaini hupingana katika pambano ndani ya mioyo yetu!

Baba Mtakatifu ameongoza Ibada ya Misa Takatifu katika Siku ya Maskini Duniani Novemba 17 katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican.Katika mabuhizi amesisitiza juu ya kutambua uwepo wa Mungu katika mateso ya maskini na kutenda kwa matumaini na huruma mbele ya dhuluma kwa sababu kila tendo la huruma ni ishara ya matumaini.

Na Angella Rwezaula – Vatican.

Katika Dominika ya Tatu ya mwezi Novemba, ambapo mama Kanisa ameadhimisha Siku ya Maskini Duniani kwa 2024, Baba Mtakatifu Francisko ameongoza Ibada ya Misa Takatifu katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro, mjini Vatican kwa ushiriki wa waamini wengi, lakini zaidi makundi ya maskini kutoka sehemu mbali mbali za dunia. Katika mahubiri yake aliongozwa na masmoo ya siku na Injili ya Marko, ambayo imemfungulia hisia kubwa za uchungu wa Ulimwengu wa leo unavyoendelea. Papa alianza kusema kuwa "Maneno ambayo tumetoka kuyasikia yanaweza kuamsha hisia za uchungu ndani yetu; kiukweli, ni tangazo kubwa la matumaini. Kwani, ikiwa kwa upande mmoja Yesu anaonekana kueleza hali ya akili ya wale ambao wameona uharibifu wa Yerusalemu na kufikiri kwamba mwisho umefika sasa, wakati huo huo Anatangaza jambo lisilo la kawaida: kwa usahihi katika saa ya giza, ukiwa, wakati kila kitu kinaonekana kuporomoka, Mungu anakuja, Mungu anakuja karibu, Mungu hutukusanya ili kutuokoa.”

Maadhimisho ya Siku ya Maskini duniani
Maadhimisho ya Siku ya Maskini duniani

Kwa njia hiyo Baba Mtakatifu ameeleza kuwa Yesu anatualika kuwa na mtazamo mkali zaidi, kuwa na mitazamo yenye uwezo wa "kusoma ndani" matukio ya historia, na kugundua kwamba, hata katika uchungu wa mioyo yetu na wakati wetu, kuna tumaini lisiloweza kutetemeka, tumaini lisilotikisika ambalo huangaza. Katika Siku hii ya Maskini Duniani, basi, tuzingatie kwa usahihi mambo haya mawili: dhiki na matumaini, ambayo daima hupingana katika pambano kwenye uwanja wa mioyo yetu. Kwanza kabisa uchungu. Ni hisia iliyoenea katika enzi yetu, ambapo mawasiliano ya kijamii huongeza matatizo na majeraha, na kufanya ulimwengu usio na usalama zaidi na wakati ujao usio na uhakika zaidi. Hata Injili leo inafungua kwa picha inayoonesha dhiki ya watu katika ulimwengu, na inafanya hivyo kwa lugha ya mwisho wa dunia(apocalyptic) kwamba “Jua litatiwa giza, mwezi hautatoa mwanga wake tena, nyota zitaanguka..." na hivyo kwenye Injli ya (Mk 13,24-25 ). Ikiwa mitazamo yetu itaacha  habari za ukweli tu, uchungu unachukua nafasi ndani yetu. Hata leo hii, kiukweli, tunaona jua lina giza na mwezi unatoka, tunaona njaa, njaa inayowakandamiza ndugu wengi wasio na chakula, tunaona maajabu ya vita, tunaona vifo vya watu wasio na hatia; na, tukikabiliwa na hali hii, tunaingia katika hatari ya kuzama katika kuvunjika moyo na kutotambua uwepo wa Mungu ndani ya janga la historia.

Maadhimisho ya Siku ya Maskini 17 Novemba
Maadhimisho ya Siku ya Maskini 17 Novemba

Hivyo, tunajihukumu wenyewe kwa kutokuwa na uwezo; tunaona dhuluma inazidi kutuzunguka ambayo husababisha maumivu ya maskini, lakini tunajiunga na mkondo wa kujiuzulu wa wale ambao, kwa urahisi au uvivu, wanafikiri kwamba “dunia iko hivyo” na kusema “siwezi kufanya chochote kuhusu hilo.” Kisha hata imani ya Kikristo yenyewe imepunguzwa kuwa ibada isiyo na madhara, ambayo haisumbui mamlaka ya ulimwengu huu na haitoi dhamira thabiti ya hisani. Na wakati sehemu ya ulimwengu inahukumiwa kuishi katika makazi duni ya historia, wakati ukosefu wa usawa unakua na uchumi unawaadhibu walio dhaifu, wakati jamii inajitolea kwenye ibada ya sanamu ya pesa na matumizi, hutokea kwamba maskini na waliotengwa hawawezi kufanya chochote ila kuendelea kusubiri (rej Waraka wa Kitume wa  Evangelii gaudium, 54). Lakini hapa Yesu, katikati ya picha hiyo ya Injili, anaakisi tumaini. Anafungua upeo wa mtazamo, anapanua mitizamo  ili tujifunze kufahamu, hata katika hatari na maumivu ya ulimwengu, uwepo wa upendo wa Mungu anayekaribia, ambaye hatutupi, ambaye anatenda kwa wokovu wetu. Kiukweli, kama vile jua linavyofanya giza na mwezi kuacha kuangaza na nyota kuanguka kutoka angani, inasema Injili, “watamwona Mwana wa Adamu akija juu ya mawingu akiwa na nguvu nyingi na utukufu”; naye “atawakusanya wateule wake kutoka pepo nne, toka mwisho wa dunia hata mwisho wa mbingu” (rej. Mk 13 26-27).

Na kwa maneno haya, Yesu kwanza kabisa anaonesha kifo chake ambacho kitatukia muda mfupi baadaye. Juu ya Kalvari, kiukweli, jua litatiwa giza, na giza litashuka juu ya ulimwengu; lakini wakati huo huo Mwana wa Adamu atakuja juu ya mawingu, kwa sababu nguvu ya ufufuko wake itavunja minyororo ya kifo, uzima wa milele wa Mungu utafufuka kutoka gizani na katika ulimwengu mpya utazaliwa kutoka kwenye vifusi vya historia iliyojeruhiwa na uovu. Papa Francisko amesisitiza kwamba, hili ndilo tumaini ambalo Yesu anataka kutupatia. Na pia anafanya hivyo kupitia picha nzuri: tazama mtini - anasema - kwa sababu "tawi lake linapokuwa laini na majani yanaonekana, ina maana kwamba wakati wa joto umekaribia" (Mk 13, 28). Vivyo hivyo, sisi pia tunaitwa kusoma hali za maisha yetu ya kidunia: ambapo inaonekana kuna ukosefu wa haki tu, maumivu na umaskini, hasa katika wakati huu wa kushangaza, Bwana anakaribia kutuweka huru, anakaribia kutuweka huru kutoka utumwani na kufanya maisha yang'ae (Mk 3, 29).

Siku ya Maskini duniani
Siku ya Maskini duniani

Naye anakuwa karibu na ukaribu wetu wa Kikristo, na udugu wetu wa Kikristo. Sio juu ya kutupa sarafu mikononi mwa yule anayehitaji. Hu ninamuuliza mtu anayetoa sadaka mambo mawili: “Je, unagusa mikono ya watu au unatupa sarafu bila kuwagusa? Unatazama machoni mwa mtu unayemsaidia au unatazama pembeni?.... Sisi ni wanafunzi wake, ambao kwa shukrani kwa Roho Mtakatifu tunaweza kupanda tumaini hili ulimwenguni. Sisi ndio tunaweza na lazima tuwashe taa za haki na mshikamano wakati vivuli vya ulimwengu uliofungwa vikikusanyika (Rej. Waraka wa Kitume wa Fratelli tutti, 9-55). Ni sisi ambao Neema yake inatuangazia, ni maisha yetu yaliyochanganyika na huruma na mapendo ambayo huwa ishara ya uwepo wa Bwana, daima karibu na mateso ya maskini, ili kutuliza majeraha yao na kubadilisha hatima yao. Papa Francisko amesisitiza kwamba “tusisahau: Tumaini la Kikristo, ambalo lilitimizwa katika Yesu na kutimizwa katika Ufalme wake, linatuhitaji, linahitaji kujitolea kwetu, linahitaji imani tendaji katika upendo, linahitaji Wakristo ambao hawawaangalii njia nyingine.” Papa amesimulia kisa kimoja kuwa: “nilikuwa nikitazama picha iliyopigwa na mpiga picha wa Kirumi: Wanandoa walioelemika walikuwa wakitoka nje ya mgahawa, wakapitia karibu na mzee, wakati wa majira ya baridi kali; kwa mwanamke aliyefunikwa vizuri na manyoya na mwanamume pia; lakini mlangoni, kulikuwa na mwanamke maskini, amelala chini, akiomba sadaka na wote wawili walikuwa wakitazama upande mwingine ... Hii hutokea kila siku.

Kwaya iliyoimba katika maadhimisho ya misa takatifu
Kwaya iliyoimba katika maadhimisho ya misa takatifu

Hebu tujiulize: je, mimi hutazama upande mwingine ninapoona umaskini, mahitaji, maumivu ya wengine? Mtaalimungu wa karne ya ishirini alisema kwamba imani ya Kikristo ni lazima itengeneze ndani yetu "uaminifu wa kisiri na mtazamo wazi", sio hali ya kiroho inayokimbia kutoka kwa ulimwengu, lakini - kinyume chake - imani inayofungua mitazamo yetu kwa mateso ya ulimwengu na mateso ya dunia kutokuwa na furaha kwa maskini ili kutekeleza huruma ile ile ya Kristo. Je! ninahisi huruma kama ya Bwana kwa maskini, kwa wale ambao hawana kazi, ambao hawana chochote cha kula, ambao wametengwa na jamii? Na ni lazima si tu kuangalia matatizo makubwa ya umaskini duniani, lakini kwa kidogo ambayo sisi sote tunaweza kufanya kila siku kwa mtindo wetu wa maisha, kwa makini na kutunza mazingira tunamoishi, kwa bidii ya kutafuta haki, na kushiriki bidhaa zetu na wale ambao ni maskini zaidi, kwa kujitolea kijamii na kisiasa kuboresha hali halisi inayotuzunguka. Inaweza kuonekana kama kitu kidogo kwetu, lakini kidogo chetu kitakuwa kama majani ya kwanza yanayochipuka mtini, kidogo chetu kitakuwa kionjo cha kiangazi kinachokaribia sasa."

Papa ameongeza, katika Siku hii ya Maskini Duniani napenda kukumbuka onyo kutoka kwa Kardinali Martini. Alisema kwamba ni lazima tuwe waangalifu kufikiri kwamba kwanza kuna Kanisa, ambalo tayari ni imara ndani yake, na kisha maskini tunaowachagua kuwatunza. Kwa uhalisia, tunakuwa Kanisa la Yesu kwa kadiri ya kuwatumikia maskini, kwa sababu ni kwa njia hii tu “kanisa “linakuwa” lenyewe, yaani, Kanisa linakuwa makao yaliyo wazi kwa wote, mahali pa huruma ya Mungu kwa ajili ya watu wote. maisha ya kila mtu» ( C.M. MARTINI, Mji usio na kuta. Barua na hotuba kwa dayosisi 1984, Bologna 1985, 350). Nami naliambia Kanisa, naiambia serikali, ninasema kwa mashirika ya kimataifa, nasema kwa kila mmoja na kila mtu: tafadhali, tusiwasahau maskini." Alihitimisha Papa Francisko.

mahubiri ya Papa Siku ya Maskini Duniani 2024
17 November 2024, 11:09