2024.10.20 Wakati wa kutangaza watakatifu wapya tarehe 20 Oktoba 2024 2024.10.20 Wakati wa kutangaza watakatifu wapya tarehe 20 Oktoba 2024   (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Papa Francisko:kila Novemba 9 Majimbo yawakumbuke Watakatifu,Wenyeheri&Watumishi wa Mungu!

Katika Barua iliyotolewa tarehe 16 Novemba 2024 ambayo Papa Fransisko anaalika kila Kanisa mahalia kugundua tena na kudumisha,katika tarehe moja,kumbukumbu ya watu maalum wa imani ambao wamebainisha njia ya Kikristo na hali ya kiroho ya mahalia.Kwa lengo hili,Mabaraza ya Maaskofu yataweza kuendeleza na kupendekeza ishara za kichungaji.

Na Angella Rwezaula – Vatican.

Makanisa mahalia, kuanzia Jubilei ijayo ya 2025, yote yanaalikwa kukumbuka na kuheshimu tarehe za utakatifu ambazo zimebainisha njia ya Kikristo na hali ya kiroho mahalia, kila mwaka ifikapo tarehe 9 Novemba, ambayo mama Kanisa anaadhimisha Sikukuu ya Kutabaruku  Basilika ya Mtakatifu Yohane huko Laterano. Baba Mtakatifu Francisko amethibitisha hilo katika Barua iliyotolewa  tarehe 16 Novemba 2024.

Ifuatayo ni barua ya Baba Mtakatifu Francisko:

Kwa Waraka wa Kitume Gaudete et exsultate nilitaka kupendekeza mwito wa ulimwengu wote wa utakatifu kwa wanafunzi waaminifu wa Kristo katika ulimwengu wa sasa. Ni kitovu cha mafundisho ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican, ambao ulikumbuka kwamba “wale wote wanaomwamini Kristo, kwa hadhi yoyote au cheo chochote, wanaitwa kwenye utimilifu wa maisha ya Kikristo na utimilifu wa mapendo” (LG, 40). Sote tunaitwa, basi, kukaribisha upendo wa Mungu ambao “umekwisha kumiminwa katika mioyo yetu na Roho Mtakatifu” (Warumi 5:5). Kwa hakika, utakatifu, badala ya kuwa tunda la jitihada za kibinadamu, unamaanisha kutoa nafasi kwa ajili ya utendaji wa Mungu. Kila mtu anaweza kutambua katika watu wengi aliokutana nao njiani, mashuhuda wa fadhila za Kikristo, hasa imani, matumaini na mapendo: wanandoa ambao wameishi upendo wao kwa uaminifu kwa kujifungulia maisha; wanaume na wanawake ambao katika kazi mbalimbali walitegemeza familia zao na kushirikiana katika kueneza Ufalme wa Mungu; vijana na wanafunzi waliomfuata Yesu kwa shauku; wachungaji ambao kwa huduma wamemimina karama za neema juu ya watu watakatifu wa Mungu; wanaume na wanawake watawa ambao kwa kuishi mashauri ya kiinjili walikuwa taswira hai ya Kristo mchumba. Hatuwezi kuwasahau maskini, wagonjwa, wanaoteseka ambao katika udhaifu wao walipata kuungwa mkono na Bwana Mungu. Ni ule utakatifu wa “siku ya juma” na “mlango wa karibu”  ambao Kanisa ulimwenguni kote limekuwa tajiri kila wakati. Tunaalikwa kujiachilia kuchochewa na mifano hii ya utakatifu, ambayo kati yao wanajitokeza kwanza kabisa mashahidi waliomwaga damu yao kwa ajili ya Kristo na wale waliotangazwa kuwa wenyeheri na kutangazwa kuwa watakatifu kwa kuwa mifano ya maisha ya Kikristo na waombezi wetu.

Basi na tuwafikirie Waheshimiwa, wanaume kwa wanawake ambao utendaji wao wa kishujaa wa wema umetambuliwa, wa wale ambao katika hali za pekee wamefanya uwepo wao kuwa sadaka ya upendo kwa Bwana na kwa ndugu zao, na kwa Watumishi wa Mungu ambao Baraza la Kipapa la Kuwatangaza mwenyeheri na kutangazwa kuwa mtakatifu zinaendelea. Taratibu hizi zinaonesha jinsi gani ushuhuda wa utakatifu ulivyo katika nyakati zetu ambapo mashuhuda wakuu wa imani wanang'aa kama nyota (rej. Flp 2:15), ambao wameweka alama ya uzoefu wa Makanisa mahalia na, wakati huo huo, wamerutubisha historia. Hawa wote ni marafiki zetu, wasafiri, ambao hutusaidia kutambua kikamilifu wito wa ubatizo na kutuonesha uso mzuri zaidi wa Kanisa, ambalo ni takatifu na ni mama wa Watakatifu. Wakati wa mwaka wa liturujia Kanisa huwaheshimu hadharani Watakatifu na Wenyeheri kwa tarehe na njia zilizowekwa kabla. Hata hivyo, inaonekana kwangu ni muhimu kwamba Makanisa yote mahalia  yawakumbuke Watakatifu na Wenyeheri pamoja na Waheshimiwa na Watumishi wa Mungu wa maeneo yao, na kwa tarehe moja. Si suala la kuingiza ukumbusho mpya katika kalenda ya kiliturujia, bali ni kukuza  mipango ifaayo nje ya liturujia, au kukumbuka ndani yake, kwa mfano katika mahubiri au wakati mwingine unaoonekana kufaa, wale watu ambao wamejitambulisha wakristo kwa  njia na ndani ya roho.

Kwa hiyo, nayaomba Makanisa mahalia, kuanzia Jubilei ijayo ya 2025, kukumbuka na kuheshimu kumbukizi hizi za utakatifu, kila mwaka ifikapo tarehe 9 Novemba, ikiwa ni Sikukuu ya Kutabaruku Basilica ya Laterano. Hii itaruhusu jumuiya binafsi za kijimbo kugundua tena au kuendeleza kumbukumbu ya wanafunzi wa ajabu wa Kristo ambao waliacha ishara hai ya uwepo wa Bwana mfufuka na bado ni viongozi salama leo katika safari ya pamoja kuelekea kwa Mungu, wakilinda na kutuunga mkono. Kwa maana hiyo, ishara na miongozo ya kichungaji inaweza, ikiwezekana kuendelezwa na kupendekezwa na Mabaraza ya Maaskofu. Watakatifu, ambao ndani yao maajabu ya neema ya kimungu yenye pande nyingi yatuangaze, watusukume kwa ushirika wa karibu zaidi na Mungu na kututia moyo na hamu ya mji ujao wa kuimba pamoja nao sifa zake Aliye Juu.

Papa:9 Novemba kumbukizi ya watakatifu katika majimbo

 

16 November 2024, 15:21