Sala ya Papa kabla ya baraka ya mwisho:'Uwafariji wanaoomboleza wapendwa wao'
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Baba Mtakatifu alitoa maombi kabla ya Baraka ya mwisho, mara baada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kuombea Marehemu wote, katika siku ya kumbukizi yao, akiwa katika makaburi ya Laurentino jijini Roma tarehe 2 Novemba 2024. Papa Francisko ameanza na sala hivi: “Katika kutembelea makaburi, mahali pa kupumzikia kaka na dada zetu waliofariki, tunapyaisha imani yetu kwa Kristo ambaye alikufa, kuzikwa na kufufuka tena kwa ajili ya wokovu wetu. Hata miili ya kufa itaamka siku ya mwisho, na wale ambao wamelala katika Bwana watashirikishwa naye katika ushindi juu ya kifo. Kwa uhakika huu, tunainua maombi yetu ya pamoja ya haki na baraka kwa Baba.
Baba Mtakatifu Francisko ameendelea na sala kuwa "Uhimidiwe Mungu, Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo, ambaye kwa rehema zake nyingi alituzaa mara ya pili ili tupate tumaini lenye uzima kwa kufufuka kwake Yesu Kristo katika wafu; tupate na urithi usioharibika, usio na uchafu, usionyauka, uliotunzwa mbinguni kwa ajili yenu. (taz1Petro 1). 3-4). Usikie maombi tunayokuelekea kwa ajili ya wapendwa wetu wote ambao wameuacha ulimwengu huu. Uwaunge mikono ya huruma yako na uwapokee katika kusanyiko tukufu la Yerusalemu takatifu. Uwafariji wale walio katika maumivu ya kuondoka kwao kwa uhakika kwamba wafu wanaishi ndani yako na kwamba hata miili, iliyokabidhiwa duniani, siku moja itashiriki katika ushindi wa Pasaka ya Mwanao. Wewe, uliyemweka Bikira Maria kuwa ishara nyororo kwenye njia ya Kanisa, kwa maombezi yake usaidie imani yetu, ili kusiwe na kizuizi chochote kinachotufanya kukengeuka kutoka katika njia iendayo kwako, ambayo ni utukufu usio na mwisho. Kwa njia ya Kristo Bwana Wetu. Amina.