Tafuta

Siku ya vijana Duniani kwa ngazi ya kijimbo tarehe 24 Novemba 2024 sambamba na Siku kuu ya Kristo Mfalme. Siku ya vijana Duniani kwa ngazi ya kijimbo tarehe 24 Novemba 2024 sambamba na Siku kuu ya Kristo Mfalme.  (JOAOLC \ GMG Lisboa 2023 / João Lopes Cardoso)

Siku ya vijana:mwaliko wa Papa kutembea kiroho kuelekea Jubilei 2025!

Wale wanaomtumaini Bwana watapiga mbio wala hawatachoka ndiyo kauli mbiu ya Ujumbe wa Papa Francisko kwa Siku ya Vijana Duniani kwa Ngazi ya Majimbo inayoadhimishwa tarehe 24 Novemba 2024,sanjari na Shere za Kristo Mfalme:Huo ni mwito wa mada za safari ya hija na matumaini.Papa anawahimiza vijana kuadhimisha katika makanisa mahalia ulimwenguni pote kwa mtazamo wa moyo unaoelekeza Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya 2025.

Na Angella Rwezaula – Vatican.

Kama sehemu ya Maandalizi ya Jubilei ya Mwaka 2025 ambayo inaongozwa na kauli mbiu: Peregrinantes in spem yaani: Mahujaji wa Matumaini, mnamo tarehe 17 Septemba 2024, Baba Mtakatifu Francisko alitoa Ujumbe kwa ajili ya madhimisho ya Siku ya XXXIX ya Vijana kwa Ngazi ya Kijimbo Duniani kote katika  kuadhimishwa tarehe 24 Novemba 2024 sanjari na Mama Kanisa kuadhimisha Siku Kuu ya Kristo Mfalme wa Ulimwengu. Ujumbe huo unaongozwa na Kauli mbiu: “Wale wanaomtumainia Bwana, watapiga mbio, wala hawatachoka” (Is 40,31). Baba Mtakatifu kwa hiyo alibainisha kuwa mwaka 2023, tulianza safari ya matumaini kuelekea Jubilei kwa kutafakari kielelezo cha Paulo kisemacho: “Furaha na matumaini”(Rm 12,12). Ni hasa katika kujiandalia hija ya Jubilei ya 2025, mwaka huu, tunajikita kuongozwa na Nabii Isaya ambaye anabainisha kuwa “"Wale wanaomtumaini Bwana watapiga mbio wala hawatachoka" (taz. Is 40:31).

Mwanzo wa hatua mpya ya matumaini

Kielelezo hiki kinatolewa katika kitabu kiitwacho faraja kuanzia (Is 40-55), ambapo inatangazwa mwisho wa uhamisho wa Waisraeli huko Babiblonia na mwanzo wa hatua moja ya matumaini na kuzaliwa upya kwa watu wa Mungu ambao sasa wanaweza kurudi makwao, shukrani kwa njia mpya ambayo katika historia,, Bwana anafungulia watoto wake (Is 40,3). Baba Mtakatifu anabainisha kuwa hata sisi, tunaishi katika nyakati zenye hali ya majanga, ambayo yanazaa, kupotea na kuzuia kutazama wakati ujao kwa roho tulivu: kuanzia janga la vita, ukosefu wa haki kijamii, ukosefu wa usawa, njaa, unyonyaji wa kuwa mwanadamu na uumbaji. Mara nyingi wanaolipa gharama kubwa ni vijana kama wao, ambao wanahisi kutokuwa na msimamo wa wakati ujao na bila kuona njia ya kupitisha ndoto zao, kwa kuhatarisha kuishi nammna isiyo na tumaini, wafungwa wa uchovu, hali ya huzuni, wakati mwingine kuvutwa kwenye udanganyifu wa uvunjaji sheria na hali halisi haribifu (tazama Hati ya Spes non confundit, 12). Kwa sababu hiyo Papa Francisko amependa kama ilivyotokea kwa Israeli huko Babeli, tangazo la tumaini lingeweza kuwafikia wote hao pia vijana kwa sababu: hata leo “Bwana anafungua njia mbele yenu na kuwaalika kuifuata kwa furaha na matumaini.” Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake amefafanua vifungu 4 ambapo kwanza ni Hija ya maisha na changamoto zake, pili hija katika jangwa, tatu, kutoka watalii kuwwanahija na hatimaye  nne, hija ya tumaini kwa ajili ya utume

1. Hija ya maisha na changamoto zake

Isaya anatabiri “kutembea bila kuchoka. Hebu basi tutafakari juu ya vipengele hivi viwili: kutembea na uchovu. Maisha yetu ni hija, safari inayotusukuma kupita sisi wenyewe, safari ya kutafuta furaha; na maisha ya Kikristo, hasa, ni hija kuelekea kwa Mungu, wokovu wetu na utimilifu wa mema yote. Malengo, ushindi na mafanikio njiani, ikiwa yatabaki nyenzo tu, baada ya wakati wa kwanza wa kuridhika bado hutuacha na njaa, tukitamani maana ya kina; kwa hakika haziridhishi kabisa nafsi zetu, kwa sababu tuliumbwa na Yeye asiye na kikomo na, kwa hiyo, ndani yetu huishi hamu ya upitaji maumbile, hali ya kutotulia inayoendelea kuelekea utimilifu wa matamanio makubwa zaidi, kuelekea zaidi. Kwa sababu hiyo, nilivyowaambia mara nyingi, “kutazama maisha kutoka kwenye balcony hakuwezi kuwatosha ninyi vijana.” Hili huleta huzuni, huku tunaishi katika wasiwasi wa harakati tupu ambayo hutuongoza kujaza siku zetu na mambo elfu moja na, licha ya hili, kuwa na hisia ya kutoweza kufanya vya kutosha na kutowahi kufikia kiwango. Uchovu mara nyingi huongezwa kwa uchovu huu.

Vijana wasio amua na wala kuchafua mikono yao

Ni juu ya hali hiyo ya kutojali na kutoridhika kwa wale ambao hawaendi, hawaamui, hawachagui, hawajihatarishi na wanapendelea kubaki katika eneo lao la faraja, wamejifungia wenyewe, wakiona na kuhukumu ulimwengu kutoka nyuma ya skrini, bila kamwe “kuchafua mikono yako" na shida, na wengine, na maisha. Uchovu wa aina hii ni sawa na saruji ambayo miguu yetu inatumbukizwa ndani yake, ambayo hatimaye hutufanya kuwa migumu, hutulemea, hutulemaza na kutuzuia kusonga mbele. Papa amesema “Napendelea uchovu wa wale wanaotembea kuliko uchovu wa wale ambao wametulia na hawana hamu ya kutembea!” Suluhisho la uchovu, kwa kushangaza, sio kukaa tuli kupumzika. Bali ni kufunga safari na kuwa mahujaji wa matumaini. Huu ndio mwaliko wangu kwenu: tembea kwa matumaini! Tumaini hushinda kila uchovu, kila shida na kila wasiwasi, ikikupatia motisha kubwa ya kusonga mbele, kwa sababu ni zawadi ambayo tunapokea kutoka kwa Mungu mwenyewe: Yeye hujaza wakati wetu kwa maana, hutuangazia njia, hutuonesha mwelekeo na lengo la maisha.

Mfano wa wanariadha katika uwanja ili kupokea tuzo

Mtume Paulo alitumia mfano wa mwanariadha katika uwanja ambaye anakimbia ili kupokea tuzo ya ushindi (Taz 1 Kor 9:24). Wale ambao mmeshiriki katika mashindano ya michezo - sio kama mtazamaji lakini kama mhusika mkuu - mnajua vyema nguvu ya ndani inayohitajika ili kufikia mstari wa mwisho. Tumaini ni nguvu mpya ambayo Mungu hutia ndani yetu, ambayo huturuhusu kudumu katika mbio, ambayo huturuhusu kuwa na "mtazamo mrefu" ambao unapita zaidi ya shida za sasa na hutuelekeza kuelekea lengo fulani la ushirika na Mungu na utimilifu wa uzima wa milele. Ikiwa kuna lengo zuri, ikiwa maisha hayaendi popote, ikiwa hakuna chochote ninachoota, kupanga na kufikia kitapotea, basi inafaa kutembea na jasho, kuvumilia vizuizi na kukabiliana na uchovu, kwa sababu malipo ya mwisho ni ya ajabu!

2.Mahujaji jangwani

Katika hija ya maisha bila shaka kutakuwa na changamoto za kukabiliana nazo. Katika nyakati za kale, katika safari ndefu zaidi, mtu alipaswa kukabiliana na mabadiliko ya misimu na mabadiliko ya hali ya hewa; kuvuka majira mazuri na ya  baridi, lakini pia milima, theluji na jangwa kali. Kwa hiyo, hata kwa wale ambao ni wamini, hija ya maisha na safari ya kuelekea mahali pa mbali bado inachosha, kwani safari ya jangwani kuelekea Nchi ya Ahadi ilikuwa ya watu wa Israeli. Hivi ndivyo ilivyo kwenu nyote. Hata kwa wale ambao wamepokea zawadi ya imani, kumekuwa na nyakati za furaha ambapo Mungu alikuwapo na ukahisi kuwa yuko karibu, na nyakati zingine ambazo ulipitia jangwa. Inaweza kutokea kwamba shauku ya awali katika masomo au kazi, au msukumo wa kumfuata Kristo - iwe katika ndoa, katika ukuhani au katika maisha ya wakfu - kufuatiwa na wakati wa shida, ambayo hufanya maisha kuonekana kama safari kuwa ngumu katika jangwa. Nyakati hizi za shida, hata hivyo, si nyakati za kupita au zisizo na maana, lakini zinaweza kuthibitisha kuwa fursa muhimu za ukuaji. Hizi ni nyakati za utakaso wa matumaini! Katika migogoro, kwa kweli, "matumaini" mengi ya uwongo hupotea, yale madogo sana kwa mioyo yetu; zimefunuliwa na, kwa hivyo, tunabaki uchi na sisi wenyewe na kwa maswali ya msingi ya maisha, zaidi ya udanganyifu wowote.  

Na katika wakati huo, kila mmoja wetu anaweza kujiuliza: juu ya matumaini gani ninaweka maisha yangu? Je, ni kweli au ni udanganyifu? Katika nyakati hizi, Bwana hatutupi; anakuja karibu na ubaba wake na daima hutupatia mkate ambao hututia nguvu tena na kuturudisha kwenye njia. Tunakumbuka kwamba alitoa mana kwa watu wa jangwani (taz Kutoka 16) na kwa nabii Eliya, akiwa amechoka na amevunjika moyo, mara mbili alitoa mkate na maji ili aweze kutembea kwa "siku arobaini mchana na usiku hadi mlimani kwa Mungu, 'Horebu' (Taz. 1 Wafalme 19:3-8). Katika historia hizi za kibiblia, imani ya Kanisa imeona vielelezo vya zawadi ya thamani ya Ekaristi, mana ya kweli na viaticum ya kweli, ambayo Mungu anatupa ili kututegemeza katika safari yetu. Kama Mwenyeheri Carlo Acutis alivyosema, Ekaristi ni njia kuu ya kwenda mbinguni. Ni kijana aliyeifanya Ekaristi kuwa tukio lake muhimu zaidi la kila siku! Hivyo, tukiwa tumeunganishwa kwa ukaribu na Bwana, tunatembea bila kuchoka kwa sababu Yeye hutembea nasi (taz. Mt 28:20). Ninawaalika mgundue tena zawadi kuu ya Ekaristi!"

Katika nyakati zisizoepukika za uchovu wa safari yetu ya hija katika ulimwengu huu, basi na tujifunze kupumzika kama Yesu na katika Yesu, ambaye anawapendekeza wanafunzi kupumzika baada ya kurudi kutoka katika utume (taz Mk 6:31), anatambua hitaji lenu la kupata, kupumzika katika mwili, wakati wa burudani zenu, kufurahia na marafiki, kucheza michezo na hata kulala. Lakini kuna pumziko la kina zaidi, pumziko la roho, ambalo wengi wanatafuta na wachache wanapata, ambalo linapatikana katika Kristo tu. Mjue kwamba uchovu wote wa ndani unaweza kupata kitulizo kwa Bwana, ambaye anawaambia: "Njooni kwangu, ninyi nyote msumbukao na wenye kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha" (taz.Mt 11:28). Uchovu wa safari unapowaelemea, mrudi kwa Yesu, mjifunze kutulia ndani yake na kubaki ndani yake, kwani "wale wanaomtumaini Bwana [...] hutembea bila kuchoka" (Isa 40,31), Papa Francisko amekazia.

3: Kutoka kuwa watalii hadi mahujaji

Wapendwa vijana, mwaliko ninaowaelekezea ni wa kuanza safari, kugundua maisha, katika njia ya upendo, katika kuutafuta uso wa Mungu, lakini ninachopendekeza kwenu ni hiki: kuanza safari si kama watalii tu, bali kama mahujaji. Hiyo ni, kutembea kwako kusiwe tu unapita katika maeneo ya maisha kwa njia ya juujuu tu, bila kushika uzuri wa kile unachokutana nacho, bila kugundua maana ya barabara zinazosafirishwa, kunasa muda mfupi, uzoefu wa muda mfupi wa kusasishwa kwenye selfie. . Mtalii anafanya hivi. Hujaji, kwa upande mwingine, hujizamisha kwa moyo wote katika maeneo anayokutana nayo, huwafanya waongee, huwafanya kuwa sehemu ya utafutaji wake wa furaha. Hija ya Jubilei, basi, inalenga kuwa ishara ya safari ya ndani ambayo sisi sote tumeitwa kuifanya, kufikia hatima ya mwisho. Kwa mitazamo hii, sote tunajitayarisha kwa Mwaka wa Jubilei. Natumaini kwamba kwa wengi wenu itawezekana kuja Roma kwa hija ya kuvuka Milango Mitakatifu.

Kwa kila mtu, kwa vyovyote vile, kutakuwa na uwezekano wa kufanya hija hii pia katika Makanisa mahususi, ili kuibua upya madhabahu mengi mahalia yanayohifadhi imani na uchaji wa watu watakatifu na waaminifu wa Mungu. Na ni matumaini yangu kwamba hija hii ya Jubilei itakuwa kwa kila mmoja wetu "wakati wa kuishi na kukutana kibinafsi na Bwana Yesu, "Mlango wa wokovu." Niwasihi muishi kwa mitazamo mitatu ya kimsingi: shukrani, ili moyo wenu ufunguke kusifu kwa zawadi mlizopokea, kwanza kabisa zawadi ya uzima; utafiti, ili safari idhihirishe hamu ya kudumu ya kumtafuta Bwana na sio kuzima kiu ya moyo; na, hatimaye, toba, ambayo inatusaidia kuangalia ndani yetu wenyewe, kutambua njia mbaya na chaguzi ambazo sisi wakati mwingine tunachukua na hivyo, kuweza kugeuka kwa Bwana na kwa mwanga wa Injili yake.

4. Mahujaji wa matumaini kwa ajili ya utume

Ninawachia picha nyingine ya kupendekeza kwa safari yenu. Mkifika kwenye Basilika ya Mtakatifu Petro, Roma, mtavuka Uwanja ambao umezungukwa na nguzo zilizoundwa na mbunifu mkuu na mchongaji wa sanamu, Gian Lorenzo Bernini. Nguzo, kwa ujumla wake, zinaoonekana kama kumbatio kubwa, ni mikono miwili iliyo wazi ya Kanisa, mama yetu, anayewakaribisha watoto wake wote! Katika Mwaka huu Mtakatifu wa Matumaini, ninawaalika ninyi nyote kuonja kukumbatiwa na Mungu wa huruma, kupata msamaha wake, ondoleo la "deni zetu zote za ndani", kama ilivyokuwa desturi katika Jubile za Biblia. Na kwa hivyo, mkikaribishwa na Mungu na kuzaliwa upya ndani Yake, ninyi pia mnakuwa mikono wazi kwa marafiki na rika zenu, wengi wanaohitaji kuhisi, kupitia kukaribishwa kwenu upendo wa Mungu Baba. Kila mmoja wenu atoe "hata tabasamu tu, ishara ya urafiki, sura ya kidugu, kusikiliza kwa dhati, huduma ya bure, mkijua kwamba, katika Roho wa Yesu, hii inaweza kuwa mbegu yenye matunda ya tumaini kwa wale wanaoipokea na hivyo kuwa wamisionari wasiochoka wa furaha.

Baba Mtakatifu Francisko akihitimisha amebainisha kuwa: "Wakati tukitembea, tuinue mitazamo, kwa macho ya imani, kuelekea watakatifu waliotangulia katika safari ambao walifika hatima na wanatutia moyo wao wa ushuhuda wakisema: ”Nimevipiga vita vilivyo vizuri, mwendo nimeumaliza, Imani nimeilinda; baada ya hayo nimewekewa taji ya haki, ambayo Bwana, mhukumu mwenye haki, atanipa siku ile; wala si mimi tu, bali na watu wote pia waliopenda kufunuliwa kwake (2Tm 4,7-8)." Mfano wa watakatifu wa kike na kiume wanatuvuta na kutusaidia. Kuweni jasiri. Papa amewakikishia anavyowapeleka moyoni mwake na kuwakabidi kila mmoja kwa Bikira Maria ili kwa mfano wake waweze kusubiri kwa uvumilivu na imani kile ambacho wanatagemea. Kwa kubaki katika mwendo kama wanahitaji  wa matumaini na upendo.

Ujumbe wa Siku ya vijana Kjimbo
23 November 2024, 16:04