Tafuta

Baba Mtakatifu Francisko anasema, hulka ya Kisinodi inapaswa pia kukita mizizi yake katika maisha ya ndoa na familia. Baba Mtakatifu Francisko anasema, hulka ya Kisinodi inapaswa pia kukita mizizi yake katika maisha ya ndoa na familia.  (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Sinodi ya XVI ya Maaskofu: Ujumbe Kwa Watu wa Ndoa na Familia: Majadiliano!

Baba Mtakatifu Francisko anasema, hulka ya Kisinodi inapaswa pia kukita mizizi yake katika maisha ya ndoa na familia; kwa kujenga na kudumisha utamaduni wa kujadiliana katika ukweli na uwazi. Wakati mwingine si rahisi sana anasema Papa Francisko kujadiliana ndani ya familia, lakini, jitihada za makusudi lazima zifanyike ili kujenga na kudumisha utamaduni wa majadiliano. Familia isiyojadiliana, hiyo ni familia ambayo imekufa. Familia: Kanisa la Kisinodi na Kimisionari.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mama Kanisa tangu mwanzo amekuwa akitoa kipaumbele cha pekee katika maisha na utume wa ndoa na familia, kwa kutambua kwamba, Familia ni Kanisa dogo la nyumbani, shule ya upendo, huruma, haki na ukarimu. Ni mahali patakatifu ambapo tunu msingi za maisha ya kiroho, kiutu, kitamaduni na kijamii zinarithishwa, tayari kuunda jamii inayowajibikiana na kutegemezana. Huu ndio mwelekeo wa pekee uliotolewa na Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican, changamoto inayofanyiwa kazi na Baba Mtakatifu Francisko, ili kweli familia ziweze kuwa ni mashuhuda wa Injili ya familia, kielelezo cha ukomavu wa imani. Mama Kanisa anawahimiza waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuhakikisha kwamba, kweli wanakuwa ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya Ndoa na Familia, kwa kutangaza na kushuhudia: Ukuu, ukweli, uzuri, utakatifu na dhamana ya maisha ya ndoa na familia katika jamii. Lakini, familia katika ulimwengu mamboleo inakabiliwa na changamoto pevu kama zilivyoainishwa na Baba Mtakatifu Francisko katika Wosia wake wa Kitume, “Amoris laetitia” yaani “Furaha ya upendo ndani ya familia.”

Familia ni Kanisa dogo la nyumbani, Kanisa la Kisinodi na Kimisionari
Familia ni Kanisa dogo la nyumbani, Kanisa la Kisinodi na Kimisionari

Injili ya Kristo ni chemchemi inayowapatia wanafamilia ari, nguvu na jeuri ya kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa watu wa nyakati hizi kwa kuzingatia tunu msingi za Injili ya familia mintarafu Mafundisho ya Kanisa. Baba Mtakatifu Francisko katika Wosia wake wa Kitume, “Amoris laetitia” yaani “Furaha ya upendo ndani ya familia” anagusia uwepo angavu wa Kristo Yesu ambaye hukaa katika familia halisi na imara, pamoja na shida na mahangaiko yao yote ya kila siku, furaha na matumaini yao. Familia ni amana na utajiri mkubwa katika maisha na utume wa Kanisa. Huu ni wakati muafaka wa kutangaza na kushuhudia familia kuwa ni Kanisa dogo la nyumbani, linalojengwa na kuimarishwa na wanandoa wenyewe katika uhalisia wa maisha yao ya kila siku kwa kutambua kwamba, Kristo Bwana, yuko daima pamoja nao! Huu ni muda muafaka wa kufanya mazoezi na kumwilisha Injili ya huruma, upendo na msamaha. Ni wakati wa kukaa pamoja na wanafamilia ili kukazia malezi bora na utu wema.

Familia zijenge utamaduni wa kusikilizana na kujadiliana katika ukweli na uwazi
Familia zijenge utamaduni wa kusikilizana na kujadiliana katika ukweli na uwazi

Maadhimisho ya Sinodi ya XVI ya Maaskofu kuanzia mwaka 2021 hadi tarehe 27 Oktoba 2024, yamenogeshwa na kauli mbiu “Kwa Ajili ya Kanisa la Kisinodi: Umoja, Ushiriki na Utume.” Hati ya Sinodi ya XVI ya Maaskofu inasema, hulka ya Kanisa la Kisinodi na Kimisionari inafumbatwa katika toba na wongofu wa ndani. Huu ni mchakato unaokita mizizi yake katika wongofu wa mahusiano na mafungamano ya kijamii, kielelezo cha ufunuo wa huruma na upendo unaobubujika kutoka katika Fumbo la Utatu Mtakatifu. Baba Mtakatifu Francisko anasema, hulka ya Kisinodi inapaswa pia kukita mizizi yake katika maisha ya ndoa na familia; kwa kujenga na kudumisha utamaduni wa kujadiliana katika ukweli na uwazi. Wakati mwingine si rahisi sana anasema Baba Mtakatifu Francisko kujadiliana ndani ya familia, lakini, jitihada za makusudi lazima zifanyike ili kujenga na kudumisha utamaduni wa majadiliano. Familia isiyojadiliana, hiyo ni familia ambayo imekufa.

Familia ni msingi bora wa malezi na makuzi ya Kikristo
Familia ni msingi bora wa malezi na makuzi ya Kikristo

Kumbe, huu ni wakati wa kujenga na kudumisha utamaduni wa majadiliano katika ukweli na uwazi; kwa kusikilizana, kuheshimiana na kuthaminiana. Ni muda wa kuratibu vyema rasilimali muda kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya familia. Umefika wakati kwa wanandoa kuangaliana usoni bila kupepesa pepesa macho ili kujenga na kuimarisha upendo na urafiki wao wa dhati, daima wakimwachia nafasi Kristo Yesu. Mazoezi haya yasaidie kukuza na kudumisha tunu msingi za maisha ya kiroho na kiutu. Ni muda wa uinjilishaji wa kina, unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Ni wakati muafaka wa kusali na kutafakari pamoja Neno la Mungu, Liturujia ya Kanisa la nyumbani ipewe uzito na msukumo wa pekee, ili kuachana na tabia ya kufanya mambo kwa mazoea. Maisha ya familia yageuzwe kuwa ni Liturujia ya Ndoa kwa njia ya Sala zinazowashirikisha wanafamilia wote, kwa kugawana majukumu; kwa kusoma na kushirikishana tafakari ya Neno la Mungu; kwa kusali kwa ajili ya mahitaji msingi ya familia pamoja na Kanisa katika ujumla wake, bila kusahau kujiaminisha chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa.

Familia Kanisa Dogo la Nyumbani, Kanisa la Kisinodi na Kimisionari
Familia Kanisa Dogo la Nyumbani, Kanisa la Kisinodi na Kimisionari

Njia za mawasiliano ya jamii, ziwezeshe familia nyingi kuweza kuunganika kwa njia ya sala pamoja na kuwashirikisha watoto katika Liturujia hii ambayo inapaswa kuwa ni Liturujia shirikishi. Wanandoa wanakumbushwa kwamba Sakramenti hii ni kwa ajili ya kuwatakatifuza na kuwakomboa wanandoa. Kwa sababu hiyo, wanandoa ni ukumbusho wa daima kwa Kanisa juu ya kile kilichotokea Msalabani; nao ni mashuhuda wa wokovu wanaoushiriki kwa njia ya Sakramenti kila mmoja mbele ya mwenzake na watoto wao. Wanandoa ni mashuhuda wa: unabii na utangazaji wa Habari Njema ya Wokovu unaomwilishwa katika uhalisia wa maisha yao ya kila siku, kielelezo makini cha zawadi kama alivyofanya Kristo Yesu.

Sinodi Ujumbe kwa Familia
02 November 2024, 11:22