Ujumbe wa Papa kwa COP29:Ni lazima kufuta madeni ya nchi maskini
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Kadiri jamii inavyozidi kuwa ya utandawazi, ndivyo inatufanya kuwa majirani lakini haitufanyi kuwa ndugu. Maendeleo ya kiuchumi hayajapunguza ukosefu wa usawa. Kinyume chake, imependelea kipaumbele cha faida na maslahi maalum kwa gharama ya ulinzi wa wanyonge, na imechangia kuzorota kwa maendeleo ya matatizo ya mazingira. Haya na mengine yamo kwenye Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko kwa washiriki wa Mkutano wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi COP29 kuanzia tarehe 11 hadi 22 Novemba 2024. Ujumbe huo ulisomwa na Kardinali Pietro Parolin, Katibu wa Vatican, Jumatano tarehe 13 Novemba 2024 huko Baku nchini Azerbajain. Kwa niaba ya Baba Mtakatifu Francisko, Kardinali Parolin ameanza kutoa salamu kwa wote na kuwahakikishia ukaribu wake, msaada na faraja yake ili COP29 iweze kufanikiwa kudhihirisha kwamba kuna jumuiya ya kimataifa iliyo tayari kuangalia zaidi ya mambo fulani na kuweka kitovu cha mema ya ubinadamu na nyumba yetu ya pamoja, ambayo Mungu ameikabidhi kwa utunzaji na wajibu wetu.
Takwimu za kisayansi zinaonesha ucheleweshaji wa kuchukua hatua
Katika ujumbe huo Papa nabainisha kuwa “Data ya kisayansi inayopatikana kwetu hairuhusu ucheleweshaji wowote zaidi na inaweka wazi kwamba uhifadhi wa uumbaji ni mojawapo ya masuala ya dharura zaidi ya wakati wetu. Tunapaswa pia kutambua kwamba inahusiana kwa karibu na kulinda amani.” COP29 inajikita katika muktadha unaosababishwa na kuongezeka kwa kukatishwa tamaa na taasisi za kimataifa na mielekeo hatari ya kujenga kuta. Ubinafsi - mtu binafsi, wa kitaifa na wa vikundi vya nguvu – humwilisha hali ya kutoaminiana na migawanyiko ambayo haijibu mahitaji ya ulimwengu unaotegemeana ambamo tunapaswa kutenda na kuishi kama washiriki wa familia moja inayoishi katika kijiji kimoja cha ulimwengu kilichounganishwa. Baba Mtakatifu katika ujumbe wake uliosomwa na mwakilishi wake anabainisa kuwa "Kadiri jamii inavyozidi kuwa ya utandawazi, ndivyo inatufanya kuwa majirani lakini haitufanyi kuwa ndugu" Maendeleo ya kiuchumi hayajapunguza ukosefu wa usawa. Kinyume chake, imependelea kipaumbele cha faida na maslahi maalum kwa gharama ya ulinzi wa wanyonge, na imechangia kuzorota kwa maendeleo ya matatizo ya mazingira.
Matokeo mabaya ya maisha huathiri kila mtu:COP29 itafute suluhisho
Ili kubadili mwelekeo na kujenga utamaduni wa kuheshimu maisha na utu wa binadamu ni muhimu kuelewa kwamba matokeo mabaya ya mtindo wa maisha huathiri kila mtu na kuunda siku zijazo pamoja, "ili kuhakikisha kwamba ufumbuzi unapendekezwa kutoka katika mtazamo wa kimataifa, na sio tu kutetea maslahi ya nchi chache. Kanuni ya "jukumu la kawaida lakini tofauti na uwezo husika unaweza kuongoza na kuhamasisha kazi za majuma haya Papa anasisitiza. Anaomba “ majukumu ya kihistoria na ya sasa yawe ahadi madhubuti na za kutazamia mbele kwa siku zijazo, ili Lengo Jipya la Pamoja la Kutathminiwa kuhusu Fedha za Hali ya tabianchi, miongoni mwa mambo ya dharura zaidi ya Mkutano huu, liweze kuibuka kutoka kwa majuma haya ya kazi.” Juhudi zinapaswa kufanywa kutafuta suluhisho ambazo hazitadhoofisha zaidi maendeleo na uwezo wa kukabiliana na hali ya nchi nyingi ambazo tayari zimeelemewa na deni la kiuchumi. Wakati wa kujadili ufadhili wa hali ya tabianchi, ni muhimu kukumbuka kuwa deni la kiikolojia na deni la nje ni pande mbili za sarafu moja, kuweka rehani siku zijazo.
Kusamehe madeni kwa nchi maskini
Kwa mtazamo huo Kardinali Parolin amependa kusisitiza wito ambao Papa Francisko alioutoa kwa matazamio ya Jubilei ya Kawaida ya mwaka 2025, akiyataka mataifa tajiri zaidi "kwamba yatambue uzito wa maamuzi yao mengi ya zamani na kuamua kusamehe madeni" ya nchi ambazo hazitaweza kulipa. Zaidi ya suala la ukarimu, hili ni suala la haki. Inafanywa kuwa mbaya zaidi leo hii na aina mpya ya ukosefu wa haki ambayo tunazidi kutambua, yaani, kwamba "deni la kweli la kiikolojia" lipo, hasa kati ya Kaskazini na Kusini mwa dunia inayohusishwa na kukosekana kwa usawa wa kibiashara na athari kwa mazingira na matumizi yasiyo ya uwiano ya maliasili na baadhi ya nchi kwa muda mrefu.” Hakika, ni muhimu kutafuta usanifu mpya wa kimataifa wa kifedha ambao unazingatia binadamu, shupavu, bunifu na unaozingatia kanuni za usawa, haki na mshikamano. Usanifu mpya wa kifedha wa kimataifa ambao unaweza kweli kuhakikisha kwa nchi zote, hasa maskini zaidi na zile zilizo hatarini zaidi kwa majanga ya hali ya tabianchi, njia za maendeleo zenye kaboni ya chini na ugawanaji mwingi ambazo huwezesha kila mtu kufikia uwezo wake kamili na kuona utu wao unaheshimiwa.
Hebu tushirikiane kuhakikisha Cop29 inaimarisha sera za kisiasa
Tuna rasilimali za kibinadamu na za kiteknolojia za kubadilisha mkondo na kufuata mzunguko mzuri wa maendeleo fungamani ambao ni wa kibinadamu na jumuishi. Hebu tushirikiane ili kuhakikisha kwamba COP29 pia inaimarisha utashi wa kisiasa wa kuelekeza rasilimali hizi kuelekea lengo hili adhimu kwa manufaa ya pamoja ya binadamu leo na kesho. Tunapaswa kurejesha tumaini letu katika uwezo wa wanadamu kwamba «siku zote kuna njia ya kutoka, kwamba tunaweza kuelekeza hatua zetu kila wakati, kwamba tunaweza kufanya kitu kutatua shida zetu.” “Matumaini letu ni kwamba ubinadamu mwanzoni mwa karne ya ishirini na moja utakumbukwa kwa kubeba kwa ukarimu majukumu yake mazito."
Vatican inaunga mkono jitihada za uwanja wa elimu ya ikolojia shirikishi
Kardinali Parolin alisitiza tena kujitolea na uungwaji mkono wa Vatican katika jitihada hii, hasa katika uwanja wa elimu ya ikolojia shirikishi na katika kuongeza ufahamu wa mazingira kama “tatizo la kibinadamu na kijamii kwa idadi yoyote ya viwango” ambayo inahitaji zaidi ya yote dhamira ya wazi, ambayo wajibu, upatikanaji wa ujuzi na ushiriki wa kila mtu ni msingi. Hatuwezi “kupita na kutazama upande mwingine”. Kutojali ni mshiriki wa dhuluma. Kwa hivyo, Maombi yake ni kwamba kwa kuzingatia manufaa ya wote, tunaweza kufichua taratibu za kujihesabia haki ambazo mara nyingi hutulemaza: na kujiuliza je ninaweza kufanya nini? Ninawezaje kuchangia? Hakuna wakati wa kutojali leo hii. Hatuwezi kunawa mikono juu yake, kwa umbali, kwa kutojali, na kutopendezwa. Hii ndiyo changamoto halisi ya karne yetu. Kwa makubaliano kabambe, kwa kila hatua na mchakato unaolenga maendeleo fungamani Kardinali Parolin awawahakikishia msaada wake na wa Baba Mtakatifu ili kutoa huduma bora kwa wanadamu, ili sote tuchukue jukumu la kulinda sio tu yetu, yako ya baadaye, lakini ya wote.