Ujumbe wa Papa:wito wetu wa Kikristo ni upatanisho wa amani&kuwatunza ndugu
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Katika ujumbe wa Papa Francisko kwa washiriki wa Mkutano kuhusu “Ulinzi katika Kanisa Katoliki barani Ulaya” ulioandaliwa na Tume ya Kipapa kwa ajili ya kulinda wadogo kuanzia tarehe 13 hadi 15 Novemba 2024, katika Jumba la Maffei, Jijini Roma ambapo unawaona wataalamu zaidi ya 100 kutoka nchi 25 za Ulaya. Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe huo alianza kuwasalimu wote waliokusanyika kwa ajili Mkutano unaojishughulisha na utume muhimu wa kuwalinda watoto na watu wazima wanaoishi katika mazingira hatarishi ndani ya Kanisa. Kujitolea kwao kwa sababu hii ni ishara ya kuendelea kwa juhudi za Kanisa kulinda walio hatarini zaidi katikati yetu. Papa amesema wanapokutana pamoja kutoka nchi zaidi ya ishirini za Ulaya, ambazo baadhi yake zinakabiliwa na changamoto za vita na migogoro, amewakumbusha kuhusu wito wetu wa Kikristo wa kuwa wapatanishi wa amani na kuwatunza kaka na dada zetu wenye uhitaji.
Ushuhuda katika umoja na mshikamano unaovuka mipaka yote
Kwa hiyo uwepo wao ni ushuhuda fasaha wa umoja na mshikamano unaovuka mipaka yote. Mazungumzo na mabadilishano katika Kongamano lao yanatoa fursa za kuahidi kwa uelewa kamili na kujitolea zaidi kwa kulinda watoto na watu wazima walio hatarini ndani ya Kanisa. Ni matumaini ya Papa kwamba juhudi zao za kuanzisha mtandao wa watu na mazoea mazuri zitatoa jukwaa linalohitajika sana la kubadilishana maarifa, kusaidiana, na kuhakikisha kuwa mipango ya ulinzi ina ufanisi na endelevu. Kwa namna fulani, Papa Francisko pia amehimiza mipango iliyofanywa ili kutoa faraja na usaidizi kwa wale ambao wameteseka, kama ishara ya kujali kwa Kanisa kwa haki, uponyaji na upatanisho. Kwa uhakikisho wa maombi yake kwamba Mkutano huo utakuwa chanzo cha maarifa yenye manufaa, na kwamba mashauri yao yatachangia Kanisa salama na lenye huruma zaidi, amewambea vipawa vya Roho Mtakatifu vya hekima na nguvu, na kuwapa Baraka.