Jubilei Kuu ya Miaka 2025 ya Ukristo: Yesu Mlango wa Imani na Matumaini
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S., - Vatican.
Tamko la Maadhimisho ya Jubilei ya Mwaka 2025 ya Ukristo linanogeshwa na kauli mbiu “Spes non confundit" yaani “Tumaini halitahayarishi.” Rum 5:5 na kwamba, kiini cha maadhimisho haya ni matumaini yanayowawezesha watu waaminifu wa Mungu kutoka sehemu mbalimbali za dunia kufanya hija ya maisha ya kiroho mjini Roma sanjari na maadhimisho haya kufanyika kwenye Makanisa mahalia, ili kukutana na Kristo Yesu aliye hai na ambaye pia ni Mlango wa maisha na uzima wa milele. Baba Mtakatifu Francisko anasema, Maadhimisho ya Jubilei ya Mwaka 2025 ya Ukristo ni muda muafaka wa kukimbilia na kuambata huruma na upendo wa Mungu; kwa kuweka kando mizigo ya zamani, na kupyaisha msukumo kuelelea siku zijazo; ili kusherehekea uwezekano wa mabadiliko katika maisha, kwa kujitahidi kupyaisha utambulisho wao na kuwa jinsi walivyo, kwa njia ya imani, tayari kushuhudia ubora wao katika maisha ya kila siku. Makanisa na Madhehebu mbalimbali ya Kikristo yanajiandaa kuadhimisha Jubilei ya Miaka 1, 700 tangu Mtaguso wa Kwanza Nicea ulipoadhimishwa kunako mwaka 325 na kilele cha maadhimisho haya ni mwaka 2025, tukio la pekee na muhimu sana. Mwaka 2025 Wakristo wote wanaadhimisha Pasaka ya Bwana siku moja, matendo makuu ya Mungu kwa waja wake. Kanuni ya Imani ya Nicea-Constantinopoli ni formula rasmi ambayo ilipitishwa na Mababa wa Mtaguso wa Kwanza wa Nicea (325) ikakamilishwa na Mtaguso wa kwanza wa Konstantinopoli (381) ili kubainisha imani sahihi ya Kanisa Katoliki dhidi ya uzushi, hasa wa Ario na wafuasi wake. Katika mazingira hayo, lengo kuu lilikuwa kwanza kabisa ni kumkiri Kristo Yesu “Mungu kweli kwa Mungu kweli” yaani Mungu kweli sawa na Baba, halafu kwamba Roho Mtakatifu anastahili kuabudiwa pamoja na Baba na Mwana (Utatu Mtakatifu).
Wakristo wanataka kutembea pamoja na Kristo Yesu ambaye ni njia, ukweli na uzima. Watu wanamtafuta Kristo Yesu hata bila ya kutambua. Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kupita katikati ya Mlango wa Imani, sanjari na kutangaza na kushuhudia kanuni ya Imani ya Nicea. Kristo Yesu anasema “Mimi ndimi mlango; mtu akiingia kwa mimi, ataokoka; ataingia na kutoka, naye atapata malisho.” Rej. Yn 10: 1-18. Uzinduzi wa Maadhimisho ya Jubilei kuu ya Mwaka 2025 ya Ukristo umewahusisha wajumbe kutoka katika Makanisa na Madhehebu mbalimbali ya Kikristo, ili kumwimbia Mungu utenzi wa sifa na shukrani, Kristo Yesu, Mungu kweli na Mtu kweli. Huu ni mwaliko kwa wajumbe hawa kuunganika na Kanisa Katoliki kutangaza na kushuhudia Imani yao kwa Kristo Yesu, Mlango wa uzima wa milele. Huu ni mwaliko kwa Wakristo wote kuwa ni mahujaji wa matumaini yasiyo danganya; umoja unaopaswa kuimarishwa; kukuza na kujenga haki, amani na furaha ya kweli katika Kristo Yesu. Kristo Yesu ndiye Lango la maisha ya uzima wa milele, anayewashirikisha waja wake Fumbo la upendo na huruma ya Mungu isiyokuwa na mipaka; huruma inayowakumbatia binadamu wote pasi na ubaguzi, changamoto na mwaliko wa kuambata toba, wongofu wa ndani na utakatifu wa maisha.
Huu ni mlango unawaohamasisha waamini kujikita katika upendo kwa Mungu na jirani kwa kuambata Injili ya furaha, daima wakimwangalia Kristo Yesu waliyemtoboa kwa mkuki ubavuni, kimbilio la wakosefu na wadhambi; watu wanaohitaji msamaha, amani na utulivu wa ndani. Kristo Yesu ni mlango wa huruma na faraja, wema na uzuri usiokuwa na kifani. Huu ndio mlango wanamopita watu wenye haki. Kristo Yesu ni mlango wa mbingu, unaowaalika wote kushiriki furaha ya uzima wa milele. Yesu anawasubiri kwa moyo wa huruma na mapendo, wale wote wanaomwendea kwa toba na wongofu wa ndani. Bikira Maria, nyota ya asubuhi anawaongoza waamini kwa Kristo Yesu, ambaye ni Lango la huruma ya Mungu. Baba Mtakatifu anasema, kunako mwaka 2015, Kanisa liliadhimisha Jubilei ya Mwaka Mtakatifu wa Huruma ya Mungu; mwaka ambao uliwawezesha waamini wengi kuvuka Lango la Huruma ya Mungu, ili kuonja upendo unaofariji, unaosamehe na kutoa matumaini. Hii ndiyo hamu inayopaswa kushuhudiwa na watu wote kwa kuwaonjesha jirani zao wema na huruma ya Mungu katika maisha yao. Baba Mtakatifu anawataka waamini kutambua kwamba, Mwenyezi Mungu amejishusha ili kuwaokoa, mwaliko kwao pia ni kujishusha na kuwainamia jirani zao wanaoteseka kutokana na sababu mbali mbali, kwa kuwa na jicho la huduma kama ilivyokuwa kwa Bikira Maria, ili kuwaonjesha watu wanaoteseka, ile “divai ya furaha na matumaini pamoja na kuwapaka mafuta ya faraja”, kama ilivyotokea kwenye Arusi ya Kana. Mlango Mtakatifu wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican unafunguliwa rasmi katika mkesha wa Noeli tarehe 24 Desemba 2024, mwanzo wa Maadhimisho ya Jubilei kuu ya Mwaka 2025; Jubilei ya Matumaini. Baba Mtakatifu Francisko anasema, huu ni mwaliko wa kufanya mabadiliko katika maisha; Ni Pasaka ya kufanywa upya, kuingia katika maisha mapya yanayobubujika kutoka kwa Kristo Yesu; Hii ni Pasaka ya kupyaishwa katika maisha na utu wa ndani, kwa kukutana na Kristo Yesu.