Jubilei Kuu ya Mwaka 2025 ya Ukristo Na Miaka 50 Ya Uhuru Msumbiji
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S., - Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana, Dominika tarehe 22 Desemba 2024 amependa kurejea tena kwenye ujumbe wake wa amani, matumaini na upatanisho kwa watu wa Mungu nchini Msumbiji. Anawasihi wajikite katika majadiliano na utafutaji wa: ustawi, maendeleo na mafao ya wote; hali inayoungwa mkono na imani na nia njema; ili kushinda hali ya kutoaminiana na mafarakano. Wakati huo huo, Baraza la Maaskofu Katoliki Msumbiji, CEM limewaandikia watu wa Mungu nchini Msumbiji ujumbe wa Noeli kwa Mwaka 2024 unaoongozwa na kauli mbiu “Mfalme wa Amani, Tupe Amani.” Huu ni ujumbe wa amani, furaha na matumaini unaowaonesha watu wa Mungu nchini Msumbiji ukaribu na nia yao ya kusonga mbele katika njia ya amani, kwa kutambua kwamba, Sherehe ya Noeli ni Siku ya Familia. Kwa Wakristo, Kristo Yesu ni Neno wa Mungu aliyekuja kuwatajirisha kwa Umungu wake watu wa nyakati hizi. Huyu ni Mungu aliyejaa huruma na upendo, mwaliko kwa watu wote kumtumaini Yeye. Hiki ni kipindi cha kutafakari utukufu wa Mungu na amani kati ya binadamu, ili kujenga umoja na Kristo Yesu; kudumisha amani mioyoni mwa watu; amani kati ya watu na amani kati ya watu wa Mungu nchini Msumbiji. Huu ni mwaliko wa kusherekea amani na Kristo Yesu, Mfalme wa amani, wanasema Maaskofu Katoliki nchini Msumbiji.
Ikumbukwe kwamba, Mwaka 2025 Mama Kanisa anaadhimisha Jubilei Kuu ya Miaka 2025 ya Ukristo sanjari na Kumbukizi ya Miaka 50 tangu Msumbiji ilipojipatia uhuru wake wa bendera. Sherehe hizi ziwe ni kikolezo cha amani na maridhiano kati ya watu wa Mungu nchini Msumbiji na hivyo kuepuka mafarakano. Huu ni mwaliko wa kujikita katika njia ya haki, amani na upatanisho kwa kujenga na kudumisha utamaduni wa kukutana kama ndugu wamoja, ili kukoleza mafundisho ya amani. Baraza la Maaskofu Katoliki Msumbiji, CEM linasema, kwa hakika matokeo ya Uchaguzi mkuu uliofanyika tarehe 9 Oktoba 2024 hayatawafurahisha wananchi wote wa Msumbiji, lakini ni matakwa yao kwamba, yatakuwa yameegemezwa kwenye ukweli wa uchaguzi unaothibitishwa na ushuhuda unaoweza kuthibitika na kuaminika. Njia ya pekee ya kuweza kusonga mbele ni upendo unaosimikwa katika haki, ujenzi na uimarishaji wa amani, maridhiano na umoja wa Kitaifa. Huu ni mwaliko kwa watu wa Mungu nchini Msumbiji kutumia kikamilifu: Ubunifu, Unyenyekevu na Akili zao ili kujenga msingi wa amani kwa wananchi wote wa Msumbiji. Wananchi wajikite katika majadiliano katika ukweli na uaminifu, waepuke vizingiti vinavyoweza kukwamisha majadiliano haya kwani amani, ustawi na maendeleo ya Msumbiji ni ya thamani kubwa kuliko masilahi binafsi, masilahi ya kichama; kundi yawe makampuni ya kitaifa au kigeni.
Wananchi wa Msumbiji wakatae katu katu kutumbukizwa kwenye: Ugandamizaji, tabia ya kulazimishwa, vurugu na uharibifu; migawanyiko na umaskini. Wananchi wajitahidi kumwilisha Neno la Mungu, nyenzo msingi ya kujenga na kuishi kwa pamoja; kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi; kujenga na kudumisha utawala bora na shirikishi; kwa kujali na kuthamini maoni ya wengi; kuacha dharau na hivyo kutoa nafasi kwa heshima, uaminifu, mshikamano, kukubalika sanjari na kuheshimiana. Upendo usimikwe katika chaguzi zao za kisiasa, kiuchumi na kijamii, ili Injili ya matumaini iweze kuwafikia watu wa wote wa Msumbiji. Ni matumaini ya Baraza La Maaskofu Katoliki Msumbiji kwamba, roho ya Noeli inaingia katika familia ili kutoa mwanga katika mijadala sanjari na chaguzi zao. Maadhimisho ya Mwaka Mpya wa 2025 yalete mwamko wa kujenga upya Msumbiji na kwamba, kila raia ashiriki kikamilifu katika ujenzi wa misingi ya haki, na amani. Mwaka 2025 uwe ni mwaka wa kujenga na kustawisha amani; amani itafutwe kwa moyo na wala si kwa silaha. Amani iwe ni mwisho wa vita na mwanzo wa ulimwengu mpya ambapo haki na amani hukumbatiana na kukamilishana. Ujumbe huu umetiwa mkwaju na Askofu Inàcio Saure, wa Jimbo Katoliki la Nampula na Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Msumbiji, CEM.