Jubilei ya Miaka 2025 Ya Ukristo: Lango la Gereza la Rebibbia Lafunguliwa
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S., - Vatican.
Tamko la Maadhimisho ya Jubilei kuu ya Mwaka 2025 ya Ukristo linanogeshwa na kauli mbiu “Spes non confundit" yaani “Tumaini halitahayarishi.” Rum 5:5 na kwamba, kiini cha maadhimisho haya ni matumaini yatakayowawezesha watu waaminifu wa Mungu kutoka sehemu mbalimbali za dunia kufanya hija ya maisha ya kiroho mjini Roma sanjari na maadhimisho haya kufanyika kwenye Makanisa mahalia, ili kukutana na Kristo Yesu aliye hai na mbaye pia ni Lango la maisha ya uzima wa milele. Rej, Yn 10:7.9. Mama Kanisa anaitwa na kutumwa kutangaza na kushuhudia Injili ya matumaini dhidi ya hofu na mashaka; ukosefu wa imani na furaha ya kweli. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko kwamba, maadhimisho ya Jubilei ya Mwaka 2025 iwe ni fursa ya kupyaisha tena matumaini kwa kuongozwa na Neno la Mungu. Katika Tamko hili, Baba Mtakatifu anakazia kuhusu Matumaini katika Neno la Mungu ili kuamini, kutumaini, kupenda na kuvumilia kwa kutambua kwamba, wao ni mahujaji wa matumaini. Alama za matumaini zinazomwilishwa katika amani, kwa kujikita katika Injili ya uhai, maboresho ya magereza; huduma kwa wagonjwa, vijana, wahamiaji na wakimbizi, wazee na maskini. Huu ni wito wa matumaini kwa kuzama katika matumizi bora ya rasilimali za dunia; msamaha wa madeni ya nje kwa nchi zinazoendelea duniani.
Jubilei ya Miaka 1, 700 tangu Mtaguso wa Nicea ulipoadhimishwa kunako mwaka 325. Nanga ya matumaini katika maisha ya uzima wa milele yanayopata asili na chimbuko lake kutoka katika mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kwa wafu; Ushuhuda wa wafiadini na waungama imani; hukumu ya Mungu na mwaliko kwa waamini kufanya toba na wongofu wa ndani; Rehema na Sakramenti ya Upatanisho; Wamisionari wa huruma ya Mungu. Bikira Maria ni shuhuda wa hali ya juu kabisa wa matumaini, Nyota ya Bahari na kwamba, hija ya maadhimisho ya Jubilei ya Mwaka 2025 ya Ukristo iwasaidie waamini kujikita katika Maandiko Matakatifu. Huu ni muhtasari wa Tamko la Maadhimisho ya Jubilei ya Mwaka 2025 ya Ukristo. Jubilei hii ni muda muafaka wa kupyaisha imani, matumaini na mapendo thabiti, kwa kuishi kama ndugu wamoja, sanjari na kusikiliza pamoja na kujibu kilio cha Dunia Mama na Kilio cha Maskini. Ni muda wa toba na wongofu wa ndani na wa kiikolojia, tayari kusimama kidete kulinda na kutunza mazingira bora nyumba ya wote. Ni muda muafaka kwa waamini kujikita katika kutangaza na kushuhudia imani na matumaini yanayomwilishwa katika huduma ya upendo kwa Mungu na jirani; kwa kukazia umoja na utofauti wa wateule watakatifu wa Mungu.
Jubilei ni muda uliokubalika na Mwenyezi Mungu wa kuhakikisha kwamba, waamini wanajitahidi kumwilisha karama na mapaji yao kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Lengo ni kutangaza na kushuhudia imani na furaha ya Injili kwa watu wa Mataifa. Baba Mtakatifu Francisko katika maisha na utume wake, ameendelea kutoa kipaumbele cha pekee kwa wafungwa magerezani. Mara nyingi Baba Mtakatifu wakati wa hija zake za kitume, amependa kutembelea, kusali na kuzungumza na wafungwa, ili kuwaonjesha huruma na upendo wa Mungu unaoponya na kumwokoa mwanadamu, ili aweze kugeuka na kuwa mtu mpya zaidi. Baba Mtakatifu anafanya yote haya kuwaonesha na kuwaonjesha wafungwa uwepo wake wa kibaba kwa njia ya sala katika shida na mahangaiko yao ya ndani, ili waweze kuwa na matumaini mapya katika maisha yao kwa siku za baadaye. Mama Kanisa katika maisha na utume wake kwa wafungwa magerezani anakazia hasa: Umuhimu wa kulinda na kudumisha utu, heshima na haki msingi za wafungwa magerezani, kwa kutambua kwamba, wafungwa na askari magereza ni vyombo na mashuhuda wa Injili. Askari magereza wawe na ujasiri wanapotekeleza dhamana na utume wao miongoni mwa wafungwa.
Baba Mtakatifu Francisko anawapongeza askari magereza kila wakati wanapotekeleza dhamana na utume wao kwa ajili ya ulinzi na usalama kwa maskini na wanyonge zaidi katika jamii, yaani wafungwa, ili kuhakikisha kwamba, haki, amani, ulinzi na usalama vinatawala ndani ya jamii. Hii ni dhamana inayowataka siku kwa siku kuwa ni wajenzi wa haki na wajumbe wa amani kwa kuwakumbuka wafungwa hao waliofungwa kana kwamba, wamefungwa pamoja nao na kama wanadhulumiwa, basi hata wao wahisi haya madhulumu mwilini wao. Maisha ya gerezani ni magumu na mara nyingine yanaweza kukatisha tamaa, kwa mfungwa kuelemewa na upweke hasi, hali ya kukata tamaa na hatimaye kushindwa kuona hatima ya maisha yake. Gereza ni mahali pa mahangaiko ya binadamu. Askari magereza wanatumia muda mrefu kuwa magerezani, ili kulinda na kudumisha ulinzi na usalama, jambo la msingi ni kuhakikisha kwamba, utu, heshima na haki msingi za binadamu zinalindwa barabara. Askari magereza wawe ni walinzi wa ndugu zao wafungwa, wawe ni madaraja kati ya magereza na jamii katika ujumla wake kwa kuonesha upendo unaowawajibisha, ili kuondoa wasiwasi na kashfa ya kutowajali wengine. Baba Mtakatifu anawataka askari magereza kutambua uzito wa kazi na wajibu wao kwa wafungwa pamoja na familia zao wenyewe. Kumbe, inawapasa kusaidiana na kushikamana ili kukabiliana na changamoto, matatizo na fursa zinazopatikana kutokana na kazi na utume wao.
Ni katika muktadha wa maadhimisho ya Jubilei kuu ya Miaka 2025 ya Ukristo, Baba Mtakatifu Francisko, Alhamisi tarehe 26 Desemba 2024, Sikukuu ya Mtakatifu Stefano Shemasi na Shuhuda wa kwanza wa imani na matumaini kuuwawa kwa kupigwa mawe hadi kufa, huku akiwa anatafakari “utukufu wa Mungu huku akiona mbingu zimefunguka anasema, Ukatili wa mwanadamu unapitwa na huruma ya Mungu, inayokusanya na kukumwokoa mwanadamu kutoka katika ubaya wa moyo! Kristo Yesu ni Lango la Imani, Matumaini, Mapendo na Msamaha wa kweli. Baba Mtakatifu Francisko baada ya kesha la Noeli 2024 kufungua Lango la Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, tarehe 26 Desemba 2024 amefungua Lango kuu la Gereza la Rebibbia lililoko mjini Roma na baadaye kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu na wafungwa pamoja na askari magereza na viongozi wapatao mia tatu. Baba Mtakatifu amewataka wafungwa kushikilia kamba ya nanga ya matumaini na kamwe wasiiache. Pili, wahakikishe kwamba wanafungua nyoyo zao kwa upana zaidi. Na hatimaye, wamwombe Kristo Yesu awasaidie kutimiza mambo haya mawili katika maisha yao kama sehemu ya maadhimisho ya Jubilei kuu ya Miaka 2025 ya Ukristo.
Baba Mtakatifu anawataka wafungwa kumfungulia Kristo Yesu malango ya maisha yao sanjari na kushiriki katika mchakato wa ujenzi wa udugu wa kibinadamu, ili kusherehekea na kufurahia maisha. Mioyo iliyojifunga na migumu ni kikwazo katika maisha. Ili waamini waweze kuishi vyema neema ya Jubilei, wanapaswa kufungua malango ya nyoyo zao kwa Kristo Yesu, chemchemi ya matumaini ambayo kamwe hayadanganyi, hata pale mtu anapoanza kukata tamaa, kamwe waamini wasikate tamaa, bali washikilie kwa nguvu zote kamba ya nanga ya matumaini. Waamini wamfungulie Kristo Yesu malango ya nyoyo zao na kamwe wasifanye shingo ngumu, ili waweze kushiriki katika ujenzi wa udugu wa kibinadamu, kila mtu kadiri ya uwezo na mbinu zake. Lango la gereza kuu la Rebibbia lililofunguliwa ni ishara ya nje, sasa wanapaswa kuzama zaidi katika undani wa nyoyo zao, tayari kumfungulia Kkristo Yesu, malango ya maisha yao. Baba Mtakatifu amewatakia wafungwa wote maadhimisho mema ya Jubilei kuu ya Miaka 2025 ya Ukristo; Amani na utulivu wa ndani. Baba Mtakatifu anawakumbuka sana wafungwa na kuwaombea.