Tafuta

Tarehe 26 Desemba 2024 Papa Francisko anatarajia kufungua Lango la Gereza kuu la Rebibbia Kielelezo cha Maadhimisho ya Jubilei kuu ya Miaka 2025 ya Ukristo. Tarehe 26 Desemba 2024 Papa Francisko anatarajia kufungua Lango la Gereza kuu la Rebibbia Kielelezo cha Maadhimisho ya Jubilei kuu ya Miaka 2025 ya Ukristo.  (AFP or licensors)

Mlango wa Jubilei ya Wafungwa Kufunguliwa Kwenye Gereza la Rebibbia

Ni katika muktadha wa maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo sanjari na Maadhimisho ya Sikukuu ya Mtakatifu Stefano, Shemasi na Shahidi wa kwanza kumfuasa Kristo Yesu kwa njia ya mateso na kifo cha ajabu, kwa kupigwa mawe hadi kufa, Baba Mtakatifu anatarajia kufungua Mlango wa Jubilei kwa wafungwa wa Gereza kuu la Rebibbia lililoko mjini Roma, kama alama muhimu sana ya maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo! Huruma na Msamaha!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, magereza yanapaswa kuboreshwa zaidi, ili kulinda na kudumisha utu na heshima ya binadamu! Inasikitisha kusikia na kuona kwamba, magereza yanageuka kuwa ni mahali pa vurugu, uvunjifu wa sheria, kanuni na taratibu za nchi. Magereza yamekuwa ni mahali ambapo: haki msingi, utu na heshima ya binadamu vinasiginwa kwa kiasi kikubwa! Utume kwa wafungwa magerezani ni kati ya mambo ambayo Baba Mtakatifu anayapatia kipaumbele, ili kuwasaidia wafungwa na mahabusu kulinda na kudumisha utu na heshima yao, chemchemi ya matumaini ya maisha mapya! Jamii inapashwa kuboresha hali ya magereza ili kuwawezesha wafungwa wanapomaliza kutumikia adhabu zao, waweze kurejea tena katika maisha ya kawaida na kwamba, kifungo si laana ya maisha! Wafungwa magerezani wajengewe mazingira mazuri yatakayowawezesha kujifunza stadi za maisha; kuboresha mahusiano na mafungamano yao ya kijamii, ili kuondokana na kishawishi cha kuwatenga watu waliomaliza kutumikia adhabu zao. Hali kama itawaongezea machungu. Baba Mtakatifu anawaalika watu kuonja udhaifu wa binadamu badala ya kuwagawa watu katika makundi ya wema na wabaya. Waone ubaya wa dhambi, tayari kukimbilia na kuambata huruma na upendo wa Mungu katika maisha yao. Baba Mtakatifu anasikitika kusema, wafungwa wengi wanawake wanateseka na watoto wao magerezani! Hii inakuwa ni changamoto kubwa kuweza kukabiliana na ugumu wa maisha! Katika hali na mazingira kama haya, wafungwa wanapaswa kujengewa matumaini, kwa kutambua kwamba, wao ni binadamu wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu, wanahistoria ya maisha na kwamba, wanayo ari ya kutaka kuambata matumaini. Maisha ya wafungwa, utu na heshima yao, familia na watu wanaowategemea ni mambo msingi yanayopaswa kuzingatiwa, watu wanapoangalia changamoto za wafungwa wa kike magerezani!

Jubilei kuu ya Miaka 2025 ni pindi cha sala, toba na wongofu wa ndani
Jubilei kuu ya Miaka 2025 ni pindi cha sala, toba na wongofu wa ndani

Tamko la Maadhimisho ya Jubilei ya Mwaka 2025 ya Ukristo linanogeshwa na kauli mbiu “Spes non confundit" yaani “Tumaini halitahayarishi.” Rum 5:5 na kwamba, kiini cha maadhimisho haya ni matumaini yatakayowawezesha watu waaminifu wa Mungu kutoka sehemu mbalimbali za dunia kufanya hija ya maisha ya kiroho mjini Roma sanjari na maadhimisho haya kufanyika kwenye Makanisa mahalia, ili kukutana na Kristo Yesu aliye hai na ambaye pia ni Mlango wa uzima. Rej, Yn 10:7.9. Mama Kanisa anaitwa na kutumwa kutangaza na kushuhudia Injili ya matumaini dhidi ya hofu na mashaka; ukosefu wa imani na furaha ya kweli. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko kwamba, maadhimisho ya Jubilei ya Mwaka 2025 ni fursa ya kupyaisha tena matumaini kwa kuongozwa na Neno la Mungu. Katika Tamko hili, Baba Mtakatifu anakazia kuhusu Matumaini katika Neno la Mungu ili kuamini, kutumaini, kupenda na kuvumilia kwa kutambua kwamba, binadamu wote ni mahujaji wa matumaini. Alama za matumaini zinazomwilishwa katika amani, kwa kujikita katika Injili ya uhai, maboresho ya magereza; huduma kwa wagonjwa, vijana, wahamiaji na wakimbizi, wazee na maskini. Wito wa matumaini kwa kujikita katika matumizi bora ya rasilimali za dunia; msamaha wa madeni ya nje kwa nchi zinazoendelea duniani. Ni katika muktadha wa maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo sanjari na Maadhimisho ya Sikukuu ya Mtakatifu Stefano, Shemasi na Shahidi wa kwanza kumfuasa Kristo Yesu kwa njia ya mateso na kifo cha ajabu, kwa kupigwa mawe hadi kufa, Baba Mtakatifu anatarajia kufungua Mlango wa Jubilei kwa wafungwa wa Gereza kuu la Rebibbia lililoko mjini Roma, kama alama muhimu sana ya maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo anasema, Askofu mkuu Salvatore Rino Fisichella, Mwenyekiti mwenza, Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa Watu.

Jubilei ni kipindi cha furaha, toba na wongofu wa ndani
Jubilei ni kipindi cha furaha, toba na wongofu wa ndani

Yesu alipokuwa kufani, alijiaminisha kwa Baba yake wa mbinguni pamoja na kuwasamehe watesi wake! Stefano Shahidi naye alipokuwa anakaribia kufa aliomba akisema, “Bwana Yesu pokea roho yangu” na hivyo kuendelea kumuiga Kristo Yesu kwa kuwasamehe watesi wake, kama Kristo mwenyewe alivyofanya, mwaliko kwa waamini kujifunza kutoka kwa Kristo Yesu, kusamehe na kusahau, ingawa yataka moyo kweli kweli anakiri Baba Mtakatifu Francisko. Msamaha unapanua moyo, unachipua ushirikiano na mshikamano; unamkirimia mwamini amani na utulivu wa ndani. Stefano, Shahidi ni kielelezo na ushuhuda unaopaswa kufuatwa ili kukuza na kudumisha mahusiano na mafungamano ya kifamilia; katika maeneo ya shule na kazi; katika parokia na maeneo mbali mbali ya shughuli za kitume na hata katika jumuiya, msamaha daima unapaswa kupewa kipaumbele cha kwanza. Baba Mtakatifu anasema, hii ni dhamana na wajibu wa Kanisa zima kama sehemu ya utekelezaji wa utume wake unaomwilisha matendo ya huruma katika uhalisia wa maisha ya watu. Wakati wa hukumu ya mwisho, watu watahukumiwa kadiri walivyowatendea ndugu zake walio wadogo, na kwa kufanya vile, walimtendea Kristo Yesu mwenyewe. (Rej. Mt. 25:40) Kristo Yesu anajitambulisha kuwa kati ya watu wenye njaa, kiu, wageni, watu walio uchi, wagonjwa na wale walioko kifungoni. Baba Mtakatifu anasema taswira inayotolewa na magereza sehemu mbalimbali za dunia inaonesha ukweli wa jamii ambamo uchoyo, ubinafsi na utandawazi wa kutoguswa na mahangaiko ya jirani vinatawala. Kuna maamuzi ambayo yamefanywa kisheria lakini yanakiuka utu, heshima na haki msingi za binadamu; kwa kujidai kukuza na kutaka kudumisha ulinzi na usalama wa raia na mali zao. Matokeo yake ni watu kutengwa na kutupwa magerezani kama suluhu ya matatizo mbalimbali yanayoisonga jamii. Lakini ikumbukwe kwamba, kuna kiasi kikubwa cha rasilimali na utajiri wa nchi unaotumika kwa ajili ya kuwahudumia wafungwa magerezani, ikilinganishwa na kiasi cha fedha zinazotengwa kwa ajili ya kuchochea kasi ya maendeleo fungamani ya binadamu, ambayo yangewezesha idadi kubwa ya wafungwa kupata kazi na kipato halali badala ya kujiingiza kwenye vitendo vya uvunjaji wa sheria.

Jubilei ni kipindi cha kutangaza na kushuhudia huruma ya Mungu kwa waja wake
Jubilei ni kipindi cha kutangaza na kushuhudia huruma ya Mungu kwa waja wake

Baba Mtakatifu anakaza kusema, ni rahisi sana kufumbia macho umuhimu wa elimu na malezi makini kwa jamii, sanjari na kushindwa kuona ukweli halisi wa matatizo na ukosefu wa haki msingi na hivyo suluhu ya haraka inayoweza kupatikana ni ujenzi wa magereza, ili “kuwashikisha adabu wale wote wanaovunja sheria za nchi.” Umefika wakati wa kutoa msukumo wa pekee kwa ajili ya maendeleo fungamani ya binadamu kwa raia wote. Kwa bahati mbaya, magereza mengi yameshindwa kutekeleza dhamana na wajibu wake wa kuweza kutoa mafunzo bora zaidi, ili wafungwa wanapomaliza adhabu zao na kutoka magerezani waweze kuwa ni watu wema zaidi kuliko walivyoingia magerezani. Ni ukweli usioweza kufumbiwa macho kwamba, kuna uhaba mkubwa wa rasilimali fedha na watu ili kukabiliana na changamoto za kijamii, kisaikolojia na kifamilia wanazokabiliana nazo wafungwa magerezani. Baba Mtakatifu Francisko anasema, magereza yamegeuka kuwa ni mahali hatari sana, ambapo utu na heshima ya binadamu vinasiginwa. Mafunzo makini kwa wafungwa yanaanza pale ambapo wafungwa wanapewa fursa ya kushiriki katika mchakato wa maendeleo, wanapopewa elimu makini na kufanyishwa kazi zenye staha. Yote haya lazima pia yazingatie huduma bora za afya kwa wafungwa pamoja na kuunda mazingira ambayo, wafungwa wataweza pia kushirikiana kwa karibu na raia wengine. Jamii inapaswa kuwa na mwelekeo tofauti sana kwa wafungwa magerezani, kwa kuwapatia msaada wa hali na mali, ili kuboresha maisha yao, kama sehemu ya faraja kutoka kwa Mwenyezi Mungu.

Injili ya Matumaini dhidi ya hofu, mashaka na ukosefu wa imani thabiti
Injili ya Matumaini dhidi ya hofu, mashaka na ukosefu wa imani thabiti

Kwa bahati mbaya sana, wafungwa wamekuwa wakiangaliwa kwa “jicho la kengeza” kiasi kwamba, si rahisi sana kuthamini utu na heshima yao. Wafungwa waonjeshwe matumaini na kupewa tena fursa ya kufanya kazi, ili kujipatia mahitaji yao msingi. Pale ambapo wafungwa baada ya kumaliza adhabu yao wanashindwa kutambuliwa utu na heshima yao, wanajikuta wakiwa kwenye majaribu makubwa kati ya kutafuta fursa za kazi, kutenda uhalifu pamoja na kujenga mazingira yasiokuwa salama. Baba Mtakatifu anaitaka Jumuiya ya waamini kuwaonjesha wafungwa huruma na mapendo, dhamana na utume unaopaswa kutekelezwa na Makanisa mahalia. Kila mwamini awe ni shuhuda na chombo cha huruma ya Mungu kwa wafungwa, ili kuiwezesha jamii kukita mizizi yake katika misingi ya haki na amani. Matendo ya huruma: kiroho na kimwili ni nyenzo thabiti katika mchakato wa huduma kwa wafungwa magerezani. Huu ni mchakato unaowawezesha watu wa Mungu kutoa huduma kwa wafungwa na hivyo kujenga ndani mwao matumaini. Waamini waendelee kumtambua Kristo Yesu anayejitambulisha kati ya wafungwa magerezani. Baba Mtakatifu anawapongeza wale wote wanaoendelea kujisadaka kwa ajili ya huduma kwa wafungwa pamoja na familia zao, hasa katika kipindi hiki kigumu cha majaribio. Baba Mtakatifu mwishoni anawaombea heri na baraka wale wote wanaojisadaka kwa ajili ya huduma za kichungaji kwa wafungwa magerezani sehemu mbali mbali za dunia, kwani kwa kufanya hivi, wanaendeleza utume ambao Kristo Yesu ameliachia Kanisa lake. Mwishoni mwa maisha yao hapa duniani, wataweza kusikia kutoka kwa Kristo Yesu “Njooni mliobarikiwa na Baba yangu, urithini ufalme mliowekewa tayari tangu kuumbwa ulimwengu.” Mt. 25:35.

Jubilei ya Wafungwa

 

24 December 2024, 15:41