Papa amekutana na wasanii wa Tamasha la Noeli: amani na matumaini!
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi tarehe 14 Desemba 2024 alikutana na Washiriki wa Masuala ya Noeli na Wasanii wa Tamasha la Noeli kwa mwaka 2024, mjini Vatican. Akianza hotuba yake alitoa salamu kwa Kardinali José Tolentino de Mendonça, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Utamaduni na Elimu na wasanii ambao wametumbuiza katika Tamasha la Noeli. Salamu zake pia kwa wawakilishi wa Mfuko wa Kipapa wa Gravissimum Educationis – Utamaduni wa Elimu, Utume wa Wasalesian (Mission don Bosco) na wote ambao wamesaidia kufanikisha tukio hili. Papa alipenda kutoa kutafakari kwa ufupi juu ya mambo mawili muhimu ambayo anaamini ana mengi ya kufundisha nayo ni amani na matumaini.
Amani
Baba Mtakatifu alidadavua la kwanza Amani: “Inatia moyo kufikiria, hapa pamoja na wasanii na wanamuziki, kwamba Yesu alipozaliwa katika ukimya wa usiku, wimbo wa amani, ulioimbwa na “umati wa jeshi la mbinguni” ( Lk 2:13 ) ulijaza mbingu kwa furaha. Hivyo ndivyo ilivyokuwa. Muziki huzungumza moja kwa moja na moyo wa mwanadamu kwa namna ya pekee; una uwezo wa ajabu wa kuunda umoja na kukuza ushirika. Kwa hivyo aliwahimiza wao kuwa “malaika wa amani” na kuwekeza vipaji vyao, usanii wao na maisha yao , kadiri wawezavyo na popote watakapokuwa, katika kukuza utamaduni huo wa udugu na upatanisho katika ulimwengu wetu wa leo, ambao unahitaji zaidi kuliko hapo awali.
Matumaini
Pili, matumaini. Papa Francisko amewashukuru uamuzi wa kutoa Tamasha hilo kwa mada hiyo, ambayo inaendesha kama kupitia ushuhuda wake wa sanaa na mshikamano, hasa katika kuunga mkono wamisionari wa Kisalesian wanaofanya kazi na vijana duniani kote. Hii inatukumbusha safari ambayo Kanisa zima linakaribia kufanya - kama "mahujaji wa matumaini" - katika Mwaka wa Jubilei ijayo. Noeli inatukumbusha kwamba tumaini ni zawadi ya kwanza kabisa kutoka kwa Mungu. Kwa hivyo, "imesimikwa kwenye imani na kukuzwa na upendo" (Hati ya Jubilei 2025 ya Spes Non Confundit, 3). Kwa upande mmoja, tumaini lazima lizamishe mizizi yake katika udongo wenye rutuba wa ushirika na Bwana, lakini lazima pia likue na kuzaa matunda kupitia maamuzi madhubuti yanayochochewa na upendo, na hivyo kujaza sasa na maana na kufungua upeo mpya kuelekea siku zijazo.
Ulimwengu na Kanisa vinahitaji talanta za wasanii
Amani na matumaini ndiyo misisisitizo miwili ya wimbo ambao Papa amewahimiza kuchukua na kufanya isikike katika mitaa ya ulimwengu wa leo hii, ili vizazi vijavyo viweze kurithi ulimwengu bora na wa amani zaidi. Watu wengi wanasubiri kupokea zawadi hii kutoka kwao. Kwa namna ya pekee, amewawafikiria vijana walioshiriki Shindano la Noeli na wanaojumuika nao jukwaani katika siku hii. Uwepo wao pamoja, ni ishara ya agano safi na lenye afya kati ya vizazi. Papa Francisko awaeleza wao kuwa “Ulimwengu na Kanisa vinahitaji talanta zenu, mawazo yenu ya ubunifu, ukarimu wenu na shauku yenu ya haki na udugu. Kwa kuzingatia hili, ninamwomba Bwana amimine baraka zake juu yenu na wapendwa wenu. Ninawatakia kila la kheri kwa Tamasha hili na Noeli Njema! Na ninawaomba, tafadhali, msisahau kuniombea. Asante,” Alihitimisha