Papa Francisko:tuombe ili Roho Mtakatifu aje na si kujihubiri bali Bwana!
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Katika mzunguko wa Katekesi, kuhusu mada ya “Roho na Mchumba. Roho Mtakatifu anaongoza Watu wa Mungu kukutana na Yesu Tumaini letu,” Baba Mtakatifu Francisko, Jumatano tarehe 4 Desemba 2024 akiwageukia waamini na mahujaji waliofika katika Uwanja wa Mtakatifu Petro, mjini Vatican amejikita na sehemu ya 16 isemayo: “Kutangaza Injili katika Roho Mtakatifu. Roho Mtakatifu na Unjilishaji.” Kabla ya kuanza tafakari yake, lilisoma somo: “Ndugu zangu, nilipokuja kwenu, [...] neno langu na mahubiri yangu hayakujikita katika maneno ya hekima yenye kuvutia sana, bali kwa udhihirisho wa Roho Mtakatifu na nguvu zake, ili imani yenu isiwe msingi wa hekima ya wanadamu; bali kwa uwezo wa Mungu,”( 1 Kor 2,1.4-5). Baba Mtakatifu alisema kuwa: Baada ya kutafakari juu ya utakaso na karama ya Roho, tunaweka katekesi hii kwa kipengele kingine: kazi ya Unjilishaji wa Roho Mtakatifu, yaani, jukumu lake la Kanisa katika kuhubiri. Barua ya Kwanza ya Petro inafafanua mitume kama "wale waliotangaza Injili kwa Roho Mtakatifu" (rej. 1:12). Katika usemi huo tunapata vipengele viwili vya msingi vya mahubiri ya Kikristo: maudhui yake, ambayo ni Injili, na njia yake, ambayo ni Roho Mtakatifu.
Kwa njia hiyo Papa alisema, hebu tuseme kitu kuhusu moja na nyingine. Katika Agano Jipya, neno “Injili” lina maana kuu mbili. Inaweza kuonesha kila mojawapo ya Injili nne zinazokubalika: Mathayo, Marko, Luka na Yohane na kwa maana hiyo Injili ina maana ya Habari Njema iliyotangazwa na Yesu wakati wa maisha yake duniani. Baada ya Pasaka, neno “Injili” linachukua maana mpya ya Habari Njema kuhusu Yesu, yaani, fumbo la Pasaka: kifo na ufufuko wa Bwana. Hiki ndicho mtume anachokiita “Injili”, anapoandika: “Siionei haya Injili, kwa maana ni uweza wa Mungu uuletao wokovu wa kila aaminiye” (Rm 1:16). Mahubiri ya Yesu na, baadaye, yale ya Mitume, pia yana wajibu wote wa kimaadili unaotokana na Injili, kuanzia amri zile kumi hadi amri “mpya” ya upendo. Lakini ikiwa hatutaki kurudi nyuma katika kosa lililolaaniwa na mtume Paulo la kutanguliza sheria mbele ya neema na matendo mbele ya imani, ni muhimu kila mara kuanza tena kutokana na tangazo la kile ambacho Kristo ametutendea. Baba Mtakatifu amesema kuwa “ Ndiyo maana katika Waraka wa Kitume wa Evangelii gaudium kuna msisitizo mkubwa juu ya jambo la kwanza kati ya hayo mawili, yaani, kerygma, au “tangazo” ambalo kila matumizi ya maadili hutegemea.
Kiukweli, “katika katekesi tangazo la kwanza au kerygma lina jukumu la msingi, ambalo lazima liwe kiini cha shughuli ya kueneza Injili na kila nia ya upyashaji wa kikanisa. […] Tunaposema kwamba tangazo hili ni "la kwanza", hii haimaanishi kuwa ni mwanzo na kisha kusahaulika au kubadilishwa na maudhui mengine yanayolizidi. Ni tangazo la kwanza kwa maana ya ubora, kwa sababu ndilo tangazo kuu, ambalo tunapaswa kurudi kila wakati kusikiliza kwa njia tofauti na kwamba lazima turudi kutangaza wakati wa katekesi kwa namna moja au nyingine, katika hatua zake zote na nyakati zake. […] Haipaswi kufikiriwa kuwa katika katekesi kerygma inaachwa kwa ajili ya malezi ambayo yanapaswa kuwa "imara" zaidi. Hakuna kitu kigumu zaidi, cha kina zaidi, hakika zaidi, thabiti na chenye hekima zaidi kuliko tangazo hili” (Na. 164-165) yaani, kerygma.
Baba Mtakatifu amesisitiza kuwa kufikia sasa tumeona maudhui ya mahubiri ya Kikristo. Hata hivyo, lazima pia tukumbuke kati ya tangazo. Injili lazima ihubiriwe “kwa Roho Mtakatifu” (1 Pt 1:12). Kanisa lazima lifanye sawasawa na kile ambacho Yesu alisema mwanzoni mwa huduma yake ya umma: “Roho wa Bwana yu juu yangu; kwa sababu hiyo alinitia mafuta na kunituma kuwahubiri maskini habari njema” (Lk 4:18). Kuhubiri kwa upako wa Roho Mtakatifu kunamaanisha kusambaza, pamoja na mawazo na mafundisho, maisha na usadikisho wa imani yetu. Inamaanisha kutegemea sio "maneno ya hekima yenye kushawishi, bali udhihirisho wa Roho na nguvu zake" (1 Kor 2:4), kama Mtakatifu Paulo alivyoandika. Ni rahisi kusema kuwa mtu anaweza kupinga, lakini tunawezaje kuiweka katika vitendo ikiwa haitegemei sisi, juu ya ujio wa Roho Mtakatifu? Kiukweli, kuna jambo moja ambalo linategemea sisi, au tuseme mawili ambapo Papa Francisko ameyataja kwa ufupi.
La kwanza ni maombi. Roho Mtakatifu huja kwa wale wanaoomba, kwa sababu imeandikwa – kwamba Baba wa mbinguni huwapa Roho Mtakatifu wale wamwombao" (Lk 11,13), hasa ikiwa wanaomba kutangaza Injili ya Mwana wake! Ole wa kuhubiri bila kuomba! Tunakuwa kile ambacho Mtume anafafanua kama "shaba ivumayo na matoazi yavumayo" (rej. 1Kor 13:1). Kwa hiyo, jambo la kwanza linalotutegemea sisi ni kuomba ili Roho Mtakatifu aje. Na la pili si kutaka kujihubiri sisi wenyewe, bali kwa njia ya Yesu Bwana (rej 2Kor 4:5). Katika hilo, Papa Francisko amefafanua kwa kirefu kwamba hiyo inahusu kuhubiri. Wakati fulani kuna mahubiri marefu, ya dakika 20, dakika 30... Lakini, tafadhali, wahubiri lazima wahubiri wazo, mapendo na mwaliko wa kutenda. Zaidi ya dakika nane mahubiri yanafifia, hajulikani wazi. Nami ninasema hivi kwa wahubiri... Watu walipiga makofu lakini Papa aliongeza: “Ninaona mnapenda kusikia haya! Wakati fulani tunaona watu ambao, wakati mahubiri yanaanza, wanatoka nje kuvuta sigara kisha wanarudi. Tafadhali, mahubiri lazima yawe na wazo, mapendo na pendekezo la hatua. Na msipite zaidi ya dakika kumi. Hili ni muhimu sana.”
Papa akiendelea alisema Jambo la pili kwamba, alikuwa amewambia kwamba siyo kutaka kujihubiri sisi wenyewe, bali Bwana. Hakuna haja ya kukaa juu ya hilo, kwa sababu mtu yeyote anayehusika katika uinjilishaji anajua vizuri maana yake, kwa hiyo ni vitendo, na sio kujihubiri mwenyewe. Baba Mtakatifu Francisko amependa kukazia juu ya kuhubiri kwamba pia kunamaanisha sio kila mara kutoa kipaumbele kwa mipango ya kichungaji inayokuzwa na sisi na kuhusishwa na jina la mtu, lakini kwa hiari kushirikiana, ikiwa imeombwa, katika mipango ya jamii, au kukabidhiwa kwetu kwa utii. Kwa kuhitimisha amesema “Roho Mtakatifu atusaidie, atusindikize na kulifundisha Kanisa kuhubiri Injili kwa wanaume na wanawake wa wakati huu! Asante.”