Papa kwa Balozi wa Urusi:Vita ni jeraha kubwa lililoletwa kwa familia ya wanadamu
Na Salvatore Cernuzio – Vatican.
Papa Francisko amechukua tena kalamu na karatasi-kama alivyofanya mnamo Novemba 19 kwa barua yake kwa Balozi wa Vatican nchini Ukraine, akiandika barua tena kwa mwakilishi wake katika Shirikisho la Urusi, Askofu Mkuu Giovanni d'Aniello. Katika barua yake, Papa alionesha masikitiko yake ya kuendelea kwa vita vya muda mrefu nchini Ukraine ambavyo vinawakilisha “jeraha kubwa lililoletwa kwa familia ya binadamu. "Ninaamini kwamba juhudi za kibinadamu zinazoelekezwa kwa walio hatarini zaidi zinaweza kufungua njia kwa juhudi mpya za kidiplomasia, muhimu kusimamisha kuendelea kwa mzozo na kufikia amani iliyosubiriwa kwa muda mrefu."
Karibu na wale wanaoteseka
Mnamo Novemba 19 iliadhimisha siku elfu moja tangu Urusi ilipoanzisha uvamizi wake kamili wa Ukraine. Karibu miaka mitatu ya milipuko ya mabomu, mauaji, majeraha, na kufungwa gerezani kumesababisha mamia ya maelfu ya watu kuuawa na mafuriko ya kilio na familia zilizovunjika. Tangu kuanza kwa vita, Papa Francisko ametaka kufanya kazi chini ya kanuni ya "ukaribu sawa" kwa wale wanaoteseka. Kanuni hii ni sahihi kwa Papa, mchungaji wa Kanisa zima, na ni sifa ya diplomasia ya Vatican
Kilio cha uchungu
Papa Francisko alisema anatafuta kufanya kama "mfasiri" wa maumivu "ya makumi ya maelfu ya mama, baba, na watoto wanaoomboleza wapendwa wao walioanguka vitani au wanahangaika juu ya wale waliopotea, waliochukuliwa kufungwa, au kujeruhiwa, iwe kuwa mwanajeshi au raia.” “Kilio chao kinainuka kwa Mungu, kikiomba amani badala ya vita, mazungumzo badala ya kishindo cha silaha, mshikamano badala ya ubinafsi, kwa sababu mtu hawezi kamwe kuua kwa jina la Mungu.”
Kujenga upya amani
"Muda wa uchungu na wa muda mrefu wa vita hivi unatupa changamoto kwa haraka, ukituita kwa jukumu la kutafakari pamoja jinsi ya kupunguza mateso ya wale walioathiriwa na kujenga upya amani," Papa aliandika. Barua yake ilitiwa saini mnamo tarehe 12 Desemba 2024 kabla ya Noleli lakini ilitolewa Jumamosi, tarehe 14 Desemba 2024. "Sote tumefungwa na wajibu wa pande zote, katika roho ya udugu wa kweli wa kibinadamu," aliongeza, akisisitiza wasiwasi wake wa kibinafsi kwa "ripoti za mateso yaliyosababishwa na vita katika eneo hilo."
Ndugu Karamazov na mateso ya wasio na hatia
Kumekuwa na ripoti nyingi za uvamizi wa anga, raia kuuawa kwa mabomu, kuongezeka kwa shehena ya silaha, na usitishaji mapigano ambao unaonekana kutoweza kufikiwa. Hata hivyo, kinachomsumbua zaidi Papa Francis, alisema, ni juu ya mateso yote ya wasio na hatia. Katika barua yake, Papa alizungumzia utamaduni wa Kirusi, akimtaja mmoja wa waandishi waliopendwa sana naye, ‘Fyodor Dostoevsky’, na kitabu chake ‘The Brothers Karamazov.’ Alikumbusha mazungumzo, yaliyo katika sura ya nne ya Kitabu V, ambamo Ivan, mmoja wa Ndugu, anamweleza Alyosha kukataa kwake ulimwengu wa Mungu kwa sababu ya kuteseka kwa wanadamu, hasa kule kwa watoto. Papa amekuwa akitaja tukio hilo mara kadhaa katika kipindi cha upapa wake. "Mateso yanayoletwa kwa wasio na hatia ni shutuma kali dhidi ya kila aina ya jeuri."
Jitihada mpya za kidiplomasia
Papa Francisko alisema anaungana na kilio cha wale wanaoteseka, akisema moyo wake "umehuzunishwa na maisha yaliyovunjika, uharibifu, na mateso, pamoja na jeraha kubwa lililosababishwa na familia ya binadamu na vita hivi." "Ninaamini kwamba juhudi za kibinadamu zinazoelekezwa kwa walio hatarini zaidi zinaweza kufungua njia kwa juhudi mpya za kidiplomasia, muhimu kusimamisha kuendelea kwa mzozo na kufikia amani iliyosubiriwa kwa muda mrefu," Papa alisema.
Kuomba zawadi ya amani
Hatimaye, akitazama kuelekea “njia hii ya kawaida,” Papa Francisko alikumbuka maneno ya “mtu mwenye hekima wa Mungu, anayependwa sana na watu wa Urusi,” Mtakatifu Seraphim wa Sarov. "Jipatie roho ya amani, na maelfu ya watu karibu nawe wataokolewa." Barua ya Papa inajumuisha maneno yale yale ya Kisiriliki: "Стяжи дух мирен и тысячи вокруг тебя спасутся."
Kwa kuhitimisha Papa Francisko alimwalika “kila mmmoja mwenye mapenzi mema kujumuika katika sala kwa Mungu, wakiomba zawadi ya amani, na katika kujitolea kuchangia lengo hili tukufu, kwa manufaa ya wanadamu wote.”