Tafuta

Mkutano wa Vijana wa Ulaya ulioandaliwa na Jumuiya ya Kiekumene ya Taizé huko  Tallin,Estonia,28 Desemba 2024 - 01 Januari 2025. Mkutano wa Vijana wa Ulaya ulioandaliwa na Jumuiya ya Kiekumene ya Taizé huko Tallin,Estonia,28 Desemba 2024 - 01 Januari 2025. 

Papa kwa vijana wa Taize:dunia inakabiliwa na majaribu makubwa

Katika ujumbe uliotiwa saini na Kardinali Parolin,Katibu wa Vatican Papa anawalekea washiriki wa mkutano wa Vijana wa Ulaya uliandaliwa na Jumuiya ya Kiekumene ya Taizé huko Tallinn nchini Estonia:"katikati ya migogoro na vurugu ni kukuza roho ya kushirikiana na udugu,kuondokana na uchovu,migogoro na wasiwasi."

Na Angella Rwezaula – Vatican.

Jumuiya ya Kiekumene ya Taizé uandaa siku za Mkutano mwishoni mwa kila Mwaka ambapo kwa mwaka huu Mkutano huo umefikia toleo la arobaini na saba la Vijana wa Ulaya uliozinduliwa kuanzia tarehe 28 Desemba 2024 hadi tarehe 1 Januari 2025 nchini Estonia. Ni katika fursa hiyo ambapo Baba Mtakatifu Francisko amewatumia ujumbe wake, uliotiwa saini na Katibu wa Vatican, Kardinali Pietro Parolin. Katika Ujumbe huo unasema: “Wapendwa vijana, Ni katika mwambao wa Baltic, huko Tallinn, ambapo mmekusanyika mwaka huu kwenye hafla ya Mkutano wa 47 wa Vijana wa Ulaya huko Tallinn, mji mkuu wa Estonia. Baba Mtakatifu Francisko anatuma salamu zake  kwao, pamoja na ndugu wa jumuiya, viongozi wa madhehebu mbalimbali ya Kikristo nchini Estonia na watu wote wenye mapenzi mema wanaowakaribisha mwishoni mwa mwaka.

Ziaya ya Papa katika Nchi tatu za kibaltic

Wakati wa ziara  yake ya kitume katika nchi tatu za Baltic mnamo mwaka wa 2018, Baba Mtakatifu alikutana na vijana katika Kanisa la Kilutheri la Kaarli, huko Tallinn, na kutamka maneno ambayo pia yanaelezea kile wanachopitia siku hizi kwamba: “Ni vyema kujumuika pamoja, kushiriki shuhuda za maisha, kueleza kile mnachofikiri na kutaka; na inapendeza sana kuwa pamoja, sisi tunaomwamini Yesu Kristo”(Mkutano wa Kiekumene na vijana, 25 Septemba 2018). Kwa njia hiyo kuwa pamoja katika roho ya kushirikiana na udugu: ni muhimu zaidi katika muktadha wa sasa, wakati ulimwengu wetu unapitia majaribu magumu. Nchi nyingi zimegubikwa na ghasia na vita, watu wengi ni wahathiriwa wa kutendewa kinyama, bado wengine wamechanganyikiwa kutokana na kukosekana kwa usawa katika jamii zetu na hatari za kiikolojia. Lakini katika siku hizi huko Tallinn wanataka "kutumaini dhidi ya matumaini yote", kama kichwa cha barua ambayo Ndugu Matthew, kabla ya mkutano wa  Taizé, aliandika kwaajili ya  mwaka unaokaribia kuanza. Kwa njia hiyo Ombi hilo, kwa kupatana na kaulimbiu ya mwaka wa Jubilei yenye  sifa ya 2025, pia inaelekezwa kwa vijana, kwa kila mmoja wao kwamba “watembee na kwa matumaini!”

Tumaini hushinda kila uchovu

Tumaini hushinda kila uchovu, kila shida na kila wasiwasi, na kutupatia motisha kubwa ya kusonga mbele, kwa sababu ni zawadi ambayo tunapokea kutoka kwa Mungu mwenyewe: Inajaza wakati wetu kwa maana, hutuangazia njia, hutuonesha mwelekeo na lengo la maisha" (Ujumbe wa Siku ya Vijana ya XXXIX Duniani, 24 Novemba 2024). “Wapendwa vijana, Baba Mtakatifu anawategemea na kuwapyaisha imani ambayo Kanisa linaweka ndani yenu, kwa sababu Kanisa la ulimwengu wote linawahitaji vijana  kutangaza habari njema ya upendo wa Mungu leo hii. Pia ni maana ya njia ya sinodi ambayo imefanywa na Kanisa Katoliki na ambayo imesababisha maendeleo makubwa katika urafiki wa kiekumene na kaka na dada zetu wa madhehebu mbalimbali ya Kikristo. Akimkabidhi kila mmoja wao na familia zao kwa Bwana, kwa maombezi ya Bikira Maria, Baba Mtakatifu Francisko anawakirimia kwa moyo wote baraka zake za kitume na kuwaomba wamuombee.

Ujumbe wa Papa kwa vijana wa Taize
30 December 2024, 16:28