Tafuta

Wakatoliki nchini Nicaragua wakiwa na picha ya Bikira Maria  na Bendera ya nchi yao. Wakatoliki nchini Nicaragua wakiwa na picha ya Bikira Maria na Bendera ya nchi yao. 

Barua ya Papa kwa waamini Nicaragua:msiwe na shaka na Mungu,hata katika nyakati ngumu zaidi!

Papa ameandika Barua ya kichungaji kwa waamini wa nchi ya Nicaragua ambapo kwa sasa waamini wanasali Novena ya Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili.Katika barua hiyo anaeleza kuwa sherehe hii katika fursa ya ufunguzi wa Jubilei ya 2025,inaweza kutoa faraja wanayohitaji wakati wa shida na ukosefu wa uhakika.Papa anawahakikishia watu hawa kusali bila kuchoka kwa Bikira Maria ili awafariji na kuwasindikiza huku akiwathibitisha katika imani.

Na Angella Rwezaula – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko amewaandikia watu wa Mungu ambao walioko katika hija nchini Nicaragua tarehe 2 Desemba 2024 katika Barua ya Kichungaji yenye kauli mbiu: Nani husababisha furaha nyingi? Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili! Ifuatayo ni barua hiyo ya kichungaji kwa watu hawa ambao wanasali Novena ya Siku 9 kuelekea Siku Kuu ya Maria tarehe 8 Desemba. Wapendwa kaka na dada katika Kristo, wapendwa wa Kanisa huko Nicaragua.  Kwa muda,  nimetaka kuwaandikia barua ya kichungaji ili kurudia, kwa mara nyingine tena, upendo nilio nao kwa watu wa Nicaragua, ambao siku zote wamejitokeza kwa ajili ya upendo wao usio wa kawaida kwa Mungu, ambaye mnamwita kwa upendo Papachu. Niko pamoja nanyi, hasa katika siku hizi mnasali Novena ya Mama Maria Mkingiwa  wa dhambi ya Asili (Immaculate Conception.) Msisahau Maongozi ya upendo ya Bwana, ambayo yanatusindikiza na ni mwongozo pekee wa uhakika. Kwa usahihi katika nyakati ngumu zaidi, ambayo inakuwa haiwezekani kibinadamu kuelewa kile ambacho Mungu anataka kutoka kwetu, tunaitwa kutokuwa na shaka uangalifu wake na huruma yake. Imani ya kimwana mliyo nayo Kwake, na pia uaminifu wenu kwa Kanisa, ni miale miwili mikuu inayoakisi uwepo wenu.

Muwe na hakika kwamba imani na tumaini hutenda miujiza. Hebu tumtazame Bikira Safi wa Moyo, Yeye ndiye shuhuda angavu ya uaminifu huu. Ninyi daima mmewahi kupata  uzoefu wa ulinzi wake wa uzazi katika mahitaji yenu  yote na mmeonesha shukrani zenu kwa udini mzuri sana na wenye utajiri wa kiroho. Mojawapo ya mtindo wa namna hizi,  za  kujitoa na kujiweka wakfu ambazo hudhihirisha furaha ya kuwa watoto wake wapenzi, ni usemi mtamu wa: 'Ni nani anayesababisha furaha  nyingi hivyo?  Maria  Mkingiwa wa dhambi!' Ninatamani kwamba maadhimisho haya ya moyo safi wa Mkingiwa dhambi , ambayo inatutayarisha kwa ufunguzi wa Jubilei ya 2025, iwapatie faraja inayohitajika wakati wa shida, na kutokuwa na uhakika na kunyimwa. Katika sherehe hii, msisahau kujiachia mikononi mwa Yesu na kwa sala za kurudia "Dios primiero", yaani “Mungu kwanza,” ambayo mnarudia mara nyingi.

Ninapenda ukaribu wangu uwafikie na uhakika kwamba ninamwomba Bikira Maria bila kukoma ili awafariji na kuwasindikiza, nikiwathibitisha katika imani yenu. Ninataka kuwambia kwa nguvu: Mama wa Mungu haachi kuwaombea  na tusiache kumwomba Yesu awashike mikono yenu daima. Kutembea pamoja tukiungwa mkono na ibada nyororo kwa Maria kunatufanya tufuate njia ya Injili kwa kujitolea na hutuongoza kupyaisha tumaini letu kwa Mungu. Ninafikiri hasa sala ya Rozari ambapo kila siku tunatafakari mafumbo ya maisha Yesu na Maria. Ni mara ngapi tunajumuisha maisha yetu wenyewe katika mafumbo ya Rozari Takatifu, pamoja na nyakati zake za furaha, uchungu, mwanga na utukufu. Kwa kusali Rozari, mafumbo haya hupitia ukaribu wa mioyo yetu, ambapo uhuru wa binti na wana wa Mungu hupata makao, ambayo hakuna mtu anayeweza kutunyang’anya. Ni neema ngapi tunapokea kutoka katika Rozari, ni sala yenye nguvu. Ninawakabidhi kwa ulinzi wa Mama Mkingiwa. Ninyi mlimchagua kuwa Mama wa watu wenu.  Hili linadhihirishwa na kilio rahisi na cha kujiamini sana: Maria wa Nikaragua, Nikaragua ya Maria! Na iwe hivyo.

Wapendwa kaka na dada wa Nicaragua, kwa kumalizia tusali  pamoja maombi niliyoandika kwa ajili ya Jubilei, tukimwomba Bwana atupe amani na neema zote tunazohitaji: “Baba uliye mbinguni, imani uliyotupa katika Mwanao Yesu Kristo, ndugu yetu, na mwali wa upendo uliomiminwa katika mioyo yetu na Roho Mtakatifu, ufufue ndani yetu tumaini lenye baraka la ujio wa Ufalme wako. Neema yako na itubadilishe kuwa wakulima wenye bidii wa mbegu za kiinjili zinazochachua ubinadamu na ulimwengu, katika kutazamia kwa uhakika mbingu mpya na dunia mpya, wakati nguvu za uovu zitakaposhindwa, utukufu wako udhihirike milele. Neema ya Jubilei na ihuishe ndani yetu, Mahujaji wa Tumaini, hamu ya mali ya mbinguni na kumimina furaha na amani ya Mkombozi wetu juu ya ulimwengu wote. Kwako Ee Mungu upewe sifa na utukufu milele. Amina.

Barua ya Papa ya Jubilei 2025: Tumaini halikatishi tamaa(Rm5,5)

Ndugu msilikizaji tukumbuke wakati wa kutangaza Mwaka Mtakatifu, Baba Mtakatifu alitoa Tamko la Maadhimisho ya Jubilei ya Mwaka 2025 ya Ukristo ikiongozwa na  kauli mbiu “Spes non confundit" yaani “Tumaini halitahayarishi”(Rm 5:5) au halikatishi tamaa na kwamba, (Rej Barua kamili ya Papa kwa ajili ya Jubilei: QUI IL TESTO INTEGRALE DELLA BOLLA DI INDIZIONE DEL GIUBILEO "SPES NON CONFUNDIT")kiini cha maadhimisho haya ni matumaini yatakayowawezesha watu waamini wa Mungu kutoka sehemu mbalimbali za dunia kufanya hija ya maisha ya kiroho mjini Roma lakini vilevile  na maadhimisho haya kufanyika kwenye Makanisa mahalia, ili kukutana na Kristo Yesu aliye hai na ambaye pia ni Mlango wa uzima.

Hata hivyo Papa akianza mwanzo aliandikia kuwa: “Katika roho ya matumaini, Mtume Paulo alizungumzia maneno haya ya kutia moyo kwa jumuiya ya Wakristo wa Roma. Matumaini pia ni ujumbe mkuu wa Jubile ijayo ambayo, kwa mujibu wa mapokeo ya kale, Papa anatangaza kila baada ya miaka ishirini na mitano. Mawazo yangu yanawaelekee mahujaji wote wa matumaini watakaosafiri kwenda Roma ili kuuonja Mwaka Mtakatifu na wale wengine ambao, ingawa hawawezi kuutembelea Mji wa Mitume Petro na Paulo, watausherehekea katika Makanisa yao mahalia. Kwa kila mtu, Jubilei na iwe ni wakati wa kukutana kiukweli, kibinafsi na Bwana Yesu, “mlango” (rej. Yn 10:7.9) wa wokovu wetu, ambao Kanisa limeagizwa kumtangaza daima, kila mahali na kwa wote kama “tumaini letu” (1 Tim 1:1).

Papa alibanisha kuwa: “Kila mtu anajua ni nini maana ya kutumaini. Katika moyo wa kila mtu, tumaini hukaa kama shauku na matarajio ya mambo mema yajayo, licha ya kutojua nini kinaweza kutokea wakati ujao. Hata hivyo, nyakati fulani kutokuwa na hakika kuhusu wakati ujao kunaweza kutokeza hisia zinazopingana, kuanzia kutumainiana hadi kuogopa, kutoka katika utulivu hadi wasiwasi, kutoka katika usadikisho thabiti hadi kusitasita na shaka. Mara nyingi tunakutana na watu ambao wamekata tamaa, wasio na matumaini na wasio na maoni juu ya siku zijazo, kana kwamba hakuna kitu kinachoweza kuwaletea furaha. Kwetu sote, Jubilei na iwe fursa ya kupyashwa kwa matumaini. Neno la Mungu hutusaidia kupata sababu za tumaini hilo. Tukilichukua kama mwongozo wetu, na turudi kwenye ujumbe ambao Mtume Paulo alitaka kuwasilisha kwa Wakristo wa Roma.

Barua ya Papa kwa waamini Nicaragua
02 December 2024, 15:53