Siku ya 58 ya Kuombea Amani Duniani 2025: Bikira Maria Mama wa Mungu
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S., - Vatican.
Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko katika Maadhimisho ya Siku ya 58 ya Kuombea Amani Duniani tarehe Mosi, Januari 2025 unanogeshwa na kauli mbiu “Utusamehe Makosa Yetu: Utupe Amani.” Huu ni mwaka wa Maadhimisho ya Jubilei kuu ya miaka 2025 ya Ukristo inayokita ujumbe wake katika roho ya matumaini. Hii ni siku ambayo Mama Kanisa anaadhimisha pia Sherehe ya Bikira Maria Mama wa Mungu. Itakumbukwa kwamba, Amani ni msingi wa wema, heshima na maendeleo fungamani ya binadamu; ni paji na zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu inayomshirikisha na kumwajibisha binadamu. Amani ni tunda la upendo linalopaswa kuboreshwa kwa njia ya malezi ya dhamiri nyofu; ukweli na uhuru; usalama wa raia na mali zao; kwa kulinda na kuheshimu utu wa binadamu, ustawi na maendeleo ya wengi. Kwa ufupi, amani ni kazi ya haki na matunda ya upendo! Amani duniani inatishiwa sana na mashindano ya silaha, utengenezaji pamoja na mchakato wa ulimbikizaji wa silaha duniani! Ni wajibu wa Jumuiya ya Kimataifa kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha amani duniani! Vita ni chanzo kikuu cha maafa, mateso na mahangaiko ya binadamu!
Mama Kanisa tarehe Mosi Januari ya kila Mwaka anaadhimisha Sherehe ya Bikira Maria Mama wa Mungu: Kwa lugha ya Kigiriki: Theotokos, Θεοτόκος; kwa Kilatini “Deipara” au “Dei genitrix.” Na kama sehemu ya maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo inayonogeshwa na kauli mbiu “Mahujaji wa Matumaini”, litafunguliwa Lango la Kanisa kuu la Bikira Maria Mkuu, Jimbo kuu la Roma. Kiri ya imani kwa Bikira Maria Mama wa Mungu, Bikira Maria Mama wa Kristo ni mfano bora wa kuigwa katika kulinda na kudumisha imani inayomwilishwa katika ushuhuda. Ilikuwa ni tarehe 26 Juni 431 katika maadhimisho ya Mtaguso wa Efeso, Mababa wa Kanisa walipotamka kwamba, yule ambaye Bikira Maria amemchukua mimba kama mtu na ambaye amekuwa ni Mwana wake kadiri ya mwili, ndiye Mwana wa milele wa Baba, Nafsi ya Pili ya Fumbo la Utatu Mtakatifu. Kanisa linaungama kwamba, kweli Bikira Maria ni “Mama wa Mungu” “Theotokos, Θεοτόκος.” Hiki ndicho kiini cha Taalimungu na Ibada kwa Bikira kwa sababu mhusika mkuu ni Mwenyezi Mungu. Katika Agano Jipya, Bikira Maria anatambulikana kuwa ni Mama wa Yesu.
Tangu mwanzo, Kanisa lilimtambua Bikira Maria kuwa ni Mama wa Mungu lakini kiri hii ya imani ikaendelezwa na kufikia kilele chake kwenye Mtaguso wa Efeso ili kukabiliana na changamoto zilizoibuliwa na wazushi wa nyakati zile, waliokuwa wanapinga Umungu wa Kristo. Mtaguso wa Efeso ukaweka mafundisho haya kuwa ni sehemu ya Kanuni ya Imani, muhtasari wa mafundisho makuu ya Kanisa. Kristo Yesu alitungwa mimba tumboni mwa Bikira Maria kwa nguvu ya Roho Mtakatifu. Kumbe, Kristo Yesu ni Mungu kweli na Mtu kweli. Katika karne ya tatu kulizuka mgogoro kuhusu Umungu wa Kristo na Ubinadamu wake. Mtaguso wa Efeso ulifafanua kwa kina na mapana kuhusu imani ya Kanisa na kwamba, Bikira Maria ni Mama wa Mungu. Waamini wa Efeso wakashangilia sana na huo ukawa ni mwanzo wa kukua na kuendelea kuimarika kwa Ibada kwa Bikira Maria Mama wa Mungu tangu wakati huo hadi sasa. Bikira Maria ni Mama pia wa maisha ya kiroho kama alivyofafanua Mtakatifu Augustino, Askofu na Mwalimu wa Kanisa. Bikira Maria alitekeleza mapenzi ya Mungu katika maisha yake, akawa ni zaidi ya mfuasi wa Kristo kwa sababu alikuwa kwanza kabisa ni Mama wa Kristo. Huu ni uhusiano wa ndani kabisa uliojengeka kati ya Bikira Maria na Kristo Yesu kutokana na imani thabiti ya Bikira Maria. Bikira Maria Mama wa Mungu ni cheo kikubwa kutokana na upendeleo na neema aliyopata kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Hiki ni kiini cha imani ya Kanisa. Bikira Maria Mama wa Mungu kama anavyofafanuliwa kwenye Maandiko Matakatifu anapaswa kuwa ni kiungo cha umoja na mshikamano miongoni mwa Wakristo na kamwe asiwe ni sababu ya mipasuko, kinzani, migawanyiko na utengano.
Siku ya Kuombea Amani Duniani, ilianzishwa na Mtakatifu Paulo VI, tarehe Mosi, Januari 1968. Mtakatifu Yohane XXIII katika Wosia wake wa Kitume, “Pacem in terris” yaani “Amani Duniani” anasema amani ya kweli inafumbatwa katika: ukweli, haki, upendo na uhuru. Naye Mtakatifu Paulo VI anasema, amani ni jina jipya la maendeleo endelevu na fungamani ya binadamu. Kumbe, kuna haja ya kukuza na kudumisha utamaduni wa kuheshimu haki msingi za binadamu na kwamba, kila mtu anapaswa kuwajibika, ili kujenga na kuimarisha mafungamano ya kijamii na mahusiano pamoja na Mwenyezi Mungu. Waamini na watu wote wenye mapenzi mema wanapaswa kutangaza na kushuhudia Injili ya amani duniani kwa kuzingatia utu, heshima ya binadamu na haki zake msingi. Ujumbe Baba Mtakatifu kwa ajili ya Siku ya Kuombea Amani Duniani hutumwa kwa wakuu wa nchi na Jumuiya ya Kimataifa na pia ujumbe huu huonesha dira na mwelekeo wa utendaji wa shughuli za kidiplomasia zitakazotekelezwa na Vatican katika kipindi cha Mwaka mzima. Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko katika Maadhimisho ya Siku ya 58 ya Kuombea Amani Duniani tarehe Mosi, Januari 2025 unanogeshwa na kauli mbiu “Utusamehe Makosa Yetu: Utupe Amani.” Katika ujumbe huu, Baba Mtakatifu anakazia kuhusu maadhimisho ya Jubilei kuu ya Miaka 2025 ya Ukristo yanayokita mizizi yake katika msamaha, uhuru na upatanisho kwa kujenga na kudumisha haki ya Mungu na hivyo kubomolea mbali mifumo ya ukosefu wa amani. Huu ni mwaliko wa kusimama kidete kulinda na kudumisha utu, heshima na haki msingi za binadamu na hasa wakimbizi na wahamiaji; utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Hii ni changamoto ya kufanya mabadiliko, kwa kutambua kwamba, binadamu wote ni wadeni, wanahitaji toba na msamaha; upendo na mshikamano bila kusahau msamaha wa deni kubwa la nje linalozielemea nchi changa zaidi ulimwenguni. Huu ni mwaliko wa msamaha unaosimikwa katika mshikamano wa udugu wa kibinadamu, lakini zaidi ni sehemu ya mchakato wa ujenzi wa haki.
Baba Mtakatifu anasema, maadhimisho ya Jubilei ni hija ya matumaini inayopata chimbuko lake katika huruma na upendo wa Mungu usiokuwa na kifani, wito wa kusikiliza na kujibu kilio cha maskini na dunia mama; kwa kuwaganga na kuwatibu wale waliopondeka na kuvunjika moyo; ili kudumisha utu, heshima na haki msingi za binadamu. Deni kubwa la nje linalozielemea Nchi changa zaidi duniani ni tishio kwa ustawi na maendeleo ya nchi hizi. Kumbe kuna haja ya kutambua deni la kiikolojia na hivyo Jumuiya ya Kimataifa kuanzisha mfumo wa fedha unaosimikwa katika mshikamano na haki. Baba Mtakatifu anaitaka Jumuiya ya Kimataifa kulinda na kudumisha Injili ya uhai tangu pale mtoto anapotungwa mimba hadi mauti ya kawaida yanapomfika kadiri ya mpango wa Mungu. Baba Mtakatifu anaitaka Jumuiya ya Kimataifa kufutilia mbali adhabu ya kifo kwa sababu inakwenda kinyume cha haki msingi za binadamu, matumaini ya msamaha, toba na wongofu wa ndani. Jumuiya ya Kimataifa itenge fedha ili kupambana na baa la njaa linalosigina utu, heshima na haki msingi za binadamu, ili kuweka msingi wa maendeleo endelevu sanjari na mapambano dhidi ya athari za mabadiliko ya tabianchi, tayari kujenga amani na utulivu! Kama Mzaburi asemavyo “Fadhili na kweli zimekutana, haki na amani zimebusiana” huu ni wito wa kurejesha tena amani ya Mungu duniani, kama lengo la kudumisha amani inayobubujika kutoka moyoni na wala si katika hofu ya vita. Baba Mtakatifu anatamani kuona amani inashamiri katika kipindi cha mwaka 2025, amani inayopata chimbuko lake kutoka kwa Mungu; amani inayosimikwa katika msamaha na matumaini kama sehemu ya ujenzi wa ulimwengu ulio bora zaidi. Amani ya kweli inajengwa katika msingi wa udugu wa kibinadamu. Baba Mtakatifu anamwomba Mwenyezi Mungu aweze kuwakirimia waja wake amani, awasamehe makosa yao na hatimaye, awakirimie amani, msamaha wa deni kubwa la nje sanjari na kusikiliza na kujibu kilio cha maskini na kilio cha dunia mama.