Tafuta

Papa alifungua Mlango Mtakatifu Usiku wa tarehe 24 Desemba Papa alifungua Mlango Mtakatifu Usiku wa tarehe 24 Desemba  (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Papa Francisko,tafakari kwa BBC:'Matumaini na fadhili' yanagusa moyo wa Injili!

Tafakari kuhusu “matumaini na fadhili”ambayo Papa Francisko alitumwa kwenye BBC ilitangazwa asubuhi ya tarehe 28 Desemba 2024 wakati wa kipindi cha:"Fikra kwa ajili ya Siku."Katika tafakari Papa anabainisha kuwa:"Desemba 24 iliyopita,Mwaka wa Jubilei ulianza kipindi ambacho tunaitwa kuwa mahujaji wa matumaini.Hata kama hatujui kesho inatuhusu nini,haitusaidii chochote kuangalia siku zijazo kwa kukata tamaa na kujiuzulu."

Na Angella Rwezaula – Vatican.

"Tumaini na fadhili" ni kichwa cha tafakari ya Baba Mtakatifu Francisko aliyoyuma kwa Idhaa ya Kiingereza ya BBC na kutangazwa asubuhi ya tarehe 28 Desemba 2024 wakati wa kipindi cha "Thought for the Day," yaani  “Fikra ya Siku." Katika tafakari hiyo Papa anaanza kusema: “Nimeombwa kuwaambia kuhusu matumaini na fadhili. Ninawashukuru. Mambo haya mawili yanagusa moyo wa Injili na yanaonesha njia ya kufuata ili kuongoza tabia zetu. Na nzuri zaidi ni ulimwengu uliojaa tumaini na fadhili. Jamii inayotazama wakati ujao kwa kujiamini na kuwatendea watu kwa heshima na huruma ina utu zaidi.”

Upendo hufanya mioyo yetu kuwa na bidii na ujasiri

Papa aliendelea kusema kuwa “Kama mnavyojua, Desemba 24 iliyopita, Mwaka wa Jubilei ulianza, kipindi ambacho tunaitwa kuwa mahujaji wa matumaini. Hata kama hatujui kesho inatuhusu nini, haitusaidii chochote kuangalia siku zijazo kwa kukata tamaa na kujiuzulu. Vita, ukosefu wa haki wa kijamii, aina nyingi za jeuri tunazopata kila siku hazipaswi kutuingiza kwenye kishawishi cha mashaka na kuvunjika moyo. Tunachagua upendo, na upendo hufanya mioyo yetu kuwa na bidii na ujasiri. Wale wanaopenda, hata kama wanajikuta katika hali hatari, daima hutafakari ulimwengu kwa mtazamo wa upole wa matumaini.”

Fadhili si mkakati wa kidiplomasia ni pendo unaofungua mioyo

Baba Mtakatifu Francisko anasisitiza kuwa “Fadhili si mkakati wa kidiplomasia, wala si tabia rasmi ya kufuatwa ili kuhakikisha maelewano ya kijamii au kupata manufaa ya asili nyingine. Fadhili ni aina ya upendo ambayo hufungua mioyo ya kukubalika na kusaidia kila mtu kuwa mnyenyekevu zaidi. Unyenyekevu ni muhimu kama nini! Unyenyekevu hutanguliza mazungumzo, husaidia kushinda kutokuelewana na hutoa shukrani. Katika suala hili, ningependa kumtaja mwandishi mkuu wa Uingereza Gilbert Keith Chesterton, ambaye pia aliheshimiwa sana na mshairi wa Argentina Jorge Luis Borges. Mwishoni mwa wasifu wake, Chesterton anatualika kwa busara "kuchukua vitu vya maisha kwa shukrani na kutovichukulia kuwa vya kawaida" (wasifu, sura ya 16).

Matumaini ni fadhila ya kitaalimungu pamoja na imani na mapendo

Papa Francisko  kadhalika anasema kuwa “Ninahitimisha kwa matashi ya matumaini, ambayo ni fadhila ya kitaalimungu, pamoja na imani na mapendo: Ninatumaini kwamba katika Jubilei hii tunaweza kuonesha fadhili  kama aina ya upendo wa kuhusiana na wengine. Mwaka mpya utuletee amani, udugu na shukrani. Asante!”

Chini ni kiungo cha sauti ya matangazo, ambayo yalipeperushwa asubuhi ya tarehe 28 Desemba 2024. Unaweza kusikiliza kusikiliza kwa kubonyeza: https://www.bbc.co.uk/sounds/play/p0kfgbhp.

Papa na BBC
30 December 2024, 16:54