Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko Urbi et Orbi, Noeli ya Mwaka 2024. Maadhimisho ya Jubilei kuu ya Miaka 2025 ya Ukristo Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko Urbi et Orbi, Noeli ya Mwaka 2024. Maadhimisho ya Jubilei kuu ya Miaka 2025 ya Ukristo  (Vatican Media)

Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko Urbi Et Orbi Noeli 2024

Sherehe za Noeli: 25 Desemba 2024 Papa amekazia: Huruma na upendo wa Mungu anayesamehe. Lango la matumaini liko wazi, changamoto kwa Jumuiya ya Kimataifa kujikita katika majadiliano yanayosimikwa katika ukweli na uwazi, ili kupata amani ya kudumu, faraja kwa watu wanaoteseka na vita sanjari na upatanisho wa Kitaifa. Mwaka wa Jubilei iwe ni fursa ya kujenga na kudumisha ustawi, maendeleo na mafao ya wengi, kwa kukazia utu, heshima na haki msingi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S., - Vatican.

Salam na Baraka kwa mji wa Roma na Ulimwengu katika ujumla wake, maarufu kama “Urbi et Orbi” zilianza kutolewa kwa mara ya kwanza na Mtakatifu Paulo VI kunako mwaka 1974. Kutokana na maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia ya mawasiliano ya jamii, ujumbe huu unawafikia watu wa Mungu sehemu mbalimbali za dunia kwa njia ya mfumo wa matangazo yanayorushwa kwa njia ya Satellite saba. Baba Mtakatifu Francisko katika Salam na Baraka zake kwa mji wa Roma na Ulimwengu katika ujumla wake, maarufu kama “Urbi et Orbi” wakati wa maadhimisho ya Sherehe za Noeli tarehe 25 Desemba 2024 amekazia kuhusu: Huruma na upendo wa Mungu anayesamehe. Lango la matumaini liko wazi, changamoto kwa Jumuiya ya Kimataifa kujikita katika majadiliano yanayosimikwa katika ukweli na uwazi, ili kupata amani ya kudumu, faraja kwa watu wanaoteseka na vita sanjari na upatanisho wa Kitaifa. Mwaka wa Jubilei iwe ni fursa ya kujenga na kudumisha ustawi, maendeleo na mafao ya wengi, kwa kukazia utu, heshima na haki msingi za binadamu na kwamba, maisha ya binadamu ni matakatifu; ni wakati wa kufuta deni kubwa la Kimataifa linalozielemea nchi zinazoendelea duniani.

Ujumbe wa Urbi et Orbi Noeli ya Mwaka 2024 Jubilei Kuu
Ujumbe wa Urbi et Orbi Noeli ya Mwaka 2024 Jubilei Kuu

Baba Mtakatifu Francisko katika Sherehe ya Noeli tarehe 25 Desemba 2024 alitoa salam na baraka kwa mji wa Roma na Ulimwengu katika ujumla wake, maarufu kama: “Urbi et Orbi”. Katika mkesha wa Noeli, Fumbo la Umwilisho haliachi kamwe kuwashangaza walimwengu, kwani Bikira Maria amemzaa Mwana wa Mungu, ndiye Kristo Bwana, ammevishwa nguo za kitoto, amelala katika hori ya kulishia wanyama. Hivi ndivyo wachungaji wa kondeni walivyomkuta Mtoto Yesu, huku wakiwa wamesheheni furaha na wingi wa jeshi la mbinguni, wakimsifu Mungu, na kusema, “Atukuzwe Mungu juu mbinguni, na duniani iwe amani kwa watu aliowaridhia. Rej Lk 26:6-14. Hili ni tulio lililofanyika takaribani miaka elfu mbili na “ushee iliyopita” wakati Bikira Maria alipopata mimba kwa uwezo wa Roho Mtakatifu, akamzaa Mtoto Yesu na hata katika Ulimwengu mamboleo, Neno la Wokovu linaendelea kumwilishwa na kuwahakikishia watu wa Mungu kwamba, wanapendwa, wanasamehewa, wanarudi tena kwa Mwenyezi Mungu na kwamba, lango la moyo wake daima liko wazi.

Lango la Matumaini liko wazi
Lango la Matumaini liko wazi

Hii ndiyo maana ya Lango Takatifu la Jubilei Kuu, lililofunguliwa na Baba Mtakatifu Francisko, tarehe 24 Desemba 2024 wakati wa Kesha la Noeli kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Hili ni Lango linalomwakilisha Kikristo Yesu, Lango la Wokovu ambalo liko wazi kwa watu wote. Kristo Yesu ni Lango la Baba mwenye huruma; lango ambalo limefunguliwa katikati ya Ulimwengu na katika historia ya mwanadamu, ili watu wote waweze kurejea tena kwa Mungu Baba Mwenyezi. Kristo Yesu ni lango linalowarejesha wanadamu kwa Mungu Baba Mwenyezi. Binadamu wote ni kama kondoo waliopotea na hivyo wanamhitaji Mchungaji na Lango, ili waweze kurejea tena nyumbani kwa Baba wa milele. Kumbe, Kristo Yesu ni mchungaji mwema na Lango. Huu ni mwaliko kwa waamini kuondokana na woga pamoja na wasiwasi, kwani Lango limefunguliwa; Lango liko wazi, ni fursa ya kujipatanisha na Mungu; kujipatanisha kutoka katika nafsi zao wenyewe; kati yao wao wenyewe na hata pamoja na adui zao. Huruma ya Mungu ina uwezo wa kufungua yote yaliyofungwa, kubomolea mbali kuta za utengano sanjari na kuyeyesha moyo wa chuki, tabia ya kutaka kulipiza kisasi na kwamba, Kristo Yesu ni Lango la Amani. Baba Mtakatifu anawataka waamini na watu wote wenye mapenzi mema kupitia katika Lango hili kwa sadaka pamoja na kuachilia mambo mengine yote yanayosababisha kinzani na utengano na hivyo kujiachilia mikononi mwa Mtoto Yesu, Mfalme wa Amani. Baba Mtakatifu anamwalika mwamini mmoja mmoja, watu na Mataifa yote kupitia Lango la Matumaini, wakati huu wa maadhimisho ya Jubilei kuu ya Miaka 2025 ya Ukristo, ili kweli waweze kuwa ni Mahujaji wa Matumaini sanjari na kujitahidi kuhakikisha kwamba, wanazinyamazisha silaha za vita na hivyo na kuachana na kinzani pamoja na migawanyiko kati ya watu.

Mahujaji wa Matumaini
Mahujaji wa Matumaini

Baba Mtakatifu anataka silaha za vita zinyamaze huko nchini Ukraini, tayari kuwa na ujasiri wa kufungua Lango la majadiliano, kwa kukuza na kudumisha utamaduni wa kukutana, ili hatimaye, kuweza kupata amani ya kweli na ya kudumu. Silaha za vita zizimwe huko Mashariki ya Kati; amani na maridhiano yapatikane kati ya Israeli na Palestina na hasa Ukanda wa Gaza ambayo watu wanaoishi katika hali tete sana. Wafungwa na mateka wa kivita waachiliwe huru, ili watu wanaopekenywa kwa njaa na vita waweze kupata msaada. Baba Mtakatifu amependa kuonesha uwepo wake wa karibu kwa Jumuiya ya Wakristo huko Lebanon, na hasa Kusini mwa Lebanon, bila kuishahau Siria inayopitia kipindi kigumu katika historia ya maisha yake. Malango ya haki na amani yafunguliwe kwenye Ukanda wote wa Mashariki ya Kati, ambao umeathirika sana kwa vita na machafuko ya kisiasa. Baba Mtakatifu ametumia fursa hii kuwakumbuka watu wa Mungu nchini Libia na amewatia shime kutafuta suluhu zitakazowesha kukamilika kwa mchakato wa upatanisho wa Kitaifa. Kuzaliwa kwa Kristo Yesu Mkombozi wa Ulimwengu kuwe ni fursa ya matumaini kwa familia na watoto wanaopekenywa nakuangamia kwa virusi vya mpox huko nchini DRC, Bukrina Faso, Mali, Niger na Msumbiji. Hizi ni nchi ambazo zimeathirika kwa vita ya muda mrefu, vitendo vya kigaidi pamoja na madhara makubwa ya mabadiliko ya tabianchi. Matokeo yake ni vifo vya maelfu ya watu; pamoja na maelfu ya watu kukosa makazi ya kudumu. Baba Mtakatifu amewakumbuka watu wa Mungu wanaoishi kwenye Pembe ya Afrika na kuwaombea amani, utulivu na udugu wa kibinadamu. Mtoto Yesu, Mwana wa Baba wa milele, asaidie kufanikisha juhudi za Jumuiya ya Kimataifa za kupeleka misaada ya kiutu nchini Sudan ya Kusini, na pia awezeshe majadiliano katika ukweli na uwazi, ili hatimaye, kuweza kusitisha vita.

Madhara ya vita
Madhara ya vita

Habari Njema ya Noeli ilete faraja kwa watu wa Mungu nchini Myanmar. Hawa ni watu wanaoendelea kuteseka kutokana na vita, kiasi kwamba, wanalazimika kuyakimbia makazi yao. Mtoto Yesu awasaidie viongozi wa kisiasa na watu wote wenye mapenzi mema huko Amerika ya Kusini waweze kupata suluhu ya haraka inayofumbatwa katika ukweli na amani, ili kuweza kujenga na kudumisha utulivu wa kijamii hususan; nchini Haiti, Venezuela, Colombia na Nicaragua, hasa katika kipindi hiki cha Maadhimisho ya Jubilei kuu ya Miaka 2025 ya Ukristo, ili kwa pamoja waweze kujenga na kuimarisha ustawi, maendeleo na mafao ya wengi sanjari na kutambua utu, heshima na haki msingi za kila mtu, kwa kuvuka kinzani na migawanyiko ya kisiasa. Maadhimisho ya Jubilei iwe ni fursa ya kubomolea mbali kuta za utengano: kiitikadi ambayo wakati mwingine zimeleta athari kubwa katika maisha ya kisiasa na kiutu kama hali inavyojionesha katika mgawanyiko uliopo kwenye Kisiwa cha Cyprus, hali ambayo imesababisha mpasuko wa mafungamano ya kijamii kwa zaidi ya miaka hamsini. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu kwamba, wataweza kufikia muafaka hasa katika maadhimisho wa Mwaka wa Jubilei kuu ya Miaka 2025 ya Ukristo, ili haki msingi za binadamu, utu na heshima ya wananchi wa Cyprus viweze kudumishwa. Kristo Yesu, Neno wa Mungu aliyefanyika Mwili ni Lango ambalo liko wazi, mwaliko kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema kupitia ndani mwake ili kutambua na kuthamini utakatifu wa maisha ya kila mtu, ili hatimaye, kugundua tena na tena tunu msingi za maisha ya binadamu.

Biashara haramu ya silaha ni tishio kwa ujenzi wa amani duniani.
Biashara haramu ya silaha ni tishio kwa ujenzi wa amani duniani.

Kristo Yesu anawangoja wote, lakini zaidi wale walio dhaifu, anawangoja watoto, hasa watoto wanaoteseka kutokana na madhara ya vita, njaa na magonwa: Anawasubiri wazee na hasa wanaolazimika kuishi katika hali ya upweke hasi pamoja na kutelekezwa. Anawangoja wale waliopoteza makazi yao, wanaokimbia nchi zao kwa sababu ya vita ili kupata hifadhi madhubuti. Mtoto Yesu anawasubiri kwa shauku kubwa wale wote wasiokuwa na kazi au waliopteza fursa za ajira; anawangoja wafungwa, kwani pamoja na mambo yote hayo, lakini bado wanabaki kuwa ni watoto wateule wa Mungu; kwa hakika anawasubiri wote wanaoteseka, nyanyasika na kudhulumiwa kutokana na imani yao. Mwishoni mwa salam na baraka zake kwa mji wa Roma na Ulimwengu katika ujumla wake, maarufu kama “Urbi et Orbi” wakati wa maadhimisho ya Sherehe za Noeli tarehe 25 Desemba 2024, Baba Mtakatifu Francisko amewashukuru na kuwapongeza wale wote wanaotekeleza vyema dhamana na nyajibu zao kwa ajili ya ustawi na mafao ya wengi katika hali ya ukimya na uaminifu mkubwa hawa ni: Wazazi, walezi na waalimu, watu wenye dhamana na wajibu wa kukiunda kizazi cha sasa na kile kijacho; wahudumu wa matendo ya huruma husasani wamisionari walioenea sehemu mbalimbali za dunia, hawa ndio watu wanaobeba mwanga na faraja kwa watu wenye shida na mahangaiko mbalimbali. Kwa wote hawa, Baba Mtakatifu amewaonesha moyo wake wa shukrani. Maadhimisho ya Jubilei kuu ya Miaka 2025 ya Ukristo iwe ni fursa ya kusamehe deni la nje linaloendelea kuziathiri nchi maskini zaidi ulimwenguni. Huu ni mwaliko wa kupokea na kutoa msamaha, ili Mtoto Yesu aliyezaliwa kwenye baridi na usiku wa giza nene, aweze kuwasamehe madeni yao. Kristo Yesu amekuja ulimwenguni ili kuwaganga, kuwaponya na kuwasamehe watu dhambi zao. Kama mahujaji wa matumaini, huu ni wakati wa kumwendea Kristo Yesu, kwa kufungua malango ya nyoyo zao kama Kristo Yesu alivyowafungulia Lango la Moyo wake Mtakatifu.

Urbi et Orbi Noel 2024
25 December 2024, 14:10