Katika Ujumbe wa Papa Francisko kwa ajili ya Siku ya 58 ya Amani Ulimwenguni unakazia kuondoa madeni kwa walio maskini. Katika Ujumbe wa Papa Francisko kwa ajili ya Siku ya 58 ya Amani Ulimwenguni unakazia kuondoa madeni kwa walio maskini.  (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Ujumbe wa Papa Francisko wa Siku ya 58 ya Kuombea Amani Ulimwenguni:Sote ni wadeni

Papa Francisko,tarehe 12 Desemba 2024 amechapisha Ujumbe wa Siku ya 58 ya Kuombea Amani Ulimwenguni 2025.Umegawanyika sehemu IV zenye vipengele 15.I:Kusikiliza ombi la wanadamu walio katika hatari ya kutoweka,II:Mabadiliko ya kiutamaduni:sisi sote ni wadeni,III:Safari ya Matumani:hatua zatu za kutenda,IV:Lengo la amani."Kila mmoja anaweza kutimiza matendo ya huruma na kuvunja minyoror isiyo na haki."

Na Angella Rwezaula – Vatican.

Kila tarehe Mosi Januari ya kila Mwaka, Mama Kanisa anaadhimisha Sherehe ya Bikira Maria Mama wa Mungu sambamba na Siku ya Amani Uliwenguni. Ni katika mkutadha huo ambapo Baba Mtakatifu tarehe 12 Desemba 2024 ametoa ujumbe wa Amani kwa mwaka 2025 unaoongozwa na kauli mbiu: Utusamehe makosa yetu: utupe amani yako." Ujumbe huu umegawanyika katika sehemu IV zeye vipengele 14. Tunachapisha ujumbe huo kamili wa Baba Mtakatifu.

I. Kusikiliza ombi la wanadamu walio katika hatari ya kutoweka

Katika mapambazuko ya Mwaka huu Mpya tuliopewa na Baba yetu wa mbinguni, mwaka wa Jubilei katika roho ya matumaini, ninawatakia wanaume na wanawake amani kutoka moyoni. Ninawaza hasa wale wanaohisi kukandamizwa, kulemewa na makosa yao ya zamani, wamekandamizwa na hukumu ya wengine na wasio na uwezo wa kuona hata chembe ya matumaini kwa maisha yao wenyewe. Kwa kila mtu ninaomba tumaini na amani, kwa kuwa huu ni Mwaka wa Neema uliozaliwa na Moyo wa Mkombozi!

Katika kipindi chote cha mwaka huu, Kanisa Katoliki linaadhimisha Jubilei, tukio linalojaza matumaini mioyoni. “Jubile” inakumbuka desturi ya kale ya Kiyahudi, wakati, kila mwaka wa arobaini na tisa, sauti ya pembe ya kondoo dume (kwa Kiebrania, Jobeli) ingetangaza mwaka wa msamaha na uhuru kwa watu wote (rej. Law 25:10).  Tangazo hili zito lilikusudiwa kuwa mwangwi katika nchi yote (taz. Law 25:9) na kurejesha haki ya Mungu katika kila nyanja ya maisha: katika matumizi ya ardhi, katika kumiliki mali na katika mahusiano na wengine, zaidi ya yote maskini na wasio na mali. Kupigwa kwa baragumu kuliwakumbusha watu wote, matajiri na maskini, kwamba hakuna mtu anayekuja katika ulimwengu huu akiwa amehukumiwa kukandamizwa: sisi sote ni kaka na dada, wana na binti za Baba mmoja, waliozaliwa kuishi kwa uhuru, kwa mujibu wa sheria, kwa mapenzi ya Bwana (rej. Law 25:17, 25, 43, 46, 55).

"Jubilei inatutaka kusimamia haki ya ukombozi wa Mungu"

Katika siku zetu pia, Jubilei ni tukio linalotutia moyo kutafuta kusimamisha haki ya ukombozi ya Mungu katika ulimwengu wetu. Mahali penye pembe ya kondoo dume, mwanzoni mwa Mwaka huu wa Neema tunatamani kusikia “ombi la kuomba msaada kwa waliokata tamaa ” ambalo, kama kilio cha damu ya Abeli ​​(taz. Mwa 4:10), linainuka kutoka kwa watu wengi sana wa sehemu za ulimwengu wetu , ombi ambalo Mungu hakosi kamwe kusikia. Sisi kwa upande wetu tunajiona tunalazimika kulia na kukemea hali nyingi ambazo dunia inanyonywa na majirani zetu kudhulumiwa. Udhalimu huu unaweza kuonekana mara kwa mara katika mfumo wa kile ambacho Mtakatifu Yohane Paulo II alikiita "miundo ya dhambi", ambayo hutokea sio tu kutokana na udhalimu wa baadhi ya watu lakini pia imeunganishwa na kudumishwa na mtandao wa ushirikiano.

"Kila mmoja ajisikie kuwajibika kwa uharibifu wa dunia"

Kila mmoja wetu lazima ajisikie kwa njia fulani kuwajibika kwa uharibifu ambao dunia, makao yetu ya pamoja, imepatwa, kuanzia na matendo yale ambayo, ingawa kwa njia isiyo ya moja kwa moja tu, yanachochea migogoro inayoikumba familia yetu ya kibinadamu. Changamoto za kimfumo, tofauti lakini zimeunganishwa, zinaundwa na kwa pamoja husababisha uharibifu katika ulimwengu wetu. Ninafikiri hasa, tofauti za kila aina, unyanyasaji wa kinyama unaofanywa kwa wahamiaji, uozo wa mazingira, mkanganyiko unaoletwa kimakusudi na upotoshaji, kukataa kushiriki katika mazungumzo ya aina yoyote na rasilimali nyingi zinazotumiwa kwenye tasnia ya vita. Haya yote, yakichukuliwa pamoja, yanawakilisha tishio kwa kuwepo kwa ubinadamu kwa ujumla. Basi, mwanzoni mwa mwaka huu, tunatamani kusikiliza ombi la wanadamu wanaoteseka ili kuhisi tumeitwa, pamoja na kama mtu mmoja-mmoja, kuvunja vifungo vya ukosefu wa haki na kutangaza haki ya Mungu. Vitendo vya hapa na pale vya uhisani havitoshi. Mabadiliko ya kiutamaduni na kimuundo ni muhimu, ili mabadiliko ya kudumu yaweze kutokea.

II. Mabadiliko ya kiutamaduni: sisi sote ni wadeni

Maadhimisho ya Jubilei yanatuchochea kufanya mabadiliko kadhaa ili kukabiliana na hali ya sasa ya ukosefu wa haki na ukosefu wa usawa kwa kujikumbusha kwamba mali ya dunia haikukusudiwa kwa watu wachache waliobahatika, bali kwa kila mtu. Tunapaswa kukumbuka maneno ya Mtakatifu Basili wa Kaisaria alisema: “Niambie, mambo yako ni yapi? Umeyapata wapi ya kufanya kuwa sehemu ya maisha yako? ... Je, hukutoka tumboni mwa mama yako uchi? Si utarudi tena ukiwa uchi ardhini? Mambo uliyo nayo sasa yametoka wapi? Ukisema kwamba yanakuja kwa bahati nzuri, utamkana Mungu kwa kutomtambua Muumba na kumshukuru Mpaji.” Bila shukrani, hatuwezi kutambua zawadi za Mungu. Lakini katika huruma yake isiyo na kikomo, Bwana hawaachi wanadamu wenye dhambi, lakini badala yake anathibitisha zawadi yake ya uzima kwa msamaha wa kuokoa unaotolewa kwa wote kwa njia ya Yesu Kristo. Ndiyo maana, katika kutufundisha “Baba yetu”, Yesu alituambia tuombe: “Utusamehe makosa yetu” (Mt 6:12).

"Mfumo wa kimataifa wenye roho ya mshikamano"

Mara tu tunapopoteza mtazamo wa uhusiano wetu na Baba, tunaanza kuthamini udanganyifu kwamba uhusiano wetu na wengine unaweza kutawaliwa na mantiki ya unyonyaji na ukandamizaji, ambapo kunaweza kufanya sawa. Kama wasomi wa wakati wa Yesu, ambao walifaidika kutokana na mateso ya maskini, vivyo hivyo leo hii, katika kijiji chetu cha kimataifa kilichounganishwa, mfumo wa kimataifa, isipokuwa unaongozwa na roho ya mshikamano na kutegemeana, husababisha ukosefu wa haki, unaochochewa na ufisadi, ambao unaziacha nchi maskini zikiwa zimenaswa. Mtazamo unaotumia vibaya walio na deni unaweza kutumika kama maelezo mafupi ya "shida ya madeni" ya sasa ambayo yanaelemea nchi kadhaa, zaidi ya zote za Kusini mwa ulimwengu.

"Deni la kiikolojia lina pande mbili za sarafu"

Nimekuwa nikisema mara kwa mara kwamba deni la nje limekuwa njia ya kudhibiti ambapo baadhi ya serikali na taasisi binafsi za fedha za nchi tajiri zinanyonya rasilimali watu na maliasili za nchi maskini zaidi bila ya kujali na bila ubaguzi ili kukidhi matakwa ya masoko yao wenyewe. Kwa kuongeza, watu mbalimbali, ambao tayari wameelemewa na deni la kimataifa, wanajikuta pia wanalazimika kubeba mzigo wa "deni la kiikolojia" linalotokana na nchi zilizoendelea zaidi. Deni la nje na deni la kiikolojia ni pande mbili za sarafu moja, ambayo ni mawazo ya unyonyaji ambayo yameishia kwenye mgogoro wa madeni.  Katika ari ya Mwaka huu wa Jubilei, nahimiza Jumuiya ya kimataifa kufanya kazi ya kusamehe deni la nje kwa kutambua deni la kiikolojia lililopo kati ya Kaskazini na Kusini mwa ulimwengu huu. Huu ni wito wa  mshikamano, lakini juu ya yote kwa ajili ya haki.

Mabadiliko ya kiutamaduni na kimuundo yanayohitajika ili kukabiliana na mgogoro huu yatatokea wakati hatimaye tutatambua kwamba sisi sote ni wana na binti za Baba mmoja, kwamba sote tuko katika deni lake lakini pia kwamba tunahitajiana, katika roho ya uwajibikaji wa pamoja na mseto. Tutaweza "kugundua tena mara moja tu kwamba tunahitajiana" na tuna deni sisi kwa sisi.

III. Safari ya matumaini: mapendekezo matatu

Ikiwa tutatilia maanani mabadiliko haya yanayohitajika sana, Mwaka wa Neema wa Jubilei unaweza kutumika kuweka kila mmoja wetu katika safari iliyofanywa upya ya tumaini, iliyozaliwa na uzoefu wa huruma ya Mungu isiyo na kikomo. Mungu hana deni kwa mtu yeyote, lakini daima huwapa neema na huruma zake kwa wote. Kama vile Isaka wa Ninawi, Padre wa Kanisa la Mashariki wa karne ya saba alivyosema katika mojawapo ya sala zake: “Upendo wako, Bwana, ni mkuu kuliko makosa yangu. Mawimbi ya bahari si kitu kwa wingi wa dhambi zangu, bali yakiwekwa kwenye mizani na kupimwa kwa upendo wako, yanatoweka kama chembe ya mavumbi.”  Mungu hapimi maovu tunayofanya; badala yake, yeye ni mwingi wa "utajiri wa rehema, kwa upendo mkuu aliotupenda" (Efe 2:4). Lakini pia anasikia maombi  ya  maskini na kilio cha dunia. Tungefanya vyema tu kusimama kwa muda, mwanzoni mwa mwaka huu, ili kufikiria huruma ambayo kwayo yeye husamehe dhambi zetu daima na kusamehe kila deni letu, ili mioyo yetu ijae tumaini na amani.

Katika kutufundisha kusali “Baba yetu”, Yesu anaanza kwa kumwomba Baba atusamehe makosa yetu, lakini anapitisha mara moja kwa maneno yenye changamoto: “kama sisi tunavyowasamehe wanaotukosea” (taz. Mt 6:12). Ili kuwasamehe wengine makosa yao na kuwapa tumaini, tunahitaji maisha yetu wenyewe yajazwe na tumaini lile lile, tunda la uzoefu wetu wa huruma ya Mungu. Matumaini hufurika katika ukarimu; hayana hesabu, hayatoi matakwa yaliyofichika, hayajali faida, bali yanalenga jambo moja pekee: kuwainua wale walioanguka, kuponya mioyo iliyovunjika na kutuweka huru kutoka kwa kila aina ya utumwa.

"Kutambua deni la nchi maskini"

Kwa hiyo, mwanzoni mwa Mwaka huu wa Neema, ningependa kutoa mapendekezo matatu yenye uwezo wa kurejesha utu wa maisha ya watu wote na kuwawezesha kuyaweka upya katika safari ya matumaini. Kwa njia hii, mgogoro wa madeni unaweza kushinda na sisi sote tunaweza kutambua tena kwamba sisi ni wadaiwa ambao madeni yetu yamesamehewa. Kwanza, ninatoa upya ombi lililozinduliwa na Mtakatifu Yohane Paulo II katika hafla ya Jubilei Kuu ya Mwaka 2000 kwa kuzingatia "kupunguza kwa kiasi kikubwa, kama si kufuta moja kwa moja, deni la kimataifa ambalo linatishia sana mustakabali wa mataifa mengi." Kwa kutambua deni lao la kiikolojia, ndivyo nchi zilizostawi zaidi zinapaswa kujisikia kuitwa kufanya kila linalowezekana kusamehe madeni ya nchi hizo ambazo haziko katika hali ya kulipa kiasi wanachodaiwa. Kwa kawaida, hili lisije likathibitisha kuwa ni tendo la KIpekee la hisani ambalo linaanzisha upya mzunguko mbaya wa ufadhili na madeni, ni lazima kubuniwa mfumo mpya wa kifedha, utakaopelekea kuundwa kwa Mkataba wa kifedha wa kimataifa unaozingatia mshikamano na maelewano kati ya watu.

"Kuondoa kila kizingizo cha vijana kutoona matumaini ya baadaye"

Pia ninaomba dhamira thabiti ya kuheshimu hadhi ya maisha ya mwanadamu tangu kutungwa mimba hadi kifo cha asili, ili kila mtu aweze kuthamini maisha yake na wote wautazame kwa matumaini mustakabali wa mafanikio na furaha kwao wenyewe na kwa ajili watoto wao. Bila tumaini la wakati ujao, inakuwa vigumu kwa vijana kutazamia kuleta maisha mapya duniani. Hapa ningependa kwa mara nyingine kupendekeza ishara thabiti inayoweza kusaidia kukuza utamaduni wa maisha, yaani kutokomeza hukumu ya kifo katika mataifa yote. Adhabu hii siyo tu inaafikiana na kutokiuka kwa maisha,  lakini  pia inaondoa kila tumaini la mwanadamu la msamaha na kujirekebisha. Zaidi ya hayo, kwa kufuata nyayo za Mtakatifu Paulo wa VI na Papa Benedikto wa XVI, na sisiti kutoa wito mwingine tena, kwa ajili ya vizazi vijavyo. Katika wakati huu wenye vita, hebu tutumie angalau asilimia maalum ya fedha zilizotengwa kwa ajili ya silaha kuanzisha Mfuko wa Kimataifa wa kutokomeza njaa na kuwezesha katika nchi maskini shughuli za elimu zinazolenga kukuza maendeleo endelevu na kupambana na mabadiliko ya Tabia nchi. Tunapaswa kujitahidi kuondoa kila kisingizio kinachowatia moyo vijana kuona maisha yao ya baadaye kuwa yasiyo na tumaini au kutawaliwa na kiu ya kulipiza kisasi kwa damu ya wapendwa wao. Wakati ujao ni zawadi inayokusudiwa kutuwezesha kwenda zaidi ya kushindwa huko nyuma na kutengeneza njia mpya za amani.

IV. Lengo la amani

Wale wanaochukua mapendekezo haya na kuanza safari ya matumaini kwa hakika wataona mapambazuko ya lengo linalotamaniwa sana la amani. Mtunga Zaburi anatuahidi kwamba “fadhili na uaminifu zitakutana; haki na amani zitabusiana” (Zab 85:10). Ninapojinyima kutengeneza silaha ya sifa na kurejesha njia ya matumaini kwa mmoja wa kaka au dada zangu, mimi ninachangia katika kurejesha haki ya Mungu katika dunia hii na, pamoja na mtu huyo, ninasonga mbele kuelekea lengo la amani. Kama Mtakatifu Yohane  XXIII alivyoona, amani ya kweli inaweza kuzaliwa tu kutoka katika  moyo  wa"kupokonywa silaha" ya wasiwasi na hofu ya vita.

"Mioyo iliyobadilika tayari kusaidia wengine"

Mnamo 2025 uwe ni mwaka ambao amani itastawi! Amani ya kweli na ya kudumu ambayo huenda zaidi ya kubishana kuhusu maelezo ya makubaliano na maelewano ya kibinadamu. Na tutafute amani ya kweli ambayo imetolewa na Mungu kwa mioyo isiyo na silaha: mioyo isiyozingatia kuhesabu yaliyo yangu na yaliyo yako; mioyo inayogeuza ubinafsi kuwa utayari wa kuwafikia wengine; mioyo inayojiona kuwa na deni kwa Mungu na hivyo tayari kusamehe madeni yanayowakandamiza wengine; mioyo inayochukua nafasi ya wasiwasi juu ya wakati ujao na kutumaini kwamba kila mtu anaweza kuwa rasilimali kwa ajili ya ujenzi wa ulimwengu bora.

"Kuondoa silaha mioyoni ni jukumu la kila mtu"

Kuondoa silaha katika mioyo ni jukumu  kwa kila mtu, mkubwa kwa mdogo, tajiri na maskini sawa. Wakati fulani, kitu rahisi sana kitafanyika, kama vile "tabasamu, ishara ndogo ya urafiki, sura ya fadhili, sikio lililo tayari, na tendo jema." Kwa ishara kama hizi, tunasonga mbele kuelekea lengo la amani. Tutafika haraka zaidi ikiwa, tunaposafiri pamoja na kaka  na dada zetu, tutagundua kwamba tumebadilika tangu wakati tulipoanza safari. Amani haiji tu na mwisho wa vita,  bali na mapambazuko ya ulimwengu mpya, ulimwengu ambamo tunatambua kwamba sisi ni tofauti, wa karibu zaidi na wa kidugu zaidi kuliko vile tulivyowahi kufikiria iwezekanavyo.

Sala ya Papa 

Bwana, utupatie amani yako! Ndiyo maombi yangu kwa Mwenyezi Mungu ninapowatakia heri ya mwaka mpya Wakuu wa Nchi na Serikali, viongozi wa Mashirika ya Kimataifa, viongozi wa dini mbalimbali na kila mtu mwenye mapenzi mema. Utusamehe makosa yetu, Bwana, kama sisi tunavyowasamehe waliotukosea. Katika mzunguko huu wa msamaha, utupe amani yako, amani ambayo wewe peke yako unaweza kutoa, kwa wale wanaojiruhusu kunyang'anywa silaha mioyoni, kwa wale wanaotaka kusamehe deni za ndugu zao kwa matumaini, kwa wale wasioogopa kukiri deni lao kwako, na kwa wale wasioziba masikio yao wasisikie kilio cha maskini.

Ujunbe wa Papa kwa ajili ya amani 2025
Mhutasari wa Ujumbe wa Papa wa Siku ya Amani duniani 2025

 

12 December 2024, 11:55