Papa Francisko,Ajaccio:Duniani kuna sababu kubwa za maumivu ya mataifa:umaskini,vita,ufisadi na vurugu
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Katika Ziara ya 47 ya Kitume ya Baba Mtakatifu huko Ajaccio, Corsica, katika kufunga Kongamano la Kimataifa “kuhusu Udini wa Watu wa Mungu katika Mediterania,” hatua ya Tatu ya Mkutano wake ilikuwa ni maadhimisho ya Misa Takatifu katika Uwanja wa Austerliz U Cason, ukiwa umejaa umati wa waamini wa kisiwa hicho kizuri. Baba Mtakatifu Francisko akianza mahubiri yake baada ya masomo na Injili alianza kusema “Umati unamwuliza Yohane Mbatizaji, “Tufanye nini basi?” (Lk 3:10 ). Tunapaswa kusikiliza kwa makini swali hili, kwa kuwa linaonesha hamu ya kufanywa upya kiroho na maisha bora. Yohane alitangaza kuja kwa Masiha aliyengojewa kwa muda mrefu, na wale waliosikiliza mahubiri yake walitaka kuwa tayari kwa ajili ya pambano hilo.” Baba Mtakatifu alisema, Injili ya Luka inatuambia kwamba wale wanaoonesha hamu ya uongofu ni "watu wa nje." Siyo Mafarisayo na waalimu wa sheria, bali watoza ushuru na askari waliuliza, “Mwalimu, tufanye nini?” ( Lk 3:12 ). Wale wanaojiona kuwa wenye haki hawajipyaishi.
Kwa upande mwingine, wale wanaohesabiwa kuwa watenda dhambi hadharani, wanatamani kuacha maisha yao ya zamani ya ukosefu wa uaminifu na jeuri, na kuanza maisha mapya. Wale walio mbali wanakuwa karibu wakati wowote Kristo anapokaribia. Yohane aliwajibu wale watoza ushuru na askari kwa kuwasihi wawe waadilifu, wanyoofu na waaminifu (rej. Lk 3:13-14). Tangazo la kuja kwa Bwana huchochea dhamiri. Inawavutia hasa maskini na waliotengwa, kwa sababu haji kuhukumu bali kuokoa wale waliopotea (rej. Lk 15:4-32). Baba Mtakatifu Francisko kwa njia hiyo alisema, sisi leo hii pia tunaweza kuuliza swali lile lile ambalo umati ulimwuliza Yohane Mbatizaji. Katika Kipindi hiki cha Majilio, na tupate ujasiri wa kuuliza bila woga, kwamba Je “Tufanye nini basi?”, ili kuandaa moyo mnyenyekevu na wa kutumainiwa kwa ajili ya kuja kwa Bwana. “Maandiko ambayo tumesikia yanatuonesha njia mbili tofauti za kumngojea Masiha: tunaweza kungoja ama kwa mashaka au kwa tazamio la shangwe. Hebu tutafakari juu ya mitazamo hii ya kiroho,” Papa alisisitiza.
Mtazamo wa kwanza, ule wa kushuku, umejaa kutoaminiana na wasiwasi. Tunapojifikiria sisi wenyewe kila mara na mahitaji yetu wenyewe, tunapoteza roho ya furaha. Badala ya kungoja wakati ujao kwa tumaini, tunauona kwa kutojali. Kwa kushikwa na mahangaiko ya kidunia, hatuko wazi kwa utendaji wa usimamizi wa Mungu. Maneno ya Mtakatifu Paulo yanaweza kutumika kama dawa ya kutuamsha kutoka katika ulegevu wetu: “Msiwe na wasiwasi juu ya kitu chochote” (Flp 4:6). Na kwamba “Acha kuwa na dhiki, kukata tamaa au huzuni.” Papa aliongeza kusema “ ni kwa jinsi gani magonjwa hayo ya kiroho yameenea sana siku hizi, hasa katika maeneo ambako utumiaji hovyo wa bidhaa unatawala! Jamii hizo huzeeka; wanabaki bila kuridhika, kwa kuwa hawajui tena jinsi ya kutoa. Ikiwa tunaishi kwa ajili yetu wenyewe tu, hatutapata furaha kamwe,” Papa alisema.
Mtume anapendekeza suluhisho linalofaa anapoandika, “Katika kila jambo kwa kusali na kuomba pamoja na kushukuru haja zenu na zijulikane na Mungu” (Wafilipi 4:6).” Imani katika Mungu inatoa tumaini! Kongamano ambalo limefanyika hivi punde hapa Ajaccio lilisisitiza umuhimu wa kusitawisha imani na kuthamini umuhimu wa Udini Maarufu wa Watu wa Mungu. Hebu tuchukue kama mfano wa kusali Rozari. Tunapochukua Rozari na kuisali vizuri, inatuzoeza kuweka mioyo yetu juu ya Yesu Kristo kwa kushiriki katika mtazamo wa kutafakari wa Maria. Tunaweza pia kufikiria Uhusiano wa kimapokeo, ambao una mengi ya kutufundisha kuhusu kuwahudumia jirani zetu kwa ukarimu, kwa kazi za huruma ya kiroho na kimwili. Vyama hivi vya waamini, vilivyo tajiri sana katika historia, vinashiriki kikamilifu katika liturujia na sala ya Kanisa, ambayo wanaiboresha kwa nyimbo na ibada zinazopendwa.
Papa Francisko kwa njia hiyo amewatia moyo washiriki wa Udugu wa Udini maarufu kuhudhuria zaidi, hasa kwa wale walio na uhitaji mkubwa, na kwa njia hii kutenda imani yao kupitia matendo ya upendo. Papa ameongeza kusema kuwa hiyo inatuleta katika mtazamo wa pili ambao ni: matarajio ya furaha. Furaha ya Kikristo si ya kina wala si ya muda. Kinyume chake, ni furaha iliyokita mizizi ndani ya moyo na iliyojengwa juu ya msingi imara. Kwa maana hiyo , nabii Sefania angeweza kuwaambia wasikilizaji wake wafurahi, kwa kuwa “BWANA, Mungu wao, yu katikati yao, shujaa aletaye ushindi” ( Sef 3:17 ). Kuja kwa Bwana hutuletea wokovu: hiyo ndiyo sababu ya furaha yetu. Mungu ni "mwenye nguvu", Maandiko yanatuambia. Anaweza kukomboa maisha yetu kwa sababu ana uwezo wa kutimiza yale anayoahidi! Shangwe yetu si kitulizo cha muda mfupi kinachotusaidia kusahau huzuni za maisha. Ni tunda la Roho, lililozaliwa kwa imani katika Kristo Mwokozi, ambaye anabisha kwenye mlango wa mioyo yetu na kutuweka huru kutoka katika huzuni na uchovu. Uwepo wa Bwana katikati yetu ni sababu ya sherehe; inajaza siku zijazo za kila mtu kwa matumaini. Katika ushirika wa Yesu, tunagundua furaha ya kweli ya kuishi na tunakuwa ishara za tumaini ambalo ulimwengu wetu unatafuta kwa hamu sana.
Ishara ya kwanza kati ya hizo ni amani. Yeye ajaye ni Imanueli, Mungu pamoja nasi, awapaye amani wale waliopendelewa na Bwana (rej. Lk 2:14). Tunapojiandaa kumkaribisha Yesu katika kipindi hiki cha Majilio, jumuiya zetu zikue katika uwezo wao wa kusindikiza kila mtu, na kwa namna ya pekee pia wazee. Wazee ni hekima ya watu. Tusiisahau! Na kila mmoja wetu anaweza kufikiria: nifanyeje mbele ya wazee? Niende kuwatafuta? Je, ninapoteza muda wangu pamoja nao? Je, ninawasikiliza? "Hapana, wanachosha na hadithi zao!". Je, ninawaacha? Ni watoto wangapi wanaowatelekeza wazazi wao katika nyumba za kustaafu. Nakumbuka wakati mmoja, katika Jimbo moja nilikwenda kwenye nyumba ya watu waliostaafu kuwatembelea. Na kulikuwa na mwanamke ambaye alikuwa na watoto watatu, au wanne. Niliuliza: “Na watoto wako wakoje?”, "Nina wajukuu wengi” – “Na wanakuja kumtembelea?” "Ndiyo, wanakuja kila wakati." Nilipoondoka muuguzi aliniambia: "Wanakuja mara moja kwa mwaka." Lakini mama alifunika kasoro za watoto wake. Wengi huwaacha wazee peke yao. Wanatuma salamu za Noeli au Pasaka kwenye simu! Watunzeni wazee, ambao ni hekima ya watu! Tuwafikiri vijana wanaojiandaa kwa Ubatizo na sakramenti nyingine.
Katika Corsica, Papa amesema asante Mungu, ni wengi! KAliongeza kusea: “Na pongezi! Sijawahi kuona watoto wengi kama hapa! Ni neema kutoka kwa Mungu! Na niliona mbwa wawili tu. Ndugu wapendwa, mzae watoto, mpate watoto ambao watakuwa furaha yenu, faraja yenu katika siku zijazo. Huu ndio ukweli: Sijawahi kuona watoto wengi hivyo. Ni katika Timor-ya Mashariki kulikuwa na watu wengi kama hawa, lakini katika miji mingine sio wengi sana. Hii ni furaha yenu na utukufu wenu,” Papa aliwapongeza. “Amewaomba waendelee nan jia hiyo: Kanisa huzaa matunda linapokuwa na furaha. Furaha ni "mtindo" wa tangazo letu, ambalo huleta amani ya Bwana na nuru ya imani kwa wote.” Papa Francisko kwa masikitiko alisema “kwa bahati mbaya tunajua vizuri kwamba hakuna uhaba wa sababu kubwa za maumivu kati ya mataifa: umaskini, vita, ufisadi na , vurugu. Ninawambia jambo moja: wakati mwingine watoto wa Kiukreni wanakuja kwenye vikao, ambao waliletwa hapa kutokana na vita. Mnajua nini? Hawa watoto hawatabasamu! Walisahau tabasamu. Tafadhali, tuwafikirie watoto hawa katika nchi za vita, uchungu wa watoto wengi.
Hata hivyo, Neno la Mungu hututia moyo sikuzote. Na katika uso wa uharibifu unaowakandamiza watu, Kanisa linatangaza tumaini fulani, ambalo halikatishi tamaa, kwa sababu Bwana anakuja kuishi kati yetu. Na kisha kujitolea kwetu kwa amani na haki kunapata katika ujio wake nguvu isiyoisha. Papa alisema kuwa katika kila wakati na katika kila dhiki, Kristo yupo, Kristo ndiye chanzo cha furaha yetu. Yuko pamoja nasi katika dhiki kutupeleka mbele na kutupa furaha. Daima tuitunze furaha hii mioyoni mwetu, uhakika huu kwamba Kristo yu pamoja nasi, anatembea nasi. Tusiisahau! Na hivyo kwa furaha hii, kwa uhakika huu kwamba Yesu yu pamoja nasi, tutafurahi na kuwafurahisha wengine. Huu ndiyo lazima uwe ushuhuda wetu. Alihitimisha.