Papa Francisko,Ajaccio:kujijali kiroho,wengine&kutumaini na furaha!
Na Angella Rwezaula – Vatican
Baba Mtakatifu Francisko katika hotuba yake ikiwa ya pili kati ya tatu zilizopagwa kwenye Ziara yake ya kitume ya 47 huko Ajaccio, Corsica nchini Ufaransa, na mara baada ya kutoa hotuba katika Hitimisho la Kongamano kuhusu “Udini Maarufu wa Watu wa Mungu, alisema: “Ndugu Maaskofu, wapendwa mapadre na mashemasi, watawa na waseminari. Niko hapa katika nchi yenu hii nzuri kwa siku moja tu, lakini nilitaka kukutana nanyi na kutumia angalau muda mfupi pamoja. Hii inanipa nafasi, kwanza kabisa, kusema asante. Asante kwa kuwa hapa, na zawadi ya maisha yenu. Asante kwa kazi yenu na juhudi zenu za kila siku. Asante kwa sababu ninyi ni ishara ya upendo wa huruma wa Mungu na mashuhuda wa Injili.
Kwa njia hiyo Baba Mtakatifu akiwa mbele ya maaskofu, mapadre, watawa wa kike na kiume wasiminari na wahudumu wa kanisa Katika Kanisa Kuu, la Bikira Maria Mpalizwa, aliendelea na hotuba yake kwamba kwa kitaaliano kusema asante, inamfanya mara moja kufikiria neema ya Mungu, ambayo ni msingi wa imani ya Kikristo na kila aina ya wakfu katika Kanisa. Katika muktadha wetu wa Ulaya, hatukabiliani na ukosefu wa matatizo na changamoto katika kupitisha imani. Kila siku tunapata uzoefu huu, na tunaweza kuhisi kutokuwa na msaada na kutostahili. Papa alieleza jinsi ambavyo wao ni wachache kwa idadi, hawana rasilimali nyingi, si mara zote wanafanya kazi katika mazingira ambayo yapo wazi kupokea ujumbe wa Injili. Hata hivyo umaskini huu wenyewe ni baraka! “Unatuondolea kisingizio cha kwamba tunafaulu kwa juhudi zetu wenyewe, na Unatufundisha kuuona utume wa Kikristo kuwa hautegemei uwezo wa kibinadamu bali zaidi ya yote kwa Bwana ambaye daima hufanya kazi kwa kidogo tuwezacho kumtolea.”
Tusisahau kamwe kwamba ni juu ya Bwana. Sio juu yetu, lakini juu ya Mungu. Labda hili ni jambo ambalo kila asubuhi, wakati wanajua, kila kuhani na kila mtu aliyewekwa wakfu anapaswa kurudia katika sala. Kwamba “Leo, vile vile, huduma yangu hainihusu mimi, bali ni ya Mungu.” Ukuu wa neema ya Mungu haimaanishi, hata hivyo, kwamba tunaweza kupumzika bila kuchukua majukumu yetu. Kinyume chake, “tunapaswa kujifikiria sisi wenyewe kama watenda kazi pamoja na neema ya Mungu (rej. 1 Kor 3:9). Tunapotembea na Bwana, tunapaswa kuendelea kufikiria kuhusu swali moja muhimu: Je, ninaishi vipi ukuhani wangu, kujiweka wakfu kwangu, maisha yangu kama mfuasi? Swali hili ni muhimu. Papa Francisko amewasihi waliweke akilini na wasidharau hitaji la utambuzi huu, huku wakitazama ndani yao ili wasije kuingia katika hali ya kila siku na kasi ya maisha na shughuli zao hata wakapoteza usawa wa maisha ndani ya kiroho.
Kwa upande wa Papa alipenda kuwapa mwaliko mara mbili ule wa kujijali na kuwajali wengine. Akifafanua mwaliko wa kwanza kuhusu kujijali, Papa alisema maisha ya kikuhani au ya kidini sio tu ya kusema "ndiyo" ambayo tunasema mara moja na kwa maisha yote. Hakuna kuishi mbali na Bwana! Kinyume chake, kila siku lazima tufanye upya furaha ya kukutana naye; kila wakati tunahitaji kusikiliza sauti yake upya na kuamua kwa mara nyingine kumfuata. Papa alisisitiza kumbuka hilo kwamba: maisha yetu yanaoneshwa katika zawadi yetu ya binafsi, lakini kadiri makuhani au waliowekwa wakfu wanavyojituma mara nyingi zaidi katika utumishi wa Ufalme wa Mungu, na ndivyo wanavyohitaji kujijali zaidi. Mapadre, masista au mashemasi wanaojisahau pia wataishia kuwapuuza watu waliokabidhiwa uangalizi wao.
Papa alisema ndiyo maana inachukua kanuni ya maisha kidogo - ambayo watawa tayari wanayo! hiyo inajumuisha muda uliotengwa kila siku kwa sala na Ekaristi na kwa mazungumzo na Bwana, kila mmoja kulingana na hali yake ya kiroho na mtindo wake. Papa alipenda tena kusema kwamba wanapaswa kutenga baadhi ya nyakati za upweke, wawe kaka au dada ambayo wanaweza kushiriki pamoja nao kwa uhuru kile kilicho moyoni mwao; ili wasitawishe shauku, si kama njia ya kujaza wakati wao wa ziada, lakini kama njia ya kupumzika afya kutokana mizigo ya huduma. Papa amekazia kusema kuwa “Tunapaswa kuwa na wasiwasi juu ya wale watu ambao wako safarini kila wakati, kila wakati katikati ya usikivu, na labda kwa bidii kupita kiasi kamwe hawatulii, hawachukui muda wao wenyewe. Hiyo si nzuri. Kuna haja ya kuwa na mahali pa kwenda na nyakati zilizowekwa kando ambapo kila padre na kila mtawa anaweza kujisimamia.
Jambo lingine ni sehemu ya utunzaji huu ambao ni wa udugu kati yao. Tunapaswa kujifunza kushiriki sio tu shida na changamoto zetu, lakini pia furaha zetu na urafiki wetu kati yetu wenyewe. Papa alikumbusha kwamba Askofu wao alisema jambo ambalo alilipenda, yaani, kwamba ni muhimu kuhama kutoka katika “Kitabu cha Maombolezo” hadi “Kitabu cha Wimbo ulio Bora”. Na hii ni muhimu. Zaburi moja inasema hivi: "Umegeuza maombolezo yangu kuwa ya furaha" (30:11). Hebu tushiriki furaha yetu ya kuwa mitume na wanafunzi wa Bwana!
Pili: Papa Francisko ameeleza njia ya kuwajali wengine. Utume ambao kila mmoja wao amepokea una lengo moja tu: kumpeleka Kristo kwa wengine, kupeleka faraja ya Injili mioyoni mwa kaka na dada zetu. Hapo Papa alipenda kukumbusha wakati mtume Paulo alipokuwa karibu kurudi Korintho. Akiiandikia jumuiya ya huko, alisema: “Nitatumia kwa furaha nyingi na kutumiwa kwa ajili yenu” (2 Wakor 12:15). Tunajitoa kwa ajili ya nafsi zetu, tukitumika katika kujitolea kuwatumikia wale waliokabidhiwa kwetu. Hao kaka na dada ndio kiini cha ufikiaji wao wa huduma: ustawi wao wa kiroho, hitaji lao la tumaini, hamu yao ya kusikilizwa na kuhisi ukaribu wa wengine. Na huo ndiyo mwaliko kwetu kugundua, katika muktadha wa leo hii, njia za kichungaji zenye ufanisi zaidi za uinjilishaji. Wasiogope kubadilika, kutathmini upya mbinu za zamani, kufanya upya lugha ya imani na kutambua kwamba utume si suala la mikakati ya kibinadamu, lakini zaidi ya yote ni suala la imani, shauku kwa Injili na Ufalme wa Mungu.
Kuwajali wengine: wale wanaofuata mafundisho ya Yesu, wale ambao wamepotea kutoka kwake, wale wanaohitaji kurudishwa kwenye njia sahihi au kupata faraja katikati ya mateso yao. Jali kila mtu, katika malezi na zaidi ya yote katika kukutana. Kutana na watu wanakoishi na kufanya kazi, katika kila hali. Papa Francisko amewashukuru kwa moyo wote na ameoomba kwamba huduma yao iwe yenye tumaini na furaha. Hata wakati wa uchovu au kukata tamaa, wasikate tamaa. wampe Bwana moyo wao. Yeye atafanya uwepo wake uhisiwe ikiwa wanajijali wao na wengine. Maana ndivyo anavyowajaza faraja wale aliowaita na kuwatuma. Wasonga mbele kwa ujasiri; na atawajaza furaha.
Kwa kuhitimisha, Papa Francisko alisema na “Sasa tugeukie Bikira Maria kwa maombi. Katika Kanisa Kuu hili lililopewa jina la Mama Yetu wa Kupalizwa, wamini wanaomba upendeleo wake chini ya jina la Mama wa Huduma , "Madunnuccia". Kutoka katika kisiwa hiki cha Mediterania, tumwinulie ombi letu la amani: amani kwa nchi zote zinazozunguka bahari hii, hasa Nchi Takatifu ambako Maria alimzaa Yesu. Amani kwa Palestina, kwa Israeli, kwa Lebanon, kwa Siria, na kwa Mashariki ya Kati yote! Na Mama Mtakatifu wa Mungu atupatie amani inayotamaniwa sana na watu wa Kiukreni na Kirusi. Vita daima ni kushindwa. Amani kwa dunia nzima!