Tafuta

Papa Francisko:Katika maisha yote ya Yesu tunaona chaguo la Mungu la udogo na fumbo!

Mwaka mpya unaofunguliwa,tuukabidhi kwa Maria,Mama wa Mungu,ili tujifunze kama yeye kuupata ukuu wa Mungu katika udogo wa maisha;tujifunze kutunza kila kiumbe kilichozaliwa na mwanamke:maisha katika tumbo la uzazi,watoto,wanaoteseka,maskini,wazee,wapweke na wanaokufa.Leo ni Siku ya Amani Duniani,tunaalikwa kuchukua mwaliko huu unaobubujika kutoka katika moyo wa Mama Maria kulinda,kurejesha utu wa maisha.Ni katika mahubiri ya Papa tarehe 1 Januari 2024.

Na Angella Rwezaula – Vatican.

Mwanzoni mwa mwaka mpya ambao Bwana anatujalia maishani mwetu, ni vizuri kuweza kuinua mtazamo wa  mioyo yetu kwa Maria. Kwa hakika, akiwa Mama, anatuelekeza kwenye uhusiano na Mwana: anaturudisha kwa Yesu, anazungumza nasi kuhusu Yesu, anatuongoza kwa Yesu. Hivyo, Sherehe ya Maria Mtakatifu Mama wa Mungu inatuzamisha tena katika Fumbo la Noeli: Mungu alifanyika  mwili kuwa mmoja wetu katika tumbo la uzazi la Maria na sisi tuliofungua Mlango Mtakatifu wa kuanza Jubilei, tunakumbushwa leo kwamba “Basi Maria ndiye mlango ambao Kristo aliingia katika ulimwengu huu.” Ndivyo Baba Mtakatifu Francisko alianza mahubiri yake  wakati Mama Kanisa anaadhimisha Siku Kuu ya Maria Mama wa Mungu, sambamba na Siku ya 58 ya Amani Ulimwenguni, tarehe 1 Januari 2025. Kanisa kuu la Mtakatifu Petro likiwa limejaa waamini kutoka sehemu mbali mbali, Baba Mtakatifu aliendelea kusema kuwa Mtume Paulo anatoa muhtasari wa fumbo hili kwa kusema kwamba “Mungu alimtuma Mwanawe ambaye amezaliwa na mwanamke” (Gal 4:4). Maneno haya- "aliyezaliwa na mwanamke" - yanasikika mioyoni mwetu leo ​​hii na kutukumbusha kwamba Yesu, Mwokozi wetu, alifanyika mwili na kujidhihirisha katika udhaifu wa mwili.

Papa Francisko katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro
Papa Francisko katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro

Kuzaliwa na mwanamke. Papa amesema “Usemi huu kwanza kabisa unaturudisha kwenye Noeli. Neno alifanyika mwili. Mtume Paulo anabainisha kwamba alizaliwa na mwanamke, karibu kutaka kuhisi haja ya kutukumbusha kwamba Mungu kweli alifanyika mwanadamu kupitia tumbo la uzazi wa mwanadamu. Kuna majaribu, ambayo yanawavutia watu wengi leo hii, lakini ambayo yanaweza pia kuwashawishi Wakristo wengi: kufikiria au kutengeneza Mungu "wa kufikirika,", aliyeunganishwa na wazo lisilo wazi la kidini, kwa hisia fulani nzuri zinazopita. Badala yake, yeye ni halisi, ni mwanadamu: alizaliwa na mwanamke, ana uso na jina, na anatuita tuwe na uhusiano naye.  Kristo Yesu, Mwokozi wetu, alizaliwa na mwanamke; ana nyama na damu; anatoka katika kifua cha Baba, lakini alifanyika mwili ndani ya tumbo la Bikira Maria; hutoka juu mbinguni lakini hukaa katika vilindi vya nchi; yeye ni Mwana wa Mungu, lakini alifanyika Mwana wa Adamu. Yeye, sura ya Mwenyezi Mungu, alikuja katika udhaifu; na ingawa hakuwa na dhambi, “Mungu alimfanya kuwa mdhambi kwa ajili yetu” (2Kor 5:21). Alizaliwa na mwanamke na ni mmoja wetu. Hasa kwa sababu hii anaweza kutuokoa.

Papa Francisko
Papa Francisko

Baba Mtakatifu ameendelea kuseleza juu ya 'Kuzaliwa na mwanamke.' Usemi huu pia unazungumza nasi kuhusu ubinadamu wa Kristo, kutuambia kwamba anajidhihirisha katika udhaifu wa mwili. Ikiwa alishuka kwenye tumbo la uzazi la mwanamke, akizaliwa kama viumbe vyote, hapa anajionesha katika udhaifu wa Mtoto. Hii ndiyo sababu wachungaji, wakienda kuona kwa macho yao yale ambayo Malaika aliwatangazia, hawakupata ishara za ajabu au maonesho makubwa, lakini "waliwakuta Maria na Yosefu na mtoto amelala horini"(Lk 2:16). Walimkuta mtoto mchanga asiye na msaada, dhaifu, anayehitaji utunzaji wa mama yake, akihitaji nguo za kitoto na maziwa, anayehitaji kubembelezwa na kupendwa. Mtakatifu Louis Marie Grignion wa Montfort anasema kwamba Hekima ya kimungu "haikutaka, ingawa ingeweza kufanya hivyo, kujitoa moja kwa moja kwa wanadamu, lakini ilipendelea kujitoa kupitia kwa Bikira Mtakatifu. Wala hakutaka kuja ulimwenguni katika umri wa mtu mkamilifu, asiyetegemea wengine, lakini kama mtoto maskini na mdogo, anayehitaji utunzaji na riziki ya Mama yake" ( Mkataba juu ya ibada ya kweli kwa Bikira Mtakatifu, 139).

Na kwa hivyo katika maisha yote ya Yesu tunaweza kuona chaguo hili la Mungu, chaguo la udogo na fumbo;Hatakubali kamwe kushawishiwa na uzuri wa uweza wa kimungu kufanya ishara kubwa na kujilazimisha juu ya wengine kama shetani alivyopendekeza kwake, lakini atafunua upendo wa Mungu katika uzuri wa ubinadamu wake, akiishi kati yetu, akishiriki mambo ya kawaida, maisha yaliyoundwa na taabu na ndoto, kuonesha huruma kwa mateso ya mwili na roho, kufungua macho ya vipofu na kuimarisha waliopotea. "Huruma. Papa Francisko kama kawaida yake amesisitiza tena kuwa “ Tabia tatu za Mungu ni: huruma, ukaribu na upole. Mungu anakuwa karibu na mwenye huruma na Upole. Tusisahau hili." Yesu anatuonesha Mungu kupitia ubinadamu wake dhaifu, anayewajali walio dhaifu.

Wakati wa misa tarehe 1 Januari 2025
Wakati wa misa tarehe 1 Januari 2025

Baba Mtakatifu amesisitiza kuwa ni jambo la kupendeza kufikiri kwamba Maria, msichana wa Nazareti, daima anatuongoza nyuma kwenye Fumbo la Mwana wake, Yesu, anatukumbusha kwamba Yesu anakuja katika mwili na, kwa hiyo, mahali pa pekee ambapo tunaweza kukutana yeye ndiye wa kwanza kabisa maisha yetu, ubinadamu wetu dhaifu, wa wale wanaopita karibu nasi kila siku.  Na kwa kumwita kama Mama wa Mungu, tunathibitisha kwamba Kristo alizaliwa na Baba, lakini alizaliwa kweli kutoka katika tumbo la mwanamke. Tunathibitisha kuwa Yeye ni Mungu; yeye ni Bwana wa wakati lakini anakaa wakati wetu huu, hata mwaka huu mpya, pamoja na uwepo wake wa upendo. Tunathibitisha kwamba Yeye ni Mwokozi wa ulimwengu, lakini tunaweza kukutana Naye na lazima tumtafute katika uso wa kila mwanadamu.

Na ikiwa Yeye, ambaye ni Mwana, alikua mdogo kushikwa mikononi mwa mama, kutunzwa na kunyonyeshwa, basi ina maana kwamba hata leo anakuja kwa wale wote wanaohitaji uangalizi sawa: kwa kila dada na kaka tunayekutana naye na ambaye anahitaji umakini, kusikiliza, na  huruma. Mwaka huu mpya unaofunguliwa, tuukabidhi kwa Maria, Mama wa Mungu, ili nasi tujifunze kama yeye kuupata ukuu wa Mungu katika udogo wa maisha; kwa sababu tunajifunza kutunza kila kiumbe kilichozaliwa na mwanamke, kwanza kabisa kwa kulinda zawadi ya uzima yenye thamani, kama vile Maria afanyavyo: maisha katika tumbo la uzazi, ya watoto, ya wale wanaoteseka, maisha ya maskini, maisha ya wazee, ya wale walio peke yao, ya wale wanaokufa.

Misa tarehe 1 Januari 2025
Misa tarehe 1 Januari 2025

Na leo hii, katika Siku ya Amani Duniani, Papa amesisitiza kuwa "tunaalikwa sote kuchukua mwaliko huu unaobubujika kutoka kwa moyo wa mama Maria: tunaalikwa kulinda maisha, kutunza maisha ya majeruhi - maisha yaliyojeruhiwa sana, kurejesha utu wa maisha ya kila "aliyezaliwa na mwanamke" ni msingi wa wa kujenga ustaarabu wa amani. Kwa sababu hiyo, "Ninaomba dhamira thabiti ya kukuza heshima ya utu wa maisha ya mwanadamu, tangu kutungwa mimba hadi kifo cha asili, ili kila mtu apende maisha yake na kutazama siku zijazo kwa matumaini" (Ujumbe kwa Siku ya Dunia ya LVIII ya Amani, 1 ° Januari 2025). "Historia inatuambia kwamba huko Efeso, wakati maaskofu waliingia kanisani, waamini, wakiwa na fimbo mikononi, walipiga kelele wakisema: "Mama wa Mungu!" Na kwa hakika vijiti vilikuwa ni ahadi ya kile ambacho kingetokea ikiwa hawangetangaza utambulisho wa “Mama wa Mungu.” Kwa njia hiyo Papa ameongeza kusema "Leo hii hatuna vijiti, lakini ndiyo, moyo wa mwana, na sauti.  Kwa sababu hiyo, sote kwa pamoja, tumsifu Mama Mtakatifu wa Mungu kwa pamoja: "Mama Mtakatifu wa Mungu", mara tatu:  "Mama Mtakatifu wa Mungu, Mama Mtakatifu wa Mungu, Mama Mtakatifu wa Mungu." Papa Francisko alihitimisha mahubiri yake.

01 January 2025, 11:30