Kumbukizi ya Miaka 12 Ya Uongozi wa Papa Francisko: Ibada ya Misa Kwa Wanadiplomasia
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Ilikuwa ni tarehe 13 Machi 2013, Baraza la Makardinali lilipomchagua Kardinali Jorge Mario Bergoglio kuwa Khalifa wa Matakatifu Petro na katika maadhimisho ya Sherehe ya Mtakatifu Yosefu, Mume wake Bikira Maria, tarehe 19 Machi 2013, Baba Mtakatifu akasimikwa rasmi na kuwa ni Khalifa wa Mtakatifu Petro wa 266 kwa kuchagua jina la Mtakatifu Francisko wa Assisi. Baba Mtakatifu ameadhimisha kumbukumbu hii akiwa bado amelazwa kwenye Hospitali ya Chuo Kikuu cha Agostino Gemelli iliyoko mjini Roma tangu Ijumaa tarehe 14 Februari 2025; kwa hakika Baba Mtakatifu anasema: anaonja: umakini wa huduma na huruma kutoka kwa madaktari na wafanyakazi katika sekta ya afya. Baba Mtakatifu anawashukuru kutoka katika sakafu ya moyo wake wote na anawakumbuka wote wanaowahudumia wagonjwa sehemu mbalimbali za dunia, kama ishara ya uwepo na ukaribu wa Mungu kwa waja wake na kwamba, binadamu katika udhaifu wake anahitaji kuonjeshwa “Muujiza wa huruma ya Mungu” unaowaambata na kuwasindikiza wale wote walioko kwenye majaribu na kuwakirimia mwanga mdogo katika usiku mnene wa maumivu.
Baba Mtakatifu anawashukuru kwa dhati kabisa waamini na watu wote wenye mapenzi mema, wanaoendelea kumwonesha uwepo wao wa karibu kwa njia ya Sala na Sadaka zao na kwamba, yeye pia anawakumbuka na kuwaombea. Hali ya afya ya Baba Mtakatifu inaendelea kuimarika zaidi na zaidi. Anaendelea kupata tiba, kusali, kutafakari na kufanya mazoezi ya viungo pamoja na mapumziko. Madaktari wanasema, Baba Mtakatifu bado anahitaji muda mrefu wa matibabu na mapumziko. Takwimu zinaonesha kwamba, Vatican ina uhusiano wa kidiplomasia na nchi 184 duniani. Mabalozi wakazi wanaoishi mjini Roma kwa sasa ni 89, wengine, ni mabalozi wanaowakilisha nchi zao wakiwa wanatoka nje ya Roma. Kuna Mashirika ya Kimataifa kama vile, Shirikisho la Nchi za Kiarabu pamoja na Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa, UNHCR.
Ni katika muktadha huu, Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican, Ijumaa tarehe 14 Machi 2025, ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kama sehemu ya kumbukizi ya Miaka 12 tangu Baba Mtakatifu Francisko alipochaguliwa kuliongoza Kanisa Katoliki. Ibada hii imehudhuriwa na wanadiplomasia pamoja na wawakilishi wa mashirika ya Kimataifa yaliyoko mjini Vatican. Kardinali Parolin katika mahubiri yake, amekazia umuhimu wa waamini kumtolea Mwenyezi Mungu, nyoyo zao katika ukweli na uwazi, tayari kusikiliza Neno lake. Huu ni mwaliko wa kutenda katika kweli na haki, daima wakijitahidi kutafuta na kutekeleza mapenzi ya Mungu katika maisha yao sanjari na kujenga mahusiano na mafungamano mema na jirani zao yanayosimikwa katika Injili ya upendo. Waamini wajenge utamaduni wa kumpenda Mwenyezi Mungu kwa kuonesha kwanza upendo kwa jirani zao. Mwenyezi Mungu anaangalia undani wa maisha ya mwanadamu, hivyo hii ni changamoto kwa waamini kuhakikisha kwamba, wanafikiri na kutenda kadiri ya tunu msingi za Kiinjili, ili wasiwe ni chanzo cha vita, kinzani, migogoro na mipasuko ya kijamii.
Kardinali Parolin anasema, Diplomasia ya Vatican inatoa kipaumbele cha pekee kwa uhuru wa kidini, utu na heshima ya binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu, bila kusahau utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Kumbe kuna haja ya kutambua na kuheshimu haki msingi za binadamu kwani hii ni hatua muhimu sana ya maendeleo fungamani kwa sababu mizizi ya haki za binadamu inafumbatwa katika hadhi, heshima na utu wa binadamu. Huu pia ni mwaliko kwa watu wote wa Mungu kuondokana na: Uchu wa mali na madaraka; chuki, hasira, uchoyo na ubinafsi, mambo ambayo ni chanzo cha vita, migogoro na mipasuko ya kijamii. Waamini na watu wote wenye mapenzi mema, wanahimizwa kusimika mahusiano na mafungamano yao ya kijamii katika Injili ya upendo, upatanisho, haki na msamaha wa kweli.
Kardinali Parolin anakiri kwamba, si rahisi sana kuomba wala kutoa msamaha wa kweli, lakini hii ndiyo changamoto kubwa inayotolewa na Kristo Yesu katika Injili. Familia ya binadamu iwe ni kitovu cha msamaha wa kweli, kwa kutambua kwamba, kukosa na kukoseana ni sehemu ya udhaifu wa kibinadamu, kutubu, kusamehe na kupatana ni mwanzo wa mchakato wa utakatifu wa maisha. Wanafamilia wajifunze kusema: Naomba, Asante na Samahani; maneno yanayoweza kuisaidia familia kuishi kwa amani na utulivu kama anavyokazia Baba Mtakatifu Francisko kuhusu wito wa familia, maisha ya ndoa na familia. Kardinali Parolin anakaza kusema, watu wa Mungu peke yao hawawezi kutekeleza mchakato huu wa upatanisho na msamaha wa kweli, kumbe, wanapaswa kuomba neema na baraka kutoka kwa Mungu pamoja na kuendelea kujitahidi kumwilisha Neno lake katika uhalisia wa maisha na hivyo kuwa ni mashuhuda na vyombo vya Injili ya upendo na upatanisho. Sala inapewa uzito wa pekee wakati huu, Baba Mtakatifu Francisko anapokabiliana na changamoto ya afya. Watu wa Mungu wanamwombea ili aweze kupona haraka na hatimaye, kurejea tena mjini Vatican ili kuendelea na maisha na utume wake.