Makanisa Yasali Kumwombea Papa Francisko Miaka 12 ya Utume Wake
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Itakumbukwa kwamba, Maadhimisho ya Mwaka wa Mtakatifu Yosefu yalizinduliwa rasmi na Baba Mtakatifu Francisko hapo tarehe 8 Desemba 2020 na kufungwa rasmi tarehe 8 Desemba 2021. Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa Kitume “Patris Corde” yaani “Kwa Moyo wa Kibaba”: “Mwaka wa Mtakatifu Yosefu, Kumbukumbu ya Miaka 150 Tangu Mtakatifu Yosefu alipotangazwa Kuwa Msimamizi wa Kanisa la kiulimwengu” na Papa Pio IX alitaja sifa kuu za Mtakatifu Yosefu akisema kwamba ni: “Baba mpendevu, mwenye huruma na mapendo; mtiifu na mwepesi kukubali. Ni Baba aliyebahatika kuwa na kipaji cha ubunifu na ujasiri, lakini alibaki akiwa amefichwa kwenye vivuli, akawajibika na kuwa ni chanzo cha furaha na sadaka binafsi. Katika moyo wa unyenyekevu, Mtakatifu Yosefu aliyahifadhi mafumbo yote ya maisha yaliyomzunguka Mtoto Yesu na Mama yake Bikira Maria. Mtakatifu Yosefu mtu wa busara na haki, alijiaminisha mbele ya Mwenyezi Mungu na kuyatekeleza yale yote aliyoambiwa na Malaika wa Bwana. Ni katika maadhimisho ya Sherehe ya Mtakatifu Yosefu, Mume wake Bikira Maria, tarehe 19 Machi 2013, Baba Mtakatifu aliposimikwa rasmi kuwa Khalifa wa Mtakatifu Petro wa 266 kwa kuchagua jina la Mtakatifu Francisko wa Assisi. Vipaumbele vyake tangu wakati huo ni: Maskini, Amani, Mazingira na sasa ni ujenzi wa udugu wa kibinadamu unaofumbatwa katika diplomasia ya huruma na upendo wa Mungu usiokuwa na mipaka kwa waja wake wote sanjari na ujenzi wa Kanisa la Kisinodi na Kimisionari. Ni katika kumbukizi ya miaka kumi na miwili tangu Baba Mtakatifu Francisko asimikwe kuwa ni Khalifa wa Mtakatifu Petro, akiwa kitandani amelazwa kwenye Hospitali ya Chuo Kikuu cha Agostino Gemelli iliyoko mjini Roma tangu Ijumaa tarehe 14 Februari 2025; ambako kwa hakika alionja: umakini wa huduma na huruma kutoka kwa madaktari na wafanyakazi katika sekta ya afya, Patriaki Bartolomeo wa kwanza wa Kanisa la Kiorthodox la Costantinopoli aliungana na watu wa Mungu kutoka Uturuki kusali kwa ajili ya kumwombea afya njema na uponaji wa haraka Baba Mtakatifu Francisko. Ibada hii ya kiekumene ilihudhuriwa pia na Askofu mkuu Marek Solczyński, Balozi wa Vatican nchini Uturuki.
Patriaki Bartolomeo wa kwanza anasema, Baba Mtakatifu anawahamasisha wakristo kumwilisha mchakato wa majadiliano ya kiekumene katika uhalisia wa maisha kama ndugu. Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kujipambanua katika mchakato wa ujenzi wa umoja wa Kanisa katika upendo, dhamana iliyoanzishwa na Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican, takribani miaka 50 iliyopita, baraka ambayo kwa wakati huu imewekwa chini ya ulinzi na tunza ya Mtakatifu Petro, Mtume. Huu ni mwaliko kutoka kwa Mtume Petro anayewataka watoto wa Mungu kuishi katika upendo, unyoofu; kwa kujitakasa roho zao, ili kutii kweli, ili hatimaye kufikia upendo wa kidugu usiokuwa na unafiki! Mwaliko kwa Wakristo ni kupendana kwa dhati kabisa. Baba Mtakatifu Francisko kunako mwaka 2014 alifanya hija ya kitume katika Nchi Takatifu kama kumbu kumbu ya Jubilee ya miaka 50 tangu Mtakatifu Paulo VI alipokutana na kusali pamoja na Patriaki Anathegoras wa Yerusalemu. Tangu wakati huo majadiliano ya kiekumene yameendelea kushika kasi, ili kuvuka kipeo cha kashfa ya utengano kati ya Makanisa, ili hatimaye, katika umoja, upendo na mshikamano Wakristo waweze kutoa ushuhuda wa Injili unaobubujika kutoka katika umoja wa Fumbo la Mwili wa Kristo, yaani Kanisa. Kanisa Katoliki linaendelea kujipambanua kama chombo cha kuhamasisha umoja wa Wakristo. Kwa upande wake, Kanisa la Kiorthodox linaendelea kujiimarisha katika uekumene wa udugu miongoni mwa Wakristo. Mchakato wa majadiliano ya kiekumene anasema Patriaki Bartolomeo wa kwanza unafumbatwa katika: upendo, ukweli na unabii, hatua ambayo kwa sasa ndiyo inayovaliwa njuga na viongozi wa Makanisa.
Makanisa na Madhehebu mbalimbali ya Kikristo yanajiandaa kuadhimisha Jubilei ya Miaka 1, 700 tangu Mtaguso wa Kwanza Nicea ulipoadhimishwa kunako mwaka 325 na kilele cha maadhimisho haya ni mwaka 2025, tukio la pekee na muhimu sana. Mwaka 2025 wakristo wote wanaadhimisha Pasaka ya Bwana siku moja, matendo makuu ya Mungu kwa waja wake. Kanuni ya Imani ya Nicea-Constantinopoli ni formula rasmi ambayo ilipitishwa na Mababa wa Mtaguso wa Kwanza wa Nicea (325) ikakamilishwa na Mtaguso wa kwanza wa Konstantinopoli (381) ili kubainisha imani sahihi ya Kanisa Katoliki dhidi ya uzushi, hasa wa Ario na wafuasi wake. Katika mazingira hayo, lengo kuu lilikuwa kwanza kabisa ni kumkiri Kristo Yesu “Mungu kweli kwa Mungu kweli” yaani Mungu kweli sawa na Baba, halafu kwamba: Roho Mtakatifu anastahili kuabudiwa pamoja na Baba na Mwana (Utatu Mtakatifu). Wakristo wanataka kutembea pamoja na Kristo Yesu ambaye ni njia, ukweli na uzima. Watu wanamtafuta Kristo Yesu hata bila ya kutambua. Patriaki Bartolomeo wa kwanza anamwomba Mwenyezi Mungu ili awakirimie waja wake afya na nguvu, ili kwa pamoja waweze kuadhimisha Jubilei ya Miaka 1, 700 ya Mtaguso wa kwanza wa Nicea.
Askofu Massimiliano Palinuro, Msimamizi wa Kitume wa Jimbo la Istanbul nchini Uturuki, katika mahubiri yake alisema, leo hii amani na usalama wa Jumuiya ya Kimataifa unatishiwa na uwepo wa vita, kinzani na migogoro mikubwa; ongezeko kubwa la maskini na “akina yakhe pangu pakavu tia mchuzi,” uchafuzi wa mazingira, walimwengu bado wanahitaji sauti ya Baba Mtakatifu Francisko, ili kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha utu, heshima, haki msingi sanjari na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Katika kipindi cha miaka kumi na miwili ya maisha na utume wake, Baba Mtakatifu Francisko amelialika Kanisa kurejea katika tunu msingi za Kiinjili na kwamba, Baba Mtakatifu Francisko ana ibada ya pekee kwa Mtakatifu Yosefu. Kama sehemu ya maadhimisho ya Mwaka wa Mtakatifu Yosefu, Baba Mtakatifu Francisko alianzisha mzunguko wa Katekesi Kuhusu Mtakatifu Yosefu ambaye kimsingi ni msaada, faraja na msimamizi. Kwa njia ya maisha na ushuhuda wake amekuwa ni msaada mkubwa kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema. Baba Mtakatifu aligusia kuhusu Mtakatifu Yosefu na mazingira alimoishi kadiri ya Maandiko Matakatifu; mjini Bethlehemu mahali alipozaliwa Kristo Yesu kama utimilifu wa Unabii. Nazareth ni mahali alipokulia Yesu. Hii ni miji miwili yenye uhusiano wa karibu sana na maisha ya Mtakatifu Yosefu.
Baba Mtakatifu Francisko alikaza kusema, Mwinjili Mathayo anawasaidia waamini kumwelewa Mtakatifu Yosefu, katika hali ya ukimya bila makuu, lakini, kiungo muhimu sana katika historia ya wokovu. Mtakatifu Yosefu ni mtu muhimu sana, lakini alijinyenyekesha na kamwe hakupenda kujipatia kipaumbele cha kwanza. Hii inaonesha kwamba, hata katika maisha ya kawaida, kuna watu muhimu, lakini mara nyingi husahauliwa na kamwe hawapewi kipaumbele na vichwa vya habari kwenye vyombo vya upashanaji habari. Hata leo hii ndani ya jamii, kuna watu wanashiriki kikamilifu katika malezi na makuzi ya watoto kwa njia ya mifano bora ya maisha! Hawa ni wale wanaowasaidia kukabiliana na changamoto za maisha kwa kuwajengea tabia njema pamoja na kuwafundisha namna ya kupambana na changamoto za maisha pamoja na kukuza ari na moyo wa sala. Kuna watu wengi wanaosali, wanaojisadaka na kujitosa kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.
Watu wengi wanaweza kujitambua ndani ya maisha na utume wa Mtakatifu Yosefu, aliyetekeleza dhamana na wajibu wake pasi na makuu, katika hali ya kificho, akawa mwombezi, msaada na kiongozi nyakati za shida na magumu ya maisha. Mtakatifu Yosefu anawakumbusha kwamba, wale wote wanaotekeleza nyajibu zao pasi na makuu wanaye mwenza katika historia ya wokovu. Ulimwengu unawahitaji watu kama hawa. Katika Injili kama ilivyoandikwa na Mtakatifu Luka, Mtakatifu Yosefu anaoneshwa kama mlinzi wa Yesu na Bikira Maria. Ni katika muktadha huu, Mtakatifu Yosefu ni Mlinzi na Msimamizi wa Kanisa la Kiulimwengu, kwa sababu Kanisa ni mwendelezo wa Fumbo la Mwili wa Kristo Yesu katika historia. Wakati huo huo katika tumbo la Mama Kanisa, limefunikwa na kivuli cha Bikira Maria. Mtakatifu Yosefu anaendelea na utume wake wa kumlinda Mtoto pamoja na Mama yake! Huu ni wajibu mzito wa Mtakatifu Yosefu wa kuendeleza ulinzi kwa ndugu na jirani kinyume kabisa na ilivyokuwa kwenye Agano la Kale. Jamii mamboleo inapata katika historia ya Mtakatifu Yosefu maelekezo ya umuhimu wa umoja na mafungamano ya udugu wa kibinadamu. Agano Jipya linasimulia kuhusu Ukoo wa Kristo Yesu si kwa sababu msingi za kitaalimungu, lakini pia ni kutaka kuonesha umoja na mshikamano wa udugu wa kibinadamu, unaotangulia na kuwasindikiza watu katika maisha yao. Kristo Yesu, Mwana wa Mungu, ili kuja ulimwenguni ameamua kufuata njia ya mafungamano ya kijamii. Hii ni changamoto pevu kwa watu wengi duniani kwa wale wanaojisikia kuwa wapweke, hawana nguvu wala ujasiri wa kusonga mbele na safari ya maisha.