Papa atoa shukurani kwa madaktari pia aomba silaha zinyamazishwe!
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Hali ngumu zaidi na yenye uchungu huhitaji saburi yenye kutumaini, iliyokita mzizi wake katika upendo wa Mungu. Katika tafakari ya Baba Mtakatifu Francisko iliyotayarishwa kwa ajili ya Sala ya Malaika wa Bwana ikiwa ni ya mwisho kabla ya kurudi kutoka hopitalini Gemelli, Roma, Dominika tarehe 23 Machi 2025, Papa ameonesha, umuhimu wa subira, yaani muhimu kwa maisha ya wanadamu. Subira ya Mungu, kama inavyooneshwa katika Injili ya siku ndiyo inayowachochea waamini kufanya maisha yao kuwa wakati wa kubadilika, wa uongofu kama mkulima anayengojea matunda ya mtini usiozaa. Bwan ni mkulima mvumilivu ambaye, hufanya udongo wa maisha ya watu kusubiri kwa ujasiri kurudi kwake.
Akianza kudadavua Injili hiyo ya siku kutoka Luka Lk. 13:1-9 Papa anabainisha kuwa Yesu anatumia picha ya mtini tasa, ambao hakutoa matunda yaliyotegemewa na mbao licha ya hayo mkulima hataki kuukata; anataka kuwekea mbolea ili kuona kama unaweza kutoa matunda kwa wakati ujao (Lk 13,9). Mkulima huyo mwenye subira ni Bwana, ambaye anafanya kazi kwa uangalizi mkuu wa shamba la maisha yetu na anasubiri kwa imani kurudi kwetu kwake!
Shukrani kwa madaktari
Katika kipindi hiki kirefu cha kulazwa hospitalini, nimepata fursa ya kujionea subira ya Bwana, ambayo pia naiona ikioneshwa katika utunzaji usiochoka wa madaktari na wahudumu wa afya, pamoja na usikivu na matumaini ya ndugu wa wagonjwa. Uvumilivu huu wa kutumainia, unaokitwa katika upendo usio na kikomo wa Mungu, ni muhimu sana katika maisha yetu, hasa kukabiliana na hali ngumu na chungu zaidi.
Hali mbaya Ukanda wa Gaza
Papa Francisko aidha amebainisha kuwa “Nilihuzunishwa na kuanza tena kwa mashambulizi makubwa ya mabomu ya Israeli kwenye Ukanda wa Gaza, na vifo vingi na majeruhi. Naomba silaha zinyamazishwe mara moja; na tuwe na ujasiri wa kuanza tena mazungumzo, ili mateka wote waachiliwe na kufikiwa kwa usitishaji vita wa uhakika. Hali ya kibinadamu katika Ukanda huo kwa mara nyingine tena ni mbaya sana na inahitaji hatua za haraka za pande zinazozozana na jumuiya ya kimataifa.
Mkataba wa amani kati ya Armenia na Azerbaijan
Papa Francisko kadhalika amesbainisha kuwa "Nimefurahiya kwamba Armenia na Azerbaijan zimekubaliana juu ya maandishi ya mwisho ya Mkataba wa Amani. Natumaini kwamba itatiwa saini upesi iwezekanavyo na hivyo kuchangia katika kuanzisha amani ya kudumu katika Caucasus Kusini."
Kwa uvumilivu na subira muendelee kuniombea
Papa kadhalika amesema kuwa "Kwa uvumilivu mwingi na subira mueendelea kuniombea: asante sana! Nawaombea ninyipia. Na kwa pamoja tuombe kukomeshwa kwa vita na amani, iwepo hasa katika Ukraine, Palestina, Israel, Lebanon, Myanmar, Sudan, na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo inayoteswa. Bikira Maria atulinde na aendelee kutusindikiza katika safari ya kuelekea Pasaka.