Adhabu ya Kifo Ni Ukatili wa Hali Ya Juu Dhidi Ya Utu, Heshima Na Haki Msingi za Binadamu
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Shirika la Kimataifa la Kutetea Haki za Binadamu la Amnesty International, linasema, kumekuwepo na ongezeko kubwa la idadi ya adhabu ya kifo, iliyotekelezwa katika nchi mbalimbali duniani, lakini zaidi huko Mashariki ya Kati hususan: Iran, Iraq na Saudi Arabia ambako kwa pamoja watu 1, 380 walinyongwa hadi kufa. Nchi nyingine zenye idadi kubwa ya watu walionyongwa ni pamoja na China, Korea ya Kusini na Korea ya Kaskazini pamoja na Vietnam ambako adhabu ya kifo bado inaendelea kutumika. Shirika la Kimataifa la Kutetea Haki za Binadamu la Amnesty International, halikuweza kupata kibali cha kuhakiki idadi ya watu walionyongwa hadi kufa nchini Palestina na Siria. Serikali ya DRC imetangaza nia ya kurejesha tena adhabu ya kifo, kama ilivyo pia nchini Burkina Faso. Nchi tano zinazoongoza kwa idadi kubwa ya watu walionyongwa hadi kufa ni: China, Iran, Saudi Arabia, Iraq na Yemen. Adhabu ya kifo imetolewa kwa watu waliokamatwa wakijihusisha na biashara na matumizi haramu ya dawa za kulevya pamoja na kisingizio cha usalama wa Taifa. Takwimu zinaonesha kwamba, nchini Marekani katika kipindi cha Mwaka 2024 watu 15 ndio walio hukumiwa adhabu ya kifo. Itakumbukwa kwamba, kuna nchi 113 ambazo zimefuta adhabu ya kifo na kwamba, kuna nchi 145 ambazo licha Sheria ya adhabu ya kifo kuwemo katika nchi hizi, lakini kwa muda mrefu sheria hii haijatumika. Zimbabwe imeacha alama ya kudumu kwa kufuta adhabu ya kifo katika Sheria zake. Shirika la Kimataifa la Kutetea Haki za Binadamu la Amnesty International, linasema, kuna uwezekano mkubwa wa kufuta adhabu ya kifo duniani, kama inavyojionesha kwenye Makao makuu ya Umoja wa Mataifa ambako wanachama wengi wametia nia ya kuhakikisha kwamba, adhabu ya kifo inafutwa kwenye uso wa dunia.
Mama Kanisa anasema kwamba, adhabu ya kifo ni kielelezo cha kutoheshimu zawadi ya uhai. Itakumbukwa kwamba, Baba Mtakatifu Francisko kunako mwaka 2018: “Rescriptum” aliridhia kwa Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa kufanya marekebisho kwenye Katekisimu ya Kanisa Katoliki, kifungu namba 2267 kinachozungumzia kuhusu adhabu ya kifo na tafsiri mpya inapaswa kuingizwa katika vipengele mbalimbali vya Katekisimu ya Kanisa Katoliki. Kanisa Katoliki limefuta adhabu ya kifo katika Mafundisho na Mapokeo yake kwa kukazia njia zinazotetea na kulinda maisha ya watu, amani na usalama wao dhidi ya adui; kwani hizi ni njia zinazodumisha utu, ustawi na mafao ya wengi. “Kwa kweli leo, kutokana na uwezekano ambao serikali inao siku hizi wa kuweza kufaulu kuzuia uhalifu kwa aliyetenda kosa asiweze kuleta madhara bila kumwondolea kabisa uwezo wa kujikomboa mwenyewe, kesi ambazo kumuua mkosaji ni lazima kabisa kabisa ni chache sana na “kwa kweli karibu haziko kabisa”. Kanisa linafundisha kwa mwanga wa Injili kwamba “Adhabu ya kifo haikubaliki kwa sababu inadhuru haki na utu wa mtu.” Kanisa linaendelea kujizatiti ili kuhakikisha kwamba, adhabu ya kifo inaondolewa duniani kote!
Tafsiri mpya ilianza kutumika baada ya kuchapishwa kwenye Gazeti la “L’Osservatore Romano” tarehe 3 Agosti 2018. Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 25 ya Katiba ya Kitume “Fidei depositum” iliyoridhia kuchapishwa kwa Katekisimu ya Kanisa Katoliki anasema, Katekisimu ya Kanisa Katoliki inakazia kwamba, hatima na kiini chote cha mafundisho ya imani vinaelekezwa katika upendo ambao hauna kikomo. Iwe inaelekezwa kwa ajili ya ukweli wa imani au, matumaini au wajibu wa utendaji wa maadili, upendo wa Mungu utadumu daima. Kanisa kwa kusoma alama za nyakati, linataka kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha utu, heshima na uhai wa binadamu dhidi ya adhabu ya kifo inayokumbatia utamaduni wa kifo. Mwenyezi Mungu anawapatia waja wake nafasi ya kutubu na kumwongokea, ili aweze kuwakirimia msamaha na kuwaonjesha tena huruma na upendo wake usiokuwa na kifani! Baba Mtakatifu Francisko anafafanua kwamba, hapa hakuna kinzani na Mafundisho ya Kanisa yaliyopita, kwani jambo la msingi ni kusimama kidete kulinda uhai wa binadamu tangu pale anapotungwa mimba hadi mauti ya kawaida yanapomfika mtu kadiri ya mpango wa Mungu. Huu ni mwendelezo wa uelewa wa kina wa Mafundisho tanzu ya Kanisa kwani, adhabu ya kifo ina madhara makubwa kwa utu na heshima ya binadamu. Hivyo, Kanisa katika mafundisho, maisha na ibada zake, linaendeleza daima na kuvirithisha vizazi vyote ukweli juu yake, na juu ya yale anayoyaamini. Huu ni muhtasari wa asili na utume wa Kanisa unaofafanuliwa katika mafundisho na maisha yake, kama chachu muhimu inayowaunganisha na kuwawezesha waamini kuwa ni watu wa Mungu.
Baba Mtakatifu anakaza kusema, “Amana ya imani” ni endelevu kama lilivyo pia Neno la Mungu, linalokuwa na kuendelea kukomaa katika maisha ya waamini. Na kamwe haliwezi kudumazwa na binadamu kama anavyobainisha Mtakatifu Vincent wa Lèrins kwani hii ni sehemu ya ukweli mfunuliwa unaotangazwa na kurithishwa na Mama Kanisa na wala si mabadiliko ya Mafundisho tanzu ya Kanisa, kwani hii pia ni kazi ya Roho Mtakatifu ndani ya Kanisa. Kama ilivyokuwa wakati wa Agano la Kale Mwenyezi Mungu ambaye alinena zamani na mababa katika manabii kwa sehemu nyingi na kwa njia nyingi na sasa anazungumza kwa njia ya Mwanaye Kristo Yesu, mwaliko kwa waamini kuisikiliza sauti hii kwa umakini, ili kuliwezesha Kanisa kusonga mbele kwa ari na moyo mkuu kama ilivyokuwa wakati wa Kanisa la mwanzo. Mageuzi kuhusu adhabu ya kifo ni sehemu ya mwendelezo wa Mafundisho ya Mtakatifu Yohane Paulo katika Waraka wake wa Kitume, “Evangelium vitae” yaani “Injili ya uhai.” Alipinga adhabu ya kifo na hatimaye, Katekisimu ya Kanisa Katoliki ikafanyiwa marekebisho na kwamba, adhabu ya kifo ingeweza kutumika ikiwa kama njia zisizohusisha umwagikaji wa damu zinatosha kutetea na kulinda maisha ya watu, amani na usalama wao dhidi ya adui, kwa kweli njia hizi karibu haziko kabisa. Adhabu ya kifo ni ukatili mkubwa na usio wa lazima.
Baba Mtakatifu Benedikto XVI naye alikazia umuhimu wa wakuu wa Serikali kufutilia mbali adhabu ya kifo, ili kudumisha: haki, utu wa binadamu, amani na utulivu. Papa Francisko pia anasema adhabu ya kifo haikubaliki kwa sababu inadhuru haki na utu wa mtu. Haitoi nafasi ya mtu kujitetea mbele ya vyombo vya sheria. Kutokana na mwelekeo huu Kanisa linawataka viongozi wa Serikali kusimama kidete kulinda na kutetea uhai wa binadamu kama ambavyo inafafanuliwa kwenye kipengele cha 2265 na 2266, KKK. Mwanga wa Injili unaliwezesha Kanisa kufahamu vyema zaidi kazi ya uumbaji inayofumbatwa katika Fumbo la Umwilisho; ikatakaswa na kupewa utimilifu wake. Ni mwaliko wa kuwa na huruma na subira kwa kutoa nafasi kwa watu kutubu na kuongoka. Mwelekeo mpya wa Katekisimu unatambua utu na heshima ya binadamu pamoja na umuhimu wa kuendeleza majadiliano ili hatimaye, kufutilia mbali adhabu ya kifo duniani.