Jinsi Wokovu Ulivyoingia Kwenye Nyumba ya Zakayo Mtoza Ushuru
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Katekesi kuhusu: “Roho Mtakatifu na Bibi Arusi. Roho Mtakatifu anawaongoza watu wa Mungu kuelekea kwa Yesu, tumaini letu” ni sehemu ya maandalizi ya Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo yanayonogeshwa na kauli mbiu “Peregrinantes in spem” yaani “Mahujaji wa matumaini.” “Basi palikuwa na mtu mmoja wa Mafarisayo, jina lake Nikodemo, mkuu wa Wayahudi. Huyo alimjia usiku, akamwambia, Rabi, twajua ya kuwa u mwalimu, umetoka kwa Mungu; kwa maana hakuna mtu awezaye kuzifanya ishara hizi uzifanyazo wewe, isipokuwa Mungu yu pamoja naye. Yesu akajibu, akamwambia, Amin, amin, nakuambia, Mtu asipozaliwa mara ya pili, hawezi kuuona ufalme wa Mungu. Nikodemo akamwambia, Awezaje mtu kuzaliwa, akiwa mzee?” Yn 3:1-3. Hii ni sehemu ya Maandiko Matakatifu iliyoongoza Katekesi ya Baba Mtakatifu Francisko, Jumatano tarehe 19 Machi 2025 na kunogeshwa na kauli mbiu “Hamna budi kuzaliwa mara ya pili.” Baba Mtakatifu amekwisha kugusia kuhusu yule Mwanamke Msamaria aliyekutana na Kristo Yesu akamwomba maji ya uzima wa milele. Baba Mtakatifu Francisko katika mwanga wa Injili kuhusu: Kodi, Sheria, Kutopendelea, Ukweli na Uwazi, anasema haya ni mambo ambayo yanaongoza kila siku maisha ya watu wa Mungu. Watawala wote wa dunia, walianzisha kodi na kama ilivyokuwa hata nyakati za Kristo Yesu. Warumi katika utawala wa Kaisari waliwatoza watu kodi, kazi iliyotekelezwa na watoza ushuru na kati yao alikuwepo Zakayo, mkubwa mmoja kati ya watoza ushuru naye alikuwa tajiri. Rej. Lk 19:1-9.
Zakayo alipata bahati ya kutembelewa na Kristo Yesu, akatubu na kumwongokea Mungu na wokovu ukaingia katika nyumba yake. Itakumbukwa kwamba, hata Mathayo alikuwa Mtoza ushuru na Kristo Yesu alimwita Mathayo akiwa forodhani, akaondoka akamfuata. Mathayo mtoza ushuru, akawa: Mfuasi, Mtume na Mwinjili. Itakumbukwa kwamba, Mathayo ndiye yule Mwinjili aliyetazamwa kwa jicho la huruma na upendo.Baba Mtakatifu katika Katekesi yake kuhusu Kristo Yesu, chemchemi ya matumaini kwa waja wake, maisha ya Kristo Yesu, Jumatano tarehe 2 Aprili 2025 amemzungumzia Zakayo Mtoza ushuru na jinsi ambavyo wokovu ulivyoingia nyumbani mwa tajiri huyu. Rej Lk 19: 1-10. Zakayo kwa lugha ya Kiebrania “Zakai” maana yake ni msafi, mnyofu, mtu mwenye haki. Mtoza ushuru kwa lugha ya Kigiriki anaitwa “Telones”, kumbe Zakayo ni “Archi-telones” yaani “Mkuu wa watoza ushuru. Zakayo alikuwa ni mkuu wa watoza ushuru aliyekuwa anaifanya kazi hii kwa ajili ya utawala wa Kirumi. Alikuwa ni tajiri wa kutupwa kwa sababu alipenda na kukumbatia sana rushwa katika maisha yake, lakini kwa bahati mbaya alikuwa ni mfupi wa kimo, hali iliyomfanya kudharauriwa na jamii iliyokuwa inamzunguka. Lakini alikuwa ni mtu aliyekuwa na kiu ya kutaka kumwona Kristo Yesu ambaye alisikia sana kuhusu habari zake. Kwa sababu ya ufupi wa kimo alipanda juu ya mti wa mkuyu ili Yesu anapopita yeye apate kumwona, naye Kristo Yesu alipomwona akamwambia ashuke na akaenda naye hadi nyumbani kwake. Katika muktadha huu, Kristo Yesu, anaonesha utashi wa kutekeleza mapenzi ya Baba yake wa mbinguni, kama ufunuo wa huruma na upendo wa Mungu kwa maskini, wadhambi na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa vipaumbele vya jamii.
Baba Mtakatifu Francisko anasema, Zakayo Mtoza ushuru anayo nafasi ya pekee katika hija ya maisha ya kiroho, kwani mwanzoni alionekana kuwa ni mtu asiye na matumaini, akajitahidi kumtafuta Kristo Yesu, bila kufahamu kwamba, Kristo Yesu alikuwa amekwisha anza kumtafuta kitambo! Hata leo hii, Kristo Yesu bado anaendelea kutembelea maeneo ya vita, mateso na mahangaiko ya watu wasiokuwa na hatia; watu wanaosiginwa utu, heshima na haki zao msingi kutokana na umaskini, magonjwa na baa la njaa. Kristo Yesu, hakuona sababu ya kutoa “mahubiri wala kumkaripia” Zakayo mtoza ushuru licha ya manung’uniko ya watu, lakini Kristo Yesu akaamua kushinda nyumbani mwa Zakayo ambaye alikuwa amejitumbukiza na hatimaye kumezwa na malimwengu kiasi cha kuzalisha dhambi nyingi katika maisha yake. Baba Mtakatifu anasikitika kusema kwamba, hata leo hii, pengine, waamini wengi wangeliona tukio hili kuwa ni kashfa ya mwaka. Lakini ikumbukwe kwamba, kitendo cha kuwadharau na kuwatenga wadhambi kinawaongezea “usugu” wa kutenda mabaya zaidi na kuwa na moyo mgumu hata dhidi ya jumuiya. Mwenyezi Mungu analaani dhambi zinazotendwa na mdhambi, lakini anajitahidi usiku na mchana ili kuhakikisha kwamba, mdhambi anaokolewa na kurejeshwa tena kwenye njia ya haki.
Kwa mtu ambaye katika hija ya maisha yake hapa duniani, anadhani kwamba, hajawahi kuonja huruma na upendo wa Mungu katika maisha yake, inakuwa ni vigumu kuweza kufahamu ukuu wa tendo hili na maneno yanayotolewa na Kristo Yesu kwa Zakayo mtoza ushuru. Moyo wa ukarimu, upendo na hali ya kujali pamoja na kuguswa na mahangaiko ya Zakayo mtoza ushuru yanasaidia kuleta toba, wongofu wa ndani na malipizi ya dhambi zake. Uwepo wa Kristo Yesu nyumbani mwa Zakayo mtoza ushuru, kuna mwezesha kuona na kusoma historia na matukio mbalimbali ya maisha yake katika mwanga mpya, lakini zaidi kutokana na jicho la upendo kutoka kwa Kristo Yesu ambalo lilipenyeza hadi katika “sakafu ya undani wa maisha yake.” Kwani alihisi kutengwa na kutopendwa na jamii iliyokuwa inamzunguka, kiasi cha kudhararuriwa na jamii. Zakayo akaongoka na kuwa mtu mpya, akawa na mwelekeo tofauti kabisa wa jinsi ya kutumia fedha na mali, badala ya kumezwa na uchu wa fedha, mali na utajiri wa haraka haraka, Zakayo akagundua njia mpya ya kuwasaidia maskini. Ni katika muktadha huu, Zakayo mtoza ushuru anaamua kutoa nusu ya mali yake na kuwapatia maskini na ikiwa kama alikuwa amemnyang’anya mtu kitu kwa hila atamrudishia mara nne, matendo makuu ya Mungu kwa wadhambi, wanaotubu na kumwongokea Mungu. Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, Zakayo Mtoza ushuru alikuwa na ujasiri, akatia nia ya kukutana na Kristo Yesu katika hija ya maisha yake. “Zakayo, shuka upesi, kwa kuwa leo imenipasa kushinda nyumbani mwako. Akafanya haraka, akashuka, akamkaribisha kwa furaha.” Lk 19: 5-6. Mwenyezi Mungu daima anamtafuta mdhambi, ili atubu na kumwongokea. Zakayo mtoza ushuru anaonesha ile njia ya upendo wa dhati pasi na “ndoana” yaani: upendo wa nipe nikupe!
Zakayo Mtoza ushuru aliyekuwa “amemezwa na kusiginwa” na malimwengu kwa uchu wa mali na fedha ya rushwa na ufisadi, anageuka kuwa mkarimu na mgawaji wa mapaji na utajiri ambao Mwenyezi Mungu amemkirimia katika maisha yake, kiasi hata cha kufurahia ukarimu huu unaobubujika kutoka katika undani wa moyo wake, ulioonja huruma na upendo wa Mungu. Zakayo Mtoza ushuru anatambua kwamba, anapendwa na kuthaminiwa na Mwenyezi Mungu licha ya “ufupi wake” na dhambi zote alizowahi kutenda katika maisha, anageuka kuwa ni shuhuda na chombo cha upendo kwa maskini kwa kutumia fedha na utajiri wake kama alama ya umoja na mshikamano wa upendo. Zakayo Mtoza uhuru ameonja huruma, upendo na msamaha wa dhambi zake licha ya manung’uniko ya watu waliomzunguka. Baba Mtakatifu Francisko anasema, mtazamo wa Kristo Yesu kwa Zakayo mtoza ushuru, anayemwita kwa jina kuonesha kwamba, kwa hakika alikuwa anamfahamu ni kielelezo cha maisha na utume wa Kristo Yesu, aliyetumwa kama mmisionari wa kwanza, kwani “Mwana wa Adamu alikuja kuwatafuta na kuwaokoa watu waliopotea.” Lk 19:10. Akiwa mjini Yeriko, Kristo Yesu alipofika mahali pale, alitazama juu na kumwambia Zakayo, shuka upesi, kwa kuwa leo imenipasa kushinda nyumbani mwako, kielelezo cha unyenyekevu unaofumbatwa katika historia nzima ya wokovu na kwa namna ya pekee kabisa katika Fumbo la Umwilisho. Siku ile iliyotangulia kuteswa kwake, Kristo Yesu aliweka Sakramenti ya Ekaristi Takatifu, Daraja takatifu; akaonesha unyenyekevu katika huduma ya upendo kwa kuwaosha mitume wake miguu, ili kuwarejeshea utu na heshima yao kama watoto wa Mungu.
Mitazamo kati ya Kristo Yesu na Zakayo mtoza ushuru ni muhtasari wa historia nzima ya wokovu inayomwonesha Mwenyezi Mungu akijishusha ili kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti. Mwenyezi Mungu anaendelea kumwangalia mwanadamu katika matumaini, changamoto kwa waamini ni kuhakikisha kwamba, wanavuka vikwazo, tayari kumkaribisha Kristo Yesu katika maisha yao. Zakayo Mtoza ushuru akasimama kwa ujasiri mkubwa kama mtu aliyefufuka kwa wafu na kuanza kutangaza dira na mwelekeo mpya wa maisha, kwa kupiga hatua madhubuti katika maisha yake ya kiroho, kwa kuangalia historia ya maisha yake na kutambua hatua muhimu za toba na wongofu wa ndani. Jambo la msingi anasema Baba Mtakatifu kamwe waamini wasikate tamaa ya maisha, bali wawe na matumaini kwamba, toba na wongofu wa ndani ni jambo linalowezekana katika maisha. Jambo la msingi ni kuendelea kutia nia ya kukutana na Kristo Yesu katika hija ya maisha yao, ili kuonja huruma na upendo wa Mungu unaomwandama mwanadamu katika hija yake ya maisha hapa ulimwenguni.