Tafuta

Cookie Policy
The portal Vatican News uses technical or similar cookies to make navigation easier and guarantee the use of the services. Furthermore, technical and analysis cookies from third parties may be used. If you want to know more click here. By closing this banner you consent to the use of cookies.
I AGREE
PROGRAMU YA KISWAHILI
Ratiba Podcast
Baba Mtakatifu Francisko amewahakikishia washiriki wote wa maadhimisho ya kumbukizi ya miaka 20 tangu kifo cha Mt. Yohane Paulo II baraka zake za kitume. Baba Mtakatifu Francisko amewahakikishia washiriki wote wa maadhimisho ya kumbukizi ya miaka 20 tangu kifo cha Mt. Yohane Paulo II baraka zake za kitume.  (Vatican Media)

Kumbukizi ya Miaka 20 ya Maisha na Utume Wa Papa Yohane Paulo II

Papa Francisko amewahakikishia washiriki wote wa maadhimisho ya kumbukizi ya miaka ishirini tangu kifo cha Mtakatifu Yohane Paulo II baraka zake za kitume. Hayo yamo katika barua aliyomwandikia Kardinali Stanisław Dziwisz, ambaye pia ameshiriki katika Ibada ya Misa Takatifu iliyoongozwa na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican. Katika mahubiri yake, amemkumbuka Mtakatifu Yohane Paulo II kuwa ni shuhuda wa imani, matumaini na mapendo makuu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mama Kanisa anaadhimisha Kumbukizi ya Miaka 20 tangu alipofariki dunia Mtakatifu Yohane Paulo II yaani tarehe 2 Aprili 2005, “dies natalis” yaani kuzaliwa katika utimilifu wa maisha ya mwanadamu. Baba Mtakatifu Francisko amewahakikishia washiriki wote wa maadhimisho ya kumbukizi ya miaka ishirini tangu kifo cha Mtakatifu Yohane Paulo II baraka zake za kitume. Hayo yamo katika barua aliyomwandikia Kardinali Stanisław Dziwisz, Askofu mkuu mstaafu wa Jimbo kuu la Kraków, nchini Poland ambaye pia ameshiriki katika Ibada ya Misa Takatifu iliyoongozwa na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican. Katika mahubiri yake, amemkumbuka Mtakatifu Yohane Paulo II alivyo ukumbatia Msalaba wakati wa Njia ya Msalaba kuzunguka Magofu ya Colosseo, alipoonekana kwenye dirishani, huku akishindwa kuzungumza na waamini na alipofariki dunia, kuamkia maadhimisho ya Dominika ya Huruma ya Mungu. Katika kipindi chote hiki, watu wa Mungu waliungana na Mtakatifu Yohane Paulo wa Pili katika mshikamano wa sala, huku akiendelea kujiachilia mikononi mwa Baba mwenye huruma, kwa ajili ya maisha na uzima wa milele. Mtakatifu Yohane Paulo wa Pili ni shuhuda wa imani na daima alijitahidi kutekeleza mapenzi ya Mungu katika maisha na utume wake kwani hata katika maisha na kifo, daima waamini wanaendelea kuwa ni watu wa Mungu. Katika kipindi cha miaka ishirini na sita kama Khalifa wa Mtakatifu Petro alijitahidi kuwa ni hujaji wa matumaini na chombo cha uinjilishaji wa kina hadi miisho ya dunia, huku akiwahamasisha Wakristo kutweka hadi kilindini “Duc in altum” kama mahujaji wa matumaini, tayari kuingia katika Millenia ya Tatu ya Ukristo.

Umati mkubwa wa watu wa Mungu umeshiriki katika kumbukizi hii
Umati mkubwa wa watu wa Mungu umeshiriki katika kumbukizi hii   (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Mtakatifu Yohane Paulo II alishiriki kikamilifu katika Maadhimisho ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican na akajitahidi kuhakikisha kwamba, maazimio yake yanamwilishwa katika maisha na utume wa Kanisa na kamwe waamini wasiogope kumfungulia Kristo Yesu malango ya maisha yao kwani Kristo Yesu anayo maneno ya uzima wa milele. Rej Yn 6:68.Mtakatifu Yohane Paulo II ni kiongozi aliyewamasisha viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa kuhakikisha kwamba, wanasimama kidete kulinda na kudumisha: Utu, heshima, haki msingi za binadamu; Ustawi, maendeleo na mafao ya wengi kwa kuhakikisha kwamba, wanalinda amani, lakini kama ilivyokuwa kwa Manabii wengi, sauti yake kuhusu umuhimu wa kudumisha amani duniani, iligonga mwamba, na watu wakaendelea kupigana sehemu mbalimbali za dunia. Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican wanasema, Kanisa ni Takatifu kwa maana Kristo, Mwana wa Mungu anayetangazwa pamoja na Baba na Roho Mtakatifu kwamba ni peke yake mtakatifu, amelipenda Kanisa kama Bibiarusi wake, akajitoa mwenyewe kwa ajili yake ili alitakatifuze, akaliunganisha naye kama mwili wake, akarikirimia kipaji cha Roho Mtakatifu, kwa utukufu wa Mungu! Kumbe, watu wote wa familia ya Mungu wanaitwa kuwa ni watakatifu! Haya ndiyo mapenzi ya Mungu. Kristo Yesu ndiye chemchemi na utimilifu wa utakatifu wote! Waamini wanahimizwa kujivika moyo wa rehema, utu wema, unyenyekevu, upole na uvumilivu na wawe na matunda ya Roho Mtakatifu ili wafanywe watakatifu. Kutokana na udhaifu wa binadamu, waamini wanahitaji mara kwa mara kuonjeshwa huruma na upendo wa Mungu katika maisha yao!

Kristo Yesu anayo maneno ya uzima wa milele.
Kristo Yesu anayo maneno ya uzima wa milele.   (Vatican Media)

Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican wanaendelea kudadavua kuhusu Fumbo la Kanisa kwa kusema, Wakristo wote wanaitwa na kuhamasishwa kushiriki utakatifu mmoja, kwa kumtii na kumwabudu Mwenyezi Mungu katika roho na kweli; kwa kumfuasa Kristo Yesu aliyekuwa ni: mtii, fukara na mnyenyekevu wa moyo, aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu, kwa njia hii, wastahilishwe kushiriki utukufu wa Kristo! Watakatifu na wenye heri wengi waliotangazwa na Mtakatifu Yohane Paulo II enzi ya uhai wake, sasa ni waombezi wa Kanisa huko mbinguni, ili liendelee kuwa ni chombo cha wokovu, lijikite katika ujenzi wa amani, ili kujenga mshikamano, umoja na udugu wa kibinadamu. Mtakatifu Yohane Paulo II awaombee watu watakatifu wa Mungu, ili waendelee kuwa ni mahujaji wa matumaini na Kanisa kama chombo cha amana na utajiri wa huruma na upendo wa Mungu.Itakumbukwa kwamba, Mtakatifu Yohane Paulo wa Pili alizaliwa huko Wadowice nchini Poland tarehe 18 Mei 1920 na kupewa jina la Karol Josef Wojtyla. Akiwa na umri wa miaka 20, alifiwa na wazazi wake pamoja na ndugu yake. Katika huzuni na upweke huu, Karol alivutwa sana na maisha na wito wa kipadre na hatimaye, akajiunga na seminari ya siri na kupewa Daraja Takatifu ya Upadre, tarehe Mosi, Novemba 1946. Papa Pius XII kunako tarehe 4 Julai 1958 akamteuwa kuwa Askofu msaidizi wa Jimbo kuu la Kraków, nchini Poland. Akatekeleza dhamana ya kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu kwa ari, moyo mkuu na unyenyekevu wa hali ya juu kabisa. Mtakatifu Paulo VI kunako tarehe 13 Januari 1964, akamteuwa kuwa Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Kraków. Tarehe 26 Juni 1967 akateuliwa na Mtakatifu Paulo VI kuwa Kardinali. Akachaguliwa kuliongoza Kanisa Katoliki tarehe 16 Oktoba 1978, akiwa ni Papa wa 264 kuliongoza Kanisa Katoliki. Tarehe 22 Oktoba 1978 akasimikwa na kuanza kutekeleza utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro kwa: kuongoza, kufundisha na kuwatakatifuza watu wa Mungu. Mtakatifu Yohane Paulo II alifariki dunia tarehe 2 Aprili, 2005.

Papa Yohane Paulo II alitangazwa kuwa Mtakatifu 27 Aprili 2014
Papa Yohane Paulo II alitangazwa kuwa Mtakatifu 27 Aprili 2014   (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Baba Mtakatifu Benedikto XVI, Mei Mosi, 2011 akamtangaza kuwa Mwenyeheri mbele ya bahari ya watu kutoka sehemu mbalimbali za dunia. Baba Mtakatifu Francisko akamtangaza kuwa Mtakatifu tarehe 27 Aprili 2014 sanjari na Papa Yohane XXIII, Muasisi wa Maadhimisho ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican. Mtakatifu Yohane Paulo II ameacha kumbu kumbu ya kudumu katika akili na nyoyo za watu wengi na kwamba, haitakuwa rahisi sana kuweza kufutika. Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuiga karama na maisha ya Mtakatifu Yohane Paulo II, kwa kujisadaka kwa ajili ya huduma kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, sanjari na kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa kukuza ari na mwamko na huduma za kimisionari. Itakumbukwa kwamba, Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican ulikuwa ni dira na mwongozo wa maisha na utume wa Mtakatifu Yohane Paulo II kama Khalifa wa Mtakatifu Petro. Ustawi, maendeleo na mafao ya wengi, daima binadamu na mahitaji yake msingi, ndicho alichopenda kuona kwamba, kinavaliwa njuga na Mama Kanisa katika mapambazuko ya Millenia ya Tatu ya Ukristo!

Utume wa Kanisa kwa vijana ni alama isiyofutika kabisa
Utume wa Kanisa kwa vijana ni alama isiyofutika kabisa   (Vatican Media)

Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican ni neema kubwa sana ambayo Mwenyezi Mungu amelijalia Kanisa lake. Neema hii ikamwilishwa katika maisha na utume wa Kanisa kwa njia ya Mtakatifu Yohane Paulo II aliyetangaza na kushuhudia amana na utajiri wa Mafundisho ya Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican katika maisha na utume wa Kanisa katika ulimwengu mamboleo. Mtakatifu Yohane Paulo II aliweza kufanya hija za kitume 104 nje ya Italia. Akabarikiwa kufanya hija za kichungaji 142 nchini Italia, daima maneno yake yaliambatana na vitendo; akagusa na kufariji mamilioni ya watu duniani, huku akitangaza na kushuhudia uhuru wa kidini na uhuru wa kuabudu kama kiini cha haki msingi za binadamu! Matokeo yake ni kuanguka kwa Ukuta wa Berlin kunako mwaka 1989. Kanisa likatoka kifua mbele na kusimama kidedea ili kupinga sera za kibaguzi zilizoigawa dunia, kati ya Kaskazini na Kusini: likaimarisha tunu msingi za maisha ya Kikristo, kwa kujikita katika haki, amani, ustawi na maendeleo ya wengi kama kanuni msingi za Mafundisho Jamii ya Kanisa. Hija za kichungaji zilizofanywa na Mtakatifu Yohane Paulo II, zilikuwa ni sehemu ya mchakato wa uinjilishaji na ushuhuda wa kimisionari katika kukuza na kudumisha utu, heshima, ustawi na maendeleo ya wanawake ndani na nje ya Kanisa.

Mtakatifu Yohane Paulo II aliwekeza sana kwa vijana
Mtakatifu Yohane Paulo II aliwekeza sana kwa vijana   (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Mtakatifu Yohane Paulo II katika Wosia wake wa Kitume, “Evangelium vitae” yaani “Injili ya uhai”; kwa ufupi anakazia kuhusu: Thamani ya maisha, ukuu na utu wa binadamu kama zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Hii ni Injili ya upendo wa Mungu kwa binadamu; Utu na heshima yake, mambo msingi yanayofumbatwa katika Injili. Katika ulimwengu mamboleo kuna mambo ambayo yanaendelea kutishia Injili ya uhai kwa kukumbatia utamaduni wa kifo. Haya ni matokeo ya watu kukengeuka pamoja na kuporomoka kwa kanuni maadili na utu wema. Kuna sera na mikakati mbali mbali ya kisiasa, kiuchumi na kijamii inayotishia Injili ya uhai, ustawi na maendeleo ya wengi. Mtakatifu Yohane Paulo II anawataka waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kusimama kidete: kuheshimu, kulinda na kuhudumia Injili ya uhai, ili kukuza na kudumisha haki, maendeleo fungamani ya binadamu, uhuru wa kweli, amani na furaha ya kweli inayobubujika kutoka katika sakafu ya maisha ya mwanadamu. Mtakatifu Yohane Paulo II anasema, usiue kwa sababu maisha ya mwanadamu ni matakatifu na yasioharibika na kwamba, Mwenyezi Mungu ni chanzo na utimilifu wa maisha ya binadamu. Waamini wanapaswa kujipambanua kuwa ni watu wanaotetea Injili ya uhai kwa ajili ya maisha. Kristo Yesu ni chemchemi ya utimilifu wa maisha, mwaliko kwa waamini kuwa ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo, kwa sababu maisha ni tunu adhimu inayofumbatwa katika maadili na maisha ya kiroho. Huduma shufaa itolewe kwa kuzingatia maboresho katika huduma ya afya. Injili ya uhai ni dhamana inayopaswa kutekelezwa na mtu binafsi, familia na jamii katika ujumla wake. Wanasiasa wanapaswa kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo.

Waamini wasiogope kumfungulia Kristo Yesu malango ya maisha yao
Waamini wasiogope kumfungulia Kristo Yesu malango ya maisha yao   (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Mtakatifu Yohane Paulo II kwa kufuata dira na mwongozo wa Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican, akaimarisha mchakato wa majadiliano ya kidini na kiekumene; kiasi hata cha kujiweka chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa. Ni kiongozi aliyetambua na kuthamini sana mchango wa wanawake katika ustawi na maendeleo ya jamii na Kanisa katika ujumla wake, mambo yanayojionesha hata katika Nyaraka zake za kichungaji “Mulieris dignitatem” yaani “Utu na wito wa mwanamke.” Alikazia sana umuhimu wa utakatifu wa maisha ya Kikristo kama kielelezo cha uaminifu kwa Kristo na Kanisa lake, kiasi cha kuthubutu kuwatangaza watakatifu wapya 482 na wenyeheri 1319, mwaliko na changamoto ya kumfuasa Kristo Yesu kama chemchemi ya utakatifu na utimilifu wa maisha ya Kikristo. Mtakatifu Yohane Paulo wa II, alikuwa na karama ya pekee katika maisha na utume wa Kanisa kwa vijana, kwani hawa kwake walikuwa ni jeuri na matumaini ya Kanisa na jamii katika ujumla wake, utume ambao unaendelea kutekelezwa na Mama Kanisa hata katika nyakati hizi. Majadiliano kati ya Mtakatifu Yohane Paulo II na vijana wa kizazi kipya, waliompenda upeo, ni ushuhuda unaojionesha hadi wakati huu kutokana na maadhimisho ya Siku za vijana kitaifa na Kimataifa. Katika maisha na utume wake, aligusa medani mbalimbali za maisha ya binadamu; akaimarisha mafundisho msingi ya Kanisa yanayofumbatwa katika huruma ya Mungu, Roho Mtakatifu, Uhusiano kati ya imani na akili; Ari na mwamko wa kimisionari ndani ya Kanisa. Mtakatifu Yohane Paulo II, hata dakika zake za mwisho katika udhaifu wa mwili na magonjwa, aliendelea kuwa ni: Shuhuda, Nabii na Chombo cha Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo. Akafanikiwa kuonesha ukuu, utakatifu, utu na heshima ya binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu.

Mt. Yohane Paulo II
02 Aprili 2025, 16:08
Prev
April 2025
SuMoTuWeThFrSa
  12345
6789101112
13141516171819
20212223242526
27282930   
Next
May 2025
SuMoTuWeThFrSa
    123
45678910
11121314151617
18192021222324
25262728293031