Papa Francisko: Mahubiri Dominika ya Matawi Mwaka C: Simoni Mkirene
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Mama Kanisa tarehe 13 Aprili 2025 ameadhimisha Dominika ya Matawi kwa maandamano makubwa; mwanzo wa maadhimisho ya Juma Kuu, Mama Kanisa anapoadhimisha Mafumbo ya Wokovu wa binadamu yanayofumbatwa katika: Mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu; ufufuko uletao wokovu na maisha ya uzima wa milele. Hiki ni kiini cha maadhimisho ya Mwaka wa Liturujia wa Kanisa. Waamini wanaliishi Fumbo hili kila wakati wanapoadhimisha Fumbo la Ekaristi Takatifu, chanzo na kilele cha maisha na utume wa Kanisa. Ibada ya Misa Takatifu inapyaisha Fumbo la Pasaka yaani: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu. Hii ni Njia ya Msalaba kuelekea Mlimani Kalvari. Dominika ya Matawi, Mama Kanisa anakumbuka siku ile Kristo Yesu, alipoingia mjini Yerusalemu kwa shangwe kama Mfalme na Masiha na kushangiliwa kama Mwana wa Daudi anayeleta wokovu. Hii ndiyo maana ya wimbo wa Hosana. Ni Mfalme wa utukufu anayeingia Yerusalemu akiwa amepanda Mwana punda na kushangiliwa na Watoto wa Wayahudi kama kielelezo cha amani na unyenyekevu wake. Kristo Yesu ndiye Mbarikiwa ajaye kwa jina la Bwana; ndiye Masiha na Mpakwa wa Bwana, aliyejisadaka Msalabani ili kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti, na hivyo kumshikirisha maisha ya uzima wa milele.
Mababa wa Kanisa wanasema kwamba, Kristo Yesu ni sadaka safi iletayo amani na utulivu moyoni ili kukamilisha kazi nzima ya ukombozi kwa kuviweka vitu vyote chini ya utawala wa Ufalme wake. Huu ni Ufalme wa: Kweli, Uzima, Utakatifu, Neema, Haki, Amani na Mapendo. Kristo Yesu ni Mfalme ambaye ufalme wake unajikita katika mantiki ya Injili yaani: Huruma, Upendo Msamaha na Unyenyekevu. Hii ni sadaka; katika hali ya ukimya wenye kuwajibisha na katika nguvu ya ukweli. Utawala wake ni tofauti kabisa na watawala wa dunia hii: wenye uchu wa mali na madaraka, wanaoshindana na kugombana; wanaopigana kwa kutumia silaha za hofu na woga; rushwa na udanganyifu katika dhamiri za watu. Falme za dunia hii wakati mwingine, zinajiimarisha kwa kujitutumua, kwa njia ya kinzani na hata dhuluma. Ufalme wa Kristo Yesu una ambata haki, amani na upendo na kwamba; umejinua kwa namna ya ajabu kabisa katika Fumbo la Msalaba, Kristo Yesu aliposhinda dhambi na mauti na kuonesha utukufu wa Msalaba, kielelezo cha sadaka ya Kristo Yesu kwa waja wake. Hii ni changamoto kwa Wakristo kufanya rejea katika nguvu ya Fumbo la Msalaba chemchemi ya: huruma na upendo wa Kristo Yesu, hata baada ya kukataliwa na wanadamu, lakini akaonesha ushindi wa kishindo, kwa ajili ya ukombozi wa binadamu.
Ni katika muktadha wa mwanzo wa maadhimisho ya Juma Kuu, katika Mkesha wa Dominika ya Matawi, Jumamosi tarehe 12 Aprili 2025, Baba Mtakatifu Francisko amekwenda kutembelea Kanisa kuu la Bikira Maria mkuu, Jimbo kuu la Roma, ili kusali kwenye Sanamu ya Bikira Maria Afya ya Warumi “Salus Populi Romani” iliyoko kwenye Kanisa kuu la Bikira Maria mkuu na hatimaye, kumkabidhi hija ya maisha ya kiroho ya Kanisa, katika maadhimisho ya Juma kuu kwa mwaka 2025. Itakumbukwa kwamba, Baba Mtakatifu Francisko bado anaendelea na matibabu, sala na kazi ndogo ndogo kwenye Hosteli ya Mtakatifu Martha, iliyoko mjini Vatican. Katika mahubiri yaliyoandaliwa na Baba Mtakatifu Francisko na kusomwa na Kardinali Leonardo Sandri, Mwenyekiti mstaafu wa Baraza la Kipapa kwa ajili ya Makanisa ya Mashariki ambaye pia ni Makamu wa Dekano wa Baraza la Makardinaliamesema, Kristo Yesu aliingia mjini Yerusalemu kwa shangwe kama Mfalme na Masiha, huku akiwa amepanda Mwanapunda ishara ya unyenyekevu, amani na utakatifu wake. Nao watu walimlaki kwa shangwe wakiwa na matawi ya mitende, huku wakiimba nyimbo za furaha na ushindi wakisema: “Ndiye mbarikiwa, Mfalme ajaye kwa jina la Bwana.” Lk 19:38.
Baba Mtakatifu anasema, Kristo Yesu anayeshangiliwa Dominika ya Matawi, ndiye yule yule, baada ya siku chache, ataibuka amelaaniwa, kuhukumiwa na hatimaye, kubebeshwa Msalaba. Waamini katika Dominika ya Matawi, wamemfuata Kristo Yesu kwa maandamano makubwa, huku wakitembea katika Njia ya Msalaba “Via dolorosa” mwanzo wa maadhimisho ya Juma kuu, sehemu muhimu sana ya maandalizi ya maadhimisho ya Fumbo la Pasaka, yaani mateso, kifo na ufufuko wa wafu. Huu ni umati mkubwa uliosheheni watu wa kila namna, lakini kati yao kuna askari na wanawake wanaomlilia Kristo Yesu; kufumba na kufumbua katika Njia hii ya Msalaba “Na walipokuwa wakimwondoa walimkamata mtu mmoja, Simoni Mkirene, aliyekuwa ametoka shamba, wakamtwika Msalaba, auchukue nyuma yake Yesu.” Lk 23:26. Msalaba huu ulikuwa ni mzito, changamoto na mwaliko kwa waamini katika Njia ya Msalaba kumtafakari Simoni Mkirene, kwa kuuangalia moyo wake na hatua zake pamoja na Kristo Yesu.
Simoni Mkirene anaubeba Msalaba si kwa imani, bali kwa kulazimishwa na kwa njia hii, anashiriki pia mateso ya Kristo Yesu na hivyo Msalaba wa Kristo Yesu unakuwa pia ni Msalaba wa Simoni Mkirene. Mtume Petro aliyekuwa ameahidi kumfuasa Kristo Yesu katika Njia yake ya Msalaba, hakuonekana hata kidogo, bali huyu Mkirene, aliyeubeba Msalaba na kumfuasa Kristo, katika hali ya ukimya na kwamba, Msalaba unakuwa ni kielelezo cha mshikamano na Kristo Msulubiwa, akashiriki maumivu. Baba Mtakatifu Francisko anasema, Moyo Mtakatifu wa Kristo Yesu uliochomwa mkuki, ukafunguka, lakini moyo wa binadamu ukabaki ukiwa umefungwa; Msalaba wa Kristo Yesu, ukawa ni kielelezo cha ukombozi wa mwanadamu, Msalaba uliobeba dhambi za walimwengu; kielelezo cha upendo, utii na unyenyekevu kwa Baba yake wa mbinguni, kielelezo kwamba, katika ukombozi hakuna mgeni wala mtu wa nje, wote wanahusishwa kikamilifu. Kristo Yesu anakuja kukutana na watu wote katika hali zao mbalimbali; Mwenyezi Mungu aligeuza chuki na jeuri ya binadamu na kuwa ni sehemu ya ukombozi.
Baba Mtakatifu anawauliza waamini na watu wote wenye mapenzi mema, Je, leo hii kuna watu wangapi wanaobeba Msalaba wa Kristo Yesu? Huu ni mwaliko wa kumwona na kumtambua Kristo Yesu kati ya watu wanaoteseka kwa sababu ya vita, njaa na magonjwa na kwamba, waamini kwa kuubeba vyema Msalaba wa Kristo Yesu wanashiriki pia katika upendo unaookoa. Mateso ya Kristo Yesu yanakuwa ni chemchemi ya upendo, pale ambapo waamini wanawasaidia maskini, wanawanyanyua wale walioteleza na kuanguka na zaidi pale wanapogeuka kuwa ni vyombo na mashuhuda wa faraja kwa watu waliovunjika na kupondeka moyo. Fumbo la Msalaba wa Kristo Yesu ni muujiza mkubwa wa huruma na upendo wa Mungu kwa mwanadamu. Huu ni mwaliko kwa waamini katika maadhimisho ya Juma kuu, kuhakikisha kwamba, wanaubeba Msalaba wa Kristo Yesu nyoyoni mwao; wawasaidie jirani zao wanaoteseka, lakini zaidi, wale watu wasiojulikana, ambao Mwenyezi Mungu amewawezesha kukutana nao katika safari ya maisha. Waamini wajiandae kuadhimisha Pasaka ya Bwana kwa kujitahidi kufuata mfano wa Simoni Mkirene.