Papa ashangaza wanajubilei kwa kufika katika Uwanja wa Mtakatifu Petro na kushukuru!
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Ulikuwa ni mshangao mzuri mwishoni mwa Misa ya Jubilei kwa wagonjwa na ulimwengu wa huduma za afya hasa wa kuwasili kwa Baba Mtakatifu Francisko kwenye uwanja wa Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Dominika tarehe 6 Aprili 2025. Katika kiti cha magurudumu, akifuatana na muuguzi wake wa kibinafsi Massimiliano Strappetti. Ni yeye aliyemepeleka kwenye madhabahu, ambapo, baada ya baraka ya mwisho ya mshereheshaji, Askofu Mkuu Fisichella, alitangaza salamu fupi: Dominika njema kwa kila mtu, asante sana!" Kwa hisia za wote waliokuwepo uwanjani, na wasomaji kisha wakasambaza ujumbe wake wa shukrani.
Katika ujumbe huo Papa Francisko anawasalimu kwa upendo wote walioshiriki katika maadhimisho haya na kuwashukuru kwa dhati kwa sala iliyoinuliwa kwa Mwenyezi Mungu kwa ajili ya afya yake, akitumain kwamba hija ya Jubilei hiyo itakuwa na matunda tele". Kisha ametoa baraka za kitume, anazozipeleka “kwa wapendwa, wagonjwa na wanaoteseka, pamoja na waamini wote waliokusanyika leo”.
Kabla ya kutoka nje katika Uwanja, kwa mujibu wa Ofisi ya Habari ya Vatican iliripoti, kwamba Papa alipokea sakramenti ya upatanisho katika Kanisa kuu la Mtakatifu Petro, na kukaa kitambo kwa sala na baadaye akavuka Mlango Mtakatifu. Kwa hiyo Papa aliungana na wanahija wa Jubilei ya wagonjwa na wa Ulimwengu wa kiafya.