Rambi rambi za Papa kwa waathirika wa kuanguka na klabu ya muziki huko San Domingo!
Vatican News
Baba Mtakatifu Francisko tarehe 10 Aprili 2025 ameeleza masikitiko yake baada ya kupata taarifa za kutisha za kuporomoka kwa klabu ya Muziki ‘Jet Set’ huko Santo Domingo, mji mkuu wa nchi ya Jamhuri ya Dominika, ambayo imesababisha vifo vya zaidi ya 180, kulingana na idadi ya muda iliyotolewa na Kituo cha Operesheni za Dharura. Katika telegram iliyotiwa saini na Kardinali Pietro Parolin, Katibu wa Vatican, kwa niaba ya Papa iliyoelekezwa kwa Askofu Mkuu Francisco Ozoria Acosta, wa Jimbo kuu la Santo Domingo, Papa "anatoa sala zake kwa ajili ya mapumziko ya milele kwa marehemu", na anatuma salamu za rambi rambi za kina kwa familia na "maneno ya faraja." Baba Mtakatifu anawatakia"ahueni ya haraka waliojeruhiwa," ambao ni karibu 250 kulingana na makadirio na anahimiza juhudi za misaada na usindikizaji zinazoendelea kwa sasa.” Zaidi ya yote, Papa Francisko anaomba kwa maombezi ya Bikira Maria, faraja ya wanaoteseka, kama "ishara ya matumaini."
Mshikamano wa maaskofu
Paa la ukumbi huo maarufu liliporomoka jioni ya Jumanne tarehe 8 Aprili 2025 wakati tamasha la muziki likiendelea. Vijana kadhaa walikuwa waathirika. Baraza la Maaskofu wa Dominika (CED) nalo lilionesha mshikamano wake na kuungana katika kuwaombea marehemu. Katika taarifa iliyotolewa kupitia mitandao ya kijamii, maaskofu hao wanamwomba Mwenyezi Mungu azifariji familia za wahanga na kuwaombea majeruhi wapone haraka. Sambamba na hayo, wanaziomba mamlaka na wahudumu wa afya kuendelea kutoa huduma stahiki kwa wahanga na kuwaalika wananchi kuungana na kutoa misaada kwa kutoa kipaumbele kwa magari ya kubebea wagonjwa, kuchangia damu, kutoa taarifa rasmi pekee na kuwaombea walioathirika. Sambamba na majonzi makubwa ya msiba huo, Baraza la Maaskofu limesisitiza umuhimu wa “kuweka matumaini hai”, likimuomba Mwenyezi Mungu azitie msukumo taasisi na wale wanaohusika na usalama wa miundombinu ya umma na binafsi ili kuhakikisha ulinzi wa wale wote wanaoitumia.
Misa kwa ajili ya wahanga
Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu wa Dominika, Monsinyo Faustino Burgos, aliongoza Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya wahanga: ''Tunatoa maadhimisha haya ya Ekaristi kwa ajili ya pumziko la milele wale wote walioaga dunia, ili Bwana azipokee roho zao; pia kwa jamaa zao, ili Bwana awape nguvu; kwa waliojeruhiwa, ili wapone, na kwa mamlaka yetu,” alisema wakati wa maadhimisho hayo. Na kwa upande wa Rais wa Jamhuri ya Dominika, Luis Abinader, alitangaza maombolezo ya kitaifa ya tarehe 8, 9 na 10 Aprili 2025.