Tafuta

Cookie Policy
The portal Vatican News uses technical or similar cookies to make navigation easier and guarantee the use of the services. Furthermore, technical and analysis cookies from third parties may be used. If you want to know more click here. By closing this banner you consent to the use of cookies.
I AGREE
Requiem in Re minore, per coro maschile e orchestra
Ratiba Podcast
Waamini ni vyombo na mashuhuda wa imani kwa Kristo Yesu na Kanisa lake, changamoto ni kuhakikisha kwamba, Kristo Yesu anaendelea kuwa hai miongoni mwao. Waamini ni vyombo na mashuhuda wa imani kwa Kristo Yesu na Kanisa lake, changamoto ni kuhakikisha kwamba, Kristo Yesu anaendelea kuwa hai miongoni mwao.  (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Ujumbe wa Dominika ya Matawi Nchi Takatifu Kwa Mwaka 2025

Waamini ni vyombo na mashuhuda wa imani kwa Kristo Yesu na Kanisa lake, changamoto ni kuhakikisha kwamba, Kristo Yesu anaendelea kuwa hai miongoni mwao. Wao ni watoto wa mwanga na wa ufufuo wa Yesu kwa wafu, wakite maisha yao katika Injili ya upendo inayoshinda mambo yote. Kilele cha Fumbo la Pasaka yaani mateso na kifo ni ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu, mwaliko wa kujenga na kudumisha umoja, ushirika, msamaha na upatanisho!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Dominika ya Matawi, Mama Kanisa anakumbuka siku ile Kristo Yesu, alipoingia mjini Yerusalemu kwa shangwe kama Mfalme na Masiha na kushangiliwa kama Mwana wa Daudi anayeleta wokovu. Hii ndiyo maana ya wimbo wa Hosana. Ni Mfalme wa utukufu anayeingia Yerusalemu akiwa amepanda Mwana punda na kushangiliwa na Watoto wa Wayahudi kama kielelezo cha amani na unyenyekevu wake. Kristo Yesu ndiye Mbarikiwa ajaye kwa jina la Bwana; ndiye Masiha na Mpakwa wa Bwana, aliyejisadaka Msalabani ili kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti, na hivyo kumshikirisha maisha ya uzima wa milele. Mama Kanisa tarehe 13 Aprili 2025 ameadhimisha Dominika ya Matawi kwa maandamano makubwa; mwanzo wa maadhimisho ya Juma Kuu, Mama Kanisa anapoadhimisha Mafumbo ya Wokovu wa binadamu yanayofumbatwa katika: Mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu; ufufuko uletao wokovu na maisha ya uzima wa milele. Hiki ni kiini cha maadhimisho ya Mwaka wa Liturujia wa Kanisa. Waamini wanaliishi Fumbo hili kila wakati wanapoadhimisha Fumbo la Ekaristi Takatifu, chanzo na kilele cha maisha na utume wa Kanisa. Ibada ya Misa Takatifu inapyaisha Fumbo la Pasaka yaani: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu. Hii ni Njia ya Msalaba kuelekea Mlimani Kalvari.

Kardinali Pierbattista Pizzaballa Dominika ya Matawi
Kardinali Pierbattista Pizzaballa Dominika ya Matawi   (ANSA)

Mababa wa Kanisa wanasema kwamba, Kristo Yesu ni sadaka safi iletayo amani na utulivu moyoni ili kukamilisha kazi nzima ya ukombozi kwa kuviweka vitu vyote chini ya utawala wa Ufalme wake.  Huu ni Ufalme wa: Kweli, Uzima, Utakatifu, Neema, Haki, Amani na Mapendo. Kristo Yesu ni Mfalme ambaye ufalme wake unajikita katika mantiki ya Injili yaani: Huruma, Upendo Msamaha na Unyenyekevu. Hii ni sadaka; katika hali ya ukimya wenye kuwajibisha na katika nguvu ya ukweli. Utawala wake ni tofauti kabisa na watawala wa dunia hii: wenye uchu wa mali na madaraka, wanaoshindana na kugombana; wanaopigana kwa kutumia silaha za hofu na woga; rushwa na udanganyifu katika dhamiri za watu. Falme za dunia hii wakati mwingine, zinajiimarisha kwa kujitutumua, kwa njia ya kinzani na hata dhuluma. Ufalme wa Kristo Yesu una ambata haki, amani na upendo na kwamba; umejinua kwa namna ya ajabu kabisa katika Fumbo la Msalaba, Kristo Yesu aliposhinda dhambi na mauti na kuonesha utukufu wa Msalaba, kielelezo cha sadaka ya Kristo Yesu kwa waja wake. Hii ni changamoto kwa Wakristo kufanya rejea katika nguvu ya Fumbo la Msalaba chemchemi ya: huruma na upendo wa Kristo Yesu, hata baada ya kukataliwa na wanadamu, lakini akaonesha ushindi wa kishindo, kwa ajili ya ukombozi wa binadamu.

Waamini ni mashuhuda wa Fumbo la Pasaka
Waamini ni mashuhuda wa Fumbo la Pasaka   (ANSA)

Ni katika muktadha wa maadhimisho ya Dominika ya Matawi, tarehe 13 Aprili 2025, Kardinali Pierbattista Pizzaballa, O.F.M. Patriaki wa Yerusalemu, Mlinzi mkuu wa Nchi Takatifu na Mlima wa Sion katika ujumbe wake kwa watu wa Mungu katika Nchi Takatifu amewakumbusha kwamba, wao ni vyombo na mashuhuda wa imani kwa Kristo Yesu na Kanisa lake, changamoto ni kuhakikisha kwamba, Kristo Yesu anaendelea kuwa hai miongoni mwao. Wao ni watoto wa mwanga na wa ufufuo wa Kristo Yesu kwa wafu, wakite maisha yao katika Injili ya upendo inayoshinda mambo yote. Kilele cha maadhimisho ya Fumbo la Pasaka yaani mateso na kifo ni ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu, mwaliko wa kujenga na kudumisha umoja na ushirika vinavyosimikwa katika msamaha na upatanisho wa kweli.Waamini wamsindikize Kristo Yesu katika Njia yake ya Msalaba kwa sala, machozi na kiu ya uwepo endelevu na angavu wa Kristo Yesu kati yao kwa njia ya Neno lake linalofariji na Sakramenti za Kanisa. Wakristo na watu wote wenye mapenzi mema, waendelee kumpokea Kristo Yesu kama Mfalme na Masiha, wamsindikize katika Njia ya Msalaba na hatimaye, waweze kusimama chini ya Msalaba, alama hai ya upendo wa Mungu unao okoa. Ikumbukwe kwamba, pamoja na changamoto mbalimbali zinazoendelea kuukumba Mji wa Yerusalemu, lakini utaendelea kubaki kuwa ni Mji wa Sala ya Watu wa Mungu: Rej. Isa 56:7 na kwamba, hakuna mtu yeyote yule atakayewatenga na upendo wa Kristo Yesu na Kanisa lake. Rej. Rum 8:35. Wawe tayari kujibu chuki na hasira kwa silaha ya upendo, umoja, ushirika na ukarimu.

Maandamano ya Dominika ya Matawi
Maandamano ya Dominika ya Matawi   (ANSA)

Ikumbukwe kwamba, Yerusalemu ni kielelezo cha Fumbo la Pasaka, yaani mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kwa wafu, kumbe ni mahali pa upatanisho na upendo unao okoa na kufariji, changamoto na mwaliko kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema kujenga umoja na mshikamano wa udugu wa kibinadamu na hivyo kuendelea kubomoa kuta za utengano, ili hatimaye, waamini wenyewe waweze kuwa ni vyombo na mashuhuda wa matumaini “kwa kutarajia yasiyoweza kutarajiwa.” Rum 4:18. Huu ndio ushuhuda unaopaswa kutolewa na waamini licha ya changamoto mbalimbali wanazokumbana nazo katika hija ya maisha yao ya kiroho! Kardinali Pierbattista Pizzaballa, O.F.M. Patriaki wa Yerusalemu, Mlinzi mkuu wa Nchi Takatifu na Mlima wa Sion anahitimisha ujumbe wake kwa maadhimisho ya Dominika ya Matawi kwa Mwaka 2025 akiwataka waamini kamwe wasikate wala kukatishwa tamaa na matumaini; wasiogope, bali wawe na imani thabiti, huku wakiendelea kujizatiti katika ujenzi wa jamii inayosimikwa katika amani, umoja na imani thabiti katika nguvu ya upendo wa Kristo Yesu. “Kwa maana tumekuwa washirika wa Kristo, kama tukishikamana na mwanzo wa uthabiti wetu kwa nguvu mpaka mwisho.” Ebr 3:14.

Matawi Yerusalemu
14 Aprili 2025, 14:39
Prev
April 2025
SuMoTuWeThFrSa
  12345
6789101112
13141516171819
20212223242526
27282930   
Next
May 2025
SuMoTuWeThFrSa
    123
45678910
11121314151617
18192021222324
25262728293031