Tafuta

Cookie Policy
The portal Vatican News uses technical or similar cookies to make navigation easier and guarantee the use of the services. Furthermore, technical and analysis cookies from third parties may be used. If you want to know more click here. By closing this banner you consent to the use of cookies.
I AGREE
Messa da Requiem, per soli, coro e orchestra
Ratiba Podcast
Baraza la Maaskofu Katoliki Italia, CEI kuanzia tarehe 31 Machi hadi tarehe 4 Aprili 2025 linaadhimisha Mkutano wa Pili wa Sinodi ya Makanisa nchini Italia,. Baraza la Maaskofu Katoliki Italia, CEI kuanzia tarehe 31 Machi hadi tarehe 4 Aprili 2025 linaadhimisha Mkutano wa Pili wa Sinodi ya Makanisa nchini Italia,.  (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Ujumbe Kwa Mkutano Wa Pili Wa Makanisa Nchini Italia

Kama sehemu ya utekelezaji wa mchakato wa usindikizaji, tathmini na umwilishaji wa maamuzi ya Sinodi ya XVI ya Maaskofu, Baraza la Maaskofu Katoliki Italia, CEI kuanzia tarehe 31 Machi hadi tarehe 4 Aprili 2025 linaadhimisha Mkutano wa Pili wa Sinodi ya Makanisa nchini Italia, kama sehemu ya tathmini ya safari ya shughuli za kichungaji na kijamii iliyotekelezwa katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, tayari kutoa nafasi kwa Roho Mtakatifu katika mchakato wa utimilifu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini kuliombea Kanisa linaloitwa kutafsiri na hatimaye, kumwilisha mang’amuzi yaliyofanywa katika Maadhimisho ya Sinodi ya XVI ya Maaskofu yaliyonogeshwa na kauli mbiu: “Kwa Ajili ya Kanisa la Kisinodi: Umoja, Ushiriki na Utume.” Lengo kuu la Maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu ni kuliwezesha Kanisa kuendelea kujizatiti katika ujenzi wa utamaduni wa kuwasikiliza na kuwashirikisha waamini walei katika maisha na utume wake. Maadhimisho ya Sinodi za Maaskofu yanapania pamoja na mambo mengine: kujenga na kudumisha urika wa Maaskofu, tayari kumsikiliza Roho Mtakatifu, Mhimili mkuu wa mchakato wa uinjilishaji mpya unaofumbatwa katika ushuhuda wa maisha adili na matakatifu. Baba Mtakatifu anaishukuru Sekretarieti kuu ya Sinodi kwa kuandaa mpango mkakati unaopaswa kutekelezwa na Makanisa Mahalia katika kipindi cha Miaka mitatu kuanzia sasa, yaani kuanzia mwaka 2025. Sekretarieti kuu ya Sinodi za Maaskofu imeyaandikia barua Mabaraza ya Maaskofu Katoliki, kuhusiana na mchakato wa usindikizaji, tathmini na utekelezaji wa maamuzi yaliyotolewa kwenye maadhimisho ya Sinodi ya XVI ya Maaskofu. Mchakato huu umeridhiwa na Baba Mtakatifu Francisko, tayari kwa utekelezaji wake. Baba Mtakatifu anayataka Mabaraza ya Maaskofu Katoliki sehemu mbalimbali za dunia, kuhakikisha kwamba, yanasambaza mchakato huu, ili uweze kuwafikia watu wengi zaidi na kwamba, hitimisho la mchakato huu, utakuwa ni Mkutano wa Kanisa utakaoadhimishwa Mwezi Oktoba 2028, mjini Vatican. Hatua hii ni kadiri ya Katiba ya Sinodi, ili kuhakikisha kwamba, maamuzi yake yanaingizwa na kumwilishwa katika maisha ya Makanisa mahalia na hatimaye, kwenye Kanisa zima. Lengo ni kuendelea kuimarisha mchakato uliokwisha kufikiwa hadi wakati huu na wala hakuna nia ya kuitisha tena Sinodi nyingine.

Mchakato wa usindikizaji, tathmini na umwilishaji wa maamuzi ya Sinodi
Mchakato wa usindikizaji, tathmini na umwilishaji wa maamuzi ya Sinodi   (Vatican Media)

Ni katika muktadha wa utekelezaji wa mchakato wa usindikizaji, tathmini na umwilishaji wa maamuzi yaliyotolewa kwenye maadhimisho ya Sinodi ya XVI ya Maaskofu, Baraza la Maaskofu Katoliki Italia, CEI kuanzia tarehe 31 Machi hadi tarehe 4 Aprili 2025 linaadhimisha Mkutano wa Pili wa Sinodi ya Makanisa nchini Italia, kama sehemu ya tathmini ya safari ya shughuli za kichungaji na kijamii iliyotekelezwa katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, tayari kutoa nafasi kwa Roho Mtakatifu katika mchakato wa kuliingiza Kanisa katika utimilifu wa ukweli wote. Rej Yn 16:13. Hulifanya kuwa moja katika ushirika na huduma, na kulifadhili vipawa mbalimbali vya kihierarkia na vya kikarama ambavyo kwavyo huliongoza na kuipamba kwa matunda yake. Rej Ede 4:11-12; IKor 12: 4; Gal 5:22. Kwa nguvu ya Injili hulipyaisha tena Kanisa na kurejea katika ujana wake na hivyo kukusanywa katika Fumbo la Utatu Mtakatifu. Rej Lumen gentium, 4. Hii ni sehemu ya ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko kwa washiriki wa Mkutano wa Pili wa Sinodi wa Makanisa nchini Italia, kwa kuongozwa na kichwa cha Mapendekezo “Ili furaha iwe kamili” kwani furaha ya Kikristo daima ni shirikishi na kwamba, ni kwa ajili ya wengi kwani inamwilishwa katika medani mbalimbali za maisha ya mwanadamu na kwa kuwashirikisha wengine na hivyo kuambata mtindo wa ukarimu.

Maadhimisho ya ya Mkutano wa Pili wa Sinodi ya Makanisa Italia
Maadhimisho ya ya Mkutano wa Pili wa Sinodi ya Makanisa Italia   (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Waamini wanapaswa kukumbuka daima kwamba, hii ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu; ni furaha inayokumbatia Fumbo la Msalaba na kwamba, Kristo Yesu ndiye anayewaongoza waja wake katika hija ya maisha yao. Baba Mtakatifu Francisko anakiri kwamba, wakati amelazwa kwenye Hospitali ya Chuo Kikuu cha Agostino Gemelli iliyoko mjini Roma tangu Ijumaa tarehe 14 Februari 2025 hadi tarehe 23 Machi 2025 aliporejea tena mjini Vatican na hata wakati huu anapoendelea na matibabu ameonja uwepo angavu na endelevu wa Kristo Yesu katika maisha yake. Furaha ya Kikristo ni kumtegemea Mwenyezi Mungu katika kila hali ya maisha. Wajumbe wa Mkutano wa Pili wa Sinodi ya Makanisa nchini Italia wamepata fursa ya kuzama zaidi katika maadhimisho ya Sinodi na hatimaye, watapigia kura mapendekezo kwa ajili ya mustakabali wa maisha na utume wa Makanisa nchini Italia. Baba Mtakatifu anawaalika wajumbe wa Mkutano huu, kutoa fursa kwa Roho Mtakatifu anayewakirimia kipaji cha ubunifu, ili aweze kuwaongoza, kwa kuwawezesha watu watakatifu waaminifu wa Mungu kutembea katika historia huku wakiwa wameangazwa na Neno la Mungu pamoja na Roho Mtakatifu. Baba Mtakatifu anawataka wajumbe wote kusonga mbele kwa furaha na hekima.

Mkutano wa Pili wa Sinodi ya Makanisa Nchini Italia 2025
Mkutano wa Pili wa Sinodi ya Makanisa Nchini Italia 2025   (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican Jumanne tarehe Mosi Aprili 2025 ameongoza Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya wajumbe wa Mkutano wa Pili wa Sinodi ya Makanisa nchini Italia, kwa kumwomba Roho Mtakatifu ili aweze kuwaongoza wajumbe katika maadhimisho ya Mkutano wa Pili wa Sinodi ya Makanisa nchini Italia. Imekuwa ni fursa kwa wajumbe kumwomba Roho Mtakatifu ili aweze kuwaponya walimwengu na magonjwa yanayowasumbua tayari kusimama tena na kusonga mbele kwa ari na moyo mkuu, huku wakiongozwa na Kristo Yesu aliye njia, ukweli na uzima, tayari kushiriki kikamilifu katika maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo yanayonogeshwa na kauli mbiu: “Peregrinantes in spem” yaani “Mahujaji wa matumaini.” Matumaini ya waamini yako katika Msalaba, yaani katika Kristo Yesu, chemchemi ya wokovu wa mwanadamu. Kristo Yesu ni mlango wa huruma na faraja, wema na uzuri usiokuwa na kifani. Huu ndio mlango wanamopita watu wenye haki. Kristo Yesu ni mlango wa mbingu, unaowaalika wote kushiriki furaha ya uzima wa milele. Yesu anawasubiri kwa moyo wa huruma na mapendo, wale wote wanaomwendea kwa toba na wongofu wa ndani. Wajumbe wa Mkutano wa Pili wa Sinodi ya Makanisa nchini Italia wamepita kwenye Lango la Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican.

Kristo Yesu anapaswa kuwa ni kiini cha ujenzi wa Kanisa la Kisinodi
Kristo Yesu anapaswa kuwa ni kiini cha ujenzi wa Kanisa la Kisinodi   (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Huu ni mkutano unaopania pamoja na mambo mengine, kutoa dira na mwongozo wa shughuli za kichungaji katika kipindi cha miaka mitano yaani kuanzia mwaka 2025 hadi mwaka 2030, ili kutangaza na kushuhudia imani kwa Kristo Yesu, aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu. Hii ni changamoto ya kuhakikisha kwamba, kunakuwepo na maandalizi ya kina kwa ajili ya waamini kupokea Sakramenti za kuingizwa katika Ukristo yaani: Ubatizo, Kipaimara na Ekaristi Takatifu zinazoweka misingi ya maisha yote ya Kikristo na hivyo kuwawezesha waamini kushiriki hali ya Kimungu wanayopata waamini kwa njia ya neema ya Kristo Yesu na ongezeko la utajiri wa uzima wa Kimungu na hivyo kuendelea hadi kufikia ukamilifu wa upendo. Rej KKK 1212. Lengo ni kuendeleza mchakato wa ujenzi wa Kanisa la Kisinodi na Kimisionari likiwa limekita mizizi yake kwa Kristo Yesu.

Kardinali Parolin ameongoza Ibada ya Misa kwa wajumbe
Kardinali Parolin ameongoza Ibada ya Misa kwa wajumbe   (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Kwa upande wake, Kardinali Matteo Maria Zuppi, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Italia, CEI katika hotuba yake ya ufunguzi amekazia umuhimu wa waamini kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili katika medani mbalimbali za maisha, kwa kujikita katika Heri za Mlimani, muhtasari wa mafundisho makuu ya Kristo Yesu kwa wafuasi wake, tayari kujenga Kanisa la Kisinodi na Kimisionari, kwa kujenga na kudumisha utamaduni wa kujadiliana na kusikilizana. Furaha ya Kanisa la Kisinodi ni kwa ajili ya watu wote wa Mungu sanjari na kudumisha majadiliano katika ukweli na uwazi; amani na utulivu wa ndani na walimwengu. Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wanasema, uchungu na fadhaa ya wanadamu wa nyakati zetu, hasa ya maskini na ya wale wote wanaoteswa, yote ni furaha na matumaini, uchungu na fadhaa ya wafuasi wa Kristo pia. Rej. LG 1. Kumbe Kanisa nchini Italia halina budi kutekeleza wito na wajibu wake wa Kinabii unaobubujika kutoka katika Neno la Mungu, ili kujenga mshikamano wa udugu wa kibinadamu kwani matumaini hayana ukomo!

Kardinali Matteo Maria Zuppi, Rais wa CEI ametoa hotuba ya ufunguzi
Kardinali Matteo Maria Zuppi, Rais wa CEI ametoa hotuba ya ufunguzi   (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Naye  Askofu mkuu Erio Castellucci, Rais wa Kamati ya Safari ya Kisinodi, Baraza la Maaskofu Katoliki Italia, CEI amekazia umuhimu wa wongofu wa kichungaji, tayari kujenga Kanisa la Kisinodi na Kimisionari na kwamba, Mkutano wa pili unapania kutoa mapendekezo ya utekelezaji wa maazimio ya Sinodi ya XVI ya Maaskofu kwa ushiriki mkamilifu wa watu watakatifu wa Mungu, kwa njia ya utambuzi wa imani “Sensus fidei” kwani Taifa takatifu la Mungu laishiriki pia kazi ya unabii wa Kristo Yesu kwa njia ya ushuhuda wa maisha ya imani, upendo, sadaka, dhabihu za sifa sanjari na ungamo la imani kutoka kwa watu wa Mungu. Rej. LG 12. Wote wanaalikwa kuwa ni mashuhuda wa umoja wa Kanisa kwa njia ya karama na huduma ya kitume. Mkutano huu pia utaanda “Hati ya Kutendea Kazi; yaani “Instrumentum laboris” kwa kuendelea kuzama katika utamaduni wa amani.

Wajumbe wa Sinodi watapembua vipaumbele vya Kanisa Italia
Wajumbe wa Sinodi watapembua vipaumbele vya Kanisa Italia   (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Kwa upande wake Lucia Capuzzi, Mjumbe wa Kamati ya Safari ya Kisinodi, Baraza la Maaskofu Katoliki Italia, CEI amekazia umuhimu wa safari ya ujenzi wa Kanisa la Kisinodi na Kimisionari, fursa, changamoto na matatizo ambayo wamekumbana nayo katika hija hii ya wongofu wa shughuli za kichungaji na kikanisa! Lakini, waamini wanahamasishwa kuwa ni Mitume wamisionari na mashuhuda wa Fumbo la Pasaka. Huu ni mwaliko kwa Kanisa kuendelea kujikita katika ujenzi wa utamaduni wa kumsikiliza Roho Mtakatifu, tayari kushiriki kikamilifu katika maadhimisho ya Sakramenti za Kanisa, ili kujenga familia moja ya watu wa Mungu. Hili ni Kanisa la Kiinjili linalosimikwa katika upendo na ukarimu, tayari kusikiliza na kujibu kilio cha Maskini na Dunia Mama; kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa maskini wa hali na kipato; ili kulinda na kudumisha: utu, heshima, haki msingi sanjari na utunzaji wa mazingira nyumba ya wote. Huu ni mwaliko kwa watu wa Mungu nchini Italia, kupyaisha maisha na utume wa Kanisa kama sehemu muhimu ya hija ya matumaini.

Sinodi Italia
01 Aprili 2025, 14:03
Prev
April 2025
SuMoTuWeThFrSa
  12345
6789101112
13141516171819
20212223242526
27282930   
Next
May 2025
SuMoTuWeThFrSa
    123
45678910
11121314151617
18192021222324
25262728293031