Mapadre andaeni mahubiri yanayogusa sakafu za mioyo ya waamini!
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko katika Wosia wake wa kitume “Evangelii gaudium” yaani “Furaha ya Injili” anakazia mchakato wa uinjilishaji mpya unaojikita katika ushuhuda wa imani, inayotangazwa na kumwilishwa katika matendo kwa kutambua kwamba, hii ni dhamana na wajibu wa waamini wote. Kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo, wakristo wote wanashiriki: ukuhani, ufalme na unabii wa Kristo Yesu, kumbe, wote ni wafuasi wamissionari wanaopaswa kushiriki kikamilifu katika matendo ya kiibada kama nguvu ya uinjilishaji. Waamini watumie karama na vipaji mbali mbali kwa ajili ya ujenzi wa umoja na mshikamano unaoinjilisha na kutamadunisha; kwa kuzingatia fikra na elimu makini!
Baba Mtakatifu anatoa kipaumbele cha pekee kwa mahubiri kama muktadha wa kiliturujia unaotoa nafasi kwa Mama Kanisa kuongea na watoto wake kutoka katika sakafu ya maisha na nyoyo zao. Kwa njia hii, mahubiri yanapaswa kuwasha moto wa imani, matumaini na mapendo kwa wale wanaosikiliza, ili hatimaye, waweze kuyamwilisha katika uhalisia wa maisha yao, kielelezo makini cha imani tendaji. Wakleri ambao wanashiriki kwa namna ya pekee kazi ya: kufundisha, kutakatifuza na kuwaongoza watu wa Mungu, wanapaswa kuandaa vyema mahubiri yao kwa kuzingatia heshima kwa ukweli wanaoutangaza na kuushuhudia; kwa kumwilisha Neno katika maisha yao, ili kuwa kweli ni vyombo na mashuhuda wa huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake.
Wakleri wajitahidi kuboresha mahubiri yao kwa kutumia nyenzo mbali mbali zilizowekwa na Mama Kanisa kama vile masomo ya maisha ya kiroho na tafakari kutoka kwa Mababa wa Kanisa. Wahubiri wawe makini kusoma alama za nyakati, ili mahubiri yao, yaweze kuwasaidia waamini, daima wakichota utajiri na amana ya Neno la Mungu, kama sehemu ya mchakato makini wa uinjilishaji mpya unaotumia hata vyombo vya mawasiliano ya jamii, kuhakikisha kwamba, cheche za Neno la Mungu zinawafikia watu wengi zaidi!
Kardinali Beniamino Stella, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa kwa ajili ya Wakleri anawataka Wakleri kujibidisha zaidi katika mchakato mzima wa mahubiri, ili kweli mahubiri yao yaweze kugusa sakafu ya nyoyo za waaamini wao kama anavyofanya Baba Mtakatifu Francisko kwa maneno na ujumbe rahisi, unaoingia na kugota katika sakafu ya maisha ya waamini! Papa Francisko anajipambanua kuwa kweli ni Padre na Katekista kwa ajili ya familia ya Mungu kwa nyakati hizi. Uzinduzi wa chombo cha “Clerus App” ni msaada mkubwa kwa wakleri kutafakari, kuandaa na kuhubiri Neno la Mungu kwa waamini wanaofika kushiriki katika adhimisho la Fumbo la Ekaristi Takatifu, chanzo na kilele cha maisha na utume wa Kanisa.
Kardinali Stella anakaza kusema, Baba Mtakatifu Francisko katika Wosia wake wa Kitume, “Furaha ya Injili” amekazia sana umuhimu wa mahubiri katika maadhimisho ya Mafumbo ya Kanisa kama sehemu ya uinjilishaji na katekesi. Baba Mtakatifu wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana, anatoa tafakari ya Injili ya Siku kwa muda wa dakika saba, kwa kuzingatia mambo msingi yanayofumbatwa katika Injili hiyo, changamoto na mwaliko kwa wakleri kuzingatia fursa na neema inayotolewa na Mama Kanisa katika maisha na utume wao, ili kuwalisha watu wa Mungu mkate wa Neno la Mungu. Baba Mtakatifu katika mahubiri yake, daima anapenda kukazia mambo makuu matatu, kielelezo cha mchungaji mwema anayeshuhudia kwamba kweli ni “Baba Paroko wa Ulimwengu mzima”. Waamini na watu wenye mapenzi mema, wanavutika sana kumsikiliza Baba Mtakatifu Francisko kwa sababu mahubiri na hotuba zake, zinagusa sakafu ya nyoyo za watu, kiasi hata cha kuwaacha wakiwa wamepigwa na bumbuwazi!
Kimsingi, mahubiri yanapaswa kuwa ni ushuhuda wa imani inayomwilishwa katika matendo! Watu wanavutwa zaidi na matendo, kuliko hata maneno yanayohubiriwa kwenye mimbari! Kumbe, kuna haja kwa wakleri kuhakikisha kwamba, wanakuwa ni mashuhuda wa mahubiri yao yanayomwilishwa katika maisha na utume wao kama Mapadre. Kardinali Beniamino Stella, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa kwa ajili ya Wakleri anapenda kuchukua fursa hii, kuwahimiza walezi wa seminarini na kwenye nyumba za malezi ya kitawa kuhakikisha kwamba, tangu mwanzo wana waandaa Majandokasisi ili waweze kuwa ni wahubiri mahiri, daima wakichota utajiri wa Neno la Mungu ambalo wanapaswa kulisoma, kulitafakari na kulimwilisha.
Wakleri wajenge utamaduni wa kusali, ili cheche za Neno la Mungu ziweze kuwasha moto wa imani, mapendo na matumaini kwa wale wote wanaosikiliza mahubiri na tafakari za Neno la Mungu. Wakleri wawe na heshima kwa waamini wao na kwamba, mahubiri si wakati wa kuwarushia watu “madongo na kuwapiga vijembe”! Waheshimu na kuthamini muda wa waamini wao! Tafakari ya siku ni chakula cha maisha ya kiroho kwa ajili ya waamini. Wakleri wajenge utamaduni wa kujiandaa barabara kwa ajili ya mahubiri, kwa kutolea mifano hai ya maisha ya watu wake.
Wakleri wawe na uwezo wa kukumbuka na kuwakumbusha waamini wao mambo msingi ya imani na maisha, ili kweli mahubiri yao, yawe ni matofali yanayosaidia kujenga utakatifu wa maisha yao, kwa kuyamwilisha! Kardinali Stella, anawataka Wakleri kujaribu ushauri huu, ili waweze kuonja siri ya mafanikio katika mchakato wa ushuhuda unaomwilishwa katika maisha na utume wao kama Mapadre wanaotumwa kufundisha, kutakatifuza na kuwaongoza watu wa Mungu si tu kwa maneno, bali kwa njia ya ushuhuda wenye mvuto na mashiko!