Tafakari za Kipindi cha Kwaresima 2019: Kuabudu na Kusujudu!
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Padre Raniero Cantalamessa, Mhubiri wa Nyumba ya Kipapa anasema, tafakari za Kipindi cha Kwaresima kwa Mwaka 2019 zinaongozwa na kauli mbiu "In te ipsum redi" yaani “Ingia ndani mwako” mwaliko kwa waamini kuingia katika undani wa maisha yao, kwa kuondokana na mahangaiko na changamoto za maisha, ili hatimaye, kupata amani na utulivu wa ndani; kwa kugundua na kutambua uwepo endelevu wa Mungu katika undani wa maisha yao na Walatini wanasema "Coram Deo". Ukweli wa maisha umejikita katika undani wa mtu!
Padre Cantalamessa, katika tafakari ya nne ya Kipindi cha Kwaresima kwa Mwaka huu, Ijumaa, tarehe 5 Aprili 2019, amejikita katika tema ya “Kumwabudu Mungu” kama inavyofafanuliwa kwenye Maandiko Matakatifu, maana ya kuabudu inayofumbatwa katika ukimya wa ndani; pamoja na Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu. Anasema, Kanisa linaadhimisha kumbu kumbu ya miaka 800 tangu Mtakatifu Francisko wa Assisi alipokutana na kuzungumza na Sultan Al Malik al Kamil wa Misri. Ilikuwa ni fursa kwa Mtakatifu Francisko wa Assisi kushuhudia Ibada zilizoadhimishwa na waamini wa dini ya Kiislam na kusema kwamba, hakika Mwenyezi Mungu anapaswa kupewa sifa na shukrani kwa matendo makuu yanayofumbatwa katika Ibada za waamini wa dini ya Kiislam.
Hiki ni kielelezo cha majadiliano ya kidini na chachu ya maboresho ya maisha ya kiroho yanayopania kutajirishana, ili kuzima kiu ya uwepo endelevu wa Mungu katika maisha ya waja wake. Uelewa wa Mungu kadiri ya Mapokeo ya Kikristo ni kwamba, ni mwingi wa huruma na mapendo. Kristo Yesu alipokutana na Mwanamke Msamaria na kumwomba maji, alimwambia pia kwamba, saa inakuja, sasa ipo, ambayo waabuduo halisi watamwabudu Mwenyezi Mungu katika roho na kweli na kwamba, Mungu ni roho. Huu ndiyo mwongozo wa Ibada kwa Wakristo. Agano Jipya limekuza Ibada ya Kumwabudu Mwenyezi Mungu na kuipatia kipaumbele cha kwanza pale Yesu alipomwambia Ibilisi baada ya kumjaribu jangwani kwa kusema “Imeandikwa Msujudie Bwana Mungu wako, umwabudu yeye peke yake”.
Kanisa katika Mapokeo yake, lina aina tatu za Ibada ya Kuabudu: “Latria” ni Ibada ya kumwabudu na kumkiri Mungu kuwa ni Muumba na Mkombozi; Bwana na Msimamizi wa kila kitu kilichopo, ndiye peke yake anayepaswa kusujudiwa na kuabudiwa. “Dulia” ni ibada inayotolewa kwa heshima ya watakatifu na wafidiadini na “Hyperdulia” ni Ibada inayotolewa kwa heshima ya Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa. Kuabudu na kusujudu ni mwelekeo wa ndani kabisa wa maisha ya mwamini na kwamba, hii ndiyo imani ya Kanisa kwa Roho Mtakatifu anayeabudiwa na kutukuzwa pamoja na Baba na Mwana. Matendo ya nje yanayoonesha tendo la ibada na kusujudu ni kupiga magoti au kuinamisha kichwa! Waamini wanapaswa kupiga magoti mbele ya Ekaristi Takatifu.
Kumwabudu na kumsujudu Mungu kadiri ya Mtakatifu Angela wa Foligno, ni hali ya mtu kujikusanya na hatimaye, kujizamisha katika huruma na upendo wa Mungu usiokuwa na mipaka, Ibada ya kumwabudu Mungu inafikia kilele chake katika ukimya! Hapa ndipo milango ya fahamu inapodhibitiwa na kutoa nafasi kwa ajili ya kumwabudu Mwenyezi Mungu ambaye ni asili ya wema na utakatifu wote; ndiye anayepaswa kutukuzwa katika ukimya “Tibi silentium laus”. Kuabudu ni tendo la mwamini kumwinulia Mungu utenzi wa sifa na shukrani katika ukimya na kumwachia nafasi Mungu ili kweli aitwe Mungu na kuimbiwa na kundi la Malaika wake watakatifu!
Ibada ya kuabudu inakita mizizi yake katika utu na heshima ya binadamu anayetaka kumtolea Mungu sadaka na hatimaye, kupokea neema kutoka kwake. Kwa kuabudu na kusujudu, mwamini anajikuta mbele ya ukweli kwa kujikita katika kutenda haki pamoja na kujiaminisha mbele ya Mungu. Padre Cantalamessa anakaza kusema, kwa kuabudu na kusujudi, mwamini anapata amani na furaha ya ndani na kwamba, hii ni dhamana na wajibu ambao unapaswa kutekelezwa na waamini katika maisha yao. Binadamu anapaswa kupenda na kuabudu! Mama Kanisa anasali na kufundisha kwamba, Mwenyezi Mungu hana haja ya sifa za waamini wake, bali sifa hizi ni paji la Mungu wanalomrudishia kwa shukrani. Kwa maana sifa za binadamu hazimzidishii Mungu kitu, bali zinawafaa wanadamu kupata wokovu kwa njia ya Kristo Yesu. Tendo la Ibada linapaswa kufanya kwa uhuru kamili
Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu inachukua nafasi ya pekee katika maisha na utume wa Kanisa Katoliki. Waamini wa madhehebu mengine ya Kikristo wanatoa kipaumbele cha kwanza kwa Biblia Takatifu wakati Wakristo wa Kanisa la Kiorthodox wanajielekeza zaidi kwa Picha Takatifu. Hizi ni njia za kuweza kutafakari fumbo la maisha ya Kristo Yesu. Kanisa Katoliki linamwabudu Kristo Yesu katika maumbo ya Mkate na Divai, kwa sababu hii ni Sakramenti ya sadaka, shukrani, kumbukumbu na uwepo! Waamini wamejichotea neema na baraka katika hija ya maisha yao hapa duniani kwa njia ya Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu!
Wakatoliki bado wanahamasishwa kukaa mbele ya Ekaristi Takatifu kwa ibada na uchaji; katika hali ya ukimya na sala, ili kumtafakari Kristo Yesu, Jua la haki, anayewaangazia waja wake neema za mbinguni!Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu ni sehemu muhimu sana ya uinjilishaji mpya inayofumbatwa katika ushuhuda wa imani tendaji! Kuna maelfu ya waamini ambao wanakesha kuabudu Ekaristi Takatifu. Hawa ni wale waamini ambao wameitikia wito wa kukaa na kukesha pamoja na Kristo Yesu katika mateso yake! Ibada hii ni chemchemi ya furaha na utulivu wa ndani! Padre Cantalamessa anawaalika wajumbe wa vyama mbali mbali vya kitume kuchota ari na nguvu mpya katika Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu pamoja na ushiriki mkamilifu wa maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu. Na huu ndio mwanzo wa Chama cha Uhamsho wa Kikatoliki, takriba ni miaka 50 iliyopita!