TAHARIRI: Papa Francisko aomba msamaha kwa Warom & Wasint!
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko wakati anahitimisha hija yake ya kitume nchini Romania, Jumapili, tarehe 2 Juni 2019, alipata nafasi ya kutembelea na kuzungumza na Jumuiya ya Warom na Wasint, watu wasiokuwa na makazi maalum nchini Romania. Baba Mtakatifu amekaza kusema, Kanisa ni mahali pa watu kukutana; Utu na heshima ya binadamu ivunjilie mbali maamuzi mbele na ubaguzi; wananchi wadumishe mchakato wa upatanisho, haki na amani na wala si kulipizana kisasi na kwamba, wananchi waoneshe ujasiri wa kutembea kwa pamoja!
Kanisa ni mahali pa watu kukutana kama utambulisho wake wa Kikristo, kama walivyoshuhudia wenyeheri wapya waliotangazwa, Jumapili iliyopita! Andrea Tornielli, Mhariri Mkuu wa Baraza la Kipapa la Mawasiliano katika tahariri yake anakaza kusema, Baba Mtakatifu ametumia fursa hii kuomba msamaha kwa dhambi za ubaguzi ambazo zimetendwa hata na watoto wa Kanisa. Kunako mwaka 1965 Mtakatifu Paulo VI aliomba msamaha kwa ubaguzi waliokuwa wanafanyiwa Warom na Wasint na kuwakumbusha kwamba, wao ni sehemu muhimu sana ya maisha na utume wa Kanisa. Katika historia, jamii hii ya watu imekumbana na dhuluma na ubaguzi; akaomba msamaha pia kwa madhulumu ambayo Kanisa Katoliki liliwatendea waamini wa Makanisa na Madhehebu mengine ya Kikristo.
Mtakatifu Yohane Paulo II katika maadhimisho ya Jubilei kuu ya Miaka 2000 ya Ukristo, aliadhimisha Ibada ya toba na kuomba msamaha kutokana na kiburi kilichopelekea, chuki na uhasama na uadui dhidi wahamiaji na wakimbizi kama Jumuiya ya Warom na Wasint. Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI kunako tarehe 11 Juni 2011, akizungumza na wawakilishi wa Jumuiya ya Warom na Wasint kutoka sehemu mbali mbali za dunia, alikiri kwamba, hii ni Jumuiya ambayo imekumbana na dhuluma, nyanyaso na ubaguzi. Kamwe dhamiri nyofu haiwezi kusahau matukio kama haya! Umefika wakati wa kusema, ni marufuku Warom na Wasint kuwa ni watu wa kubaguliwa, kudharauliwa na kutwezwa kwani hawa ni watu wenye utu, heshima na haki zao msingi zinazopaswa kuendelezwa na kudumishwa!
Baba Mtakatifu Francisko kunako mwaka 2015 aliomba msamaha kwa Wahindi Wekundu huko Chapas na Mwaka 2018, akaomba msamaha kwa kashfa ya nyanyaso za kijinsia iliyotendwa na baadhi ya viongozi wa Kanisa. Baba Mtakatifu alisikitika kusema kwamba, pengine, Kanisa lilichelewa kufikiri, kuamua na kutenda kwa haraka kwa kutotambua uzito wa kashfa hii katika maisha na utume wa Kanisa. Mtakatifu Yohane Paulo II kwa kufuata nyayo za Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican na za Mtakatifu Paulo IV aliomba msamaha hadharani hali ambayo ilisababisha mashambulizi kutoka ndani ya Kanisa. Mtakatifu Yohane Paulo II aliomba msamaha kutokana na Vita vya kidini, mipasuko na utengano ndani ya Makanisa; nyanyaso na dhuluma dhidi ya wanawake pamoja na hukumu ya Kanisa dhidi ya Galileo; mauaji ya kikatili dhidi ya Wayahudi pamoja na ukoloni Barani Afrika.
Andrea Tornielli anakiri kwamba, kwa Wakristo kuomba na kutoa msamaha ni jambo la kawaida, hata kama kosa bado linaendelea kubaki kwa mtu binafsi. Mama Kanisa kwa nyakati mbali mbali ameendelea kuwa mwaminifu kwa dhamana na utume wake wa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu hadi miisho ya dunia, kwa kutambua pia makosa na dhambi zilizotendwa na watoto wake katika historia. Kuomba msamaha, ni mwanzo wa hija mpya ya maisha. Kristo Yesu katika maisha na utume wake, ameonesha mshikamano na maskini, walioteseka na kudhulumiwa katika maisha yao! Alithubutu, wakati akiwa Bustanini Gethsemane, pale Mtakatifu Petro alipotwaa upanga akamkata sikio mtumwa wa Kuhani mkuu, lakini Yesu akamwambia, rudisha upanga alani mwake!