Tafuta

Kardinali Fridolin Ambongo Besungu asema Bonde la Mto Congo linakabiliwa pia na changamoto za kiekolojia zinazotishia usalama na maisha ya watu wa Mungu Ukanda huu. Kardinali Fridolin Ambongo Besungu asema Bonde la Mto Congo linakabiliwa pia na changamoto za kiekolojia zinazotishia usalama na maisha ya watu wa Mungu Ukanda huu. 

Kardinali Besungu kutoka DRC: Bonde la Mto Congo! Ekolojia!

Kardinali Fridolin Ambongo Besungu, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Kinshasa, DRC., katika mahojiano maalum na Vatican News anasema, changamoto za uchafuzi na uharibifu wa mazingira zinazoendelea kujitokeza Ukanda wa Amazoni zinakaribiana sana na zile zilizoko kwenye Bonde la Mto Congo. Mto Congo una urefu wa km 4,700 sawa na maili 2,920. Ekolijia fungamani!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia kuanzia tarehe 6-27 Oktoba, 2019 yanaongozwa na Kauli mbiu: “Amazonia: njia mpya ya Kanisa na kwa ajili ekolojia fungamani”. Lengo la Sinodi hii ni kubainisha njia mpya za uinjilishaji Ukanda wa Amazonia, kwa kusikiliza na kujibu kwa ufasaha kilio cha Dunia Mama na kilio cha maskini; kwa kupembua matatizo, changamoto na fursa zilizopo ili kutoa mapendekezo yatakayofanyiwa kazi na Khalifa wa Mtakatifu Petro kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu Ukanda wa Amazonia. Hii ni changamoto kubwa katika maisha na utume wa Kanisa. Kumbe, Kanisa linawajibika kuziinjilisha tamaduni ili kuitamadunisha Injili; kwa kusimama kidete ili kukazia ekolojia fungamani. Sinodi hii ambayo kwa sasa inaelekea ukingoni imezingatia mambo makuu manne: Shughuli za Kichungaji, Kitamaduni, Kisiasa na Kiekolojia; mambo yanayo ambatana na kukamilishana kama sehemu ya mchakato wa uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili.

Katika maadhimisho ya Sinodi hii, Bara la Afrika limewakilishwa na viongozi wafuatao: Kardinali Fridolin Ambongo Besungu, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Kinshasa, DRC; Askofu mkuu Marcel Madila Basanguka, wa Jimbo kuu la Kananga, nchini Congo Brazzaville  na ambaye pia ni Rais wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Afrika ya Kati, A.C.E.A.C. Wengine ni Padre Martín Lasarte Topolanski, S.D.B., kutoka Angola; Sr. Mary Agnes Njeri Mwangi wa Shirika la Masista wa Consolata pamoja na Padre Rigobert Minani, S.I., kutoka DRC., Mratibu wa “Réseu Ecclesial du Bassin du Congo” [REBAC]. Kardinali Fridolin Ambongo Besungu, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Kinshasa, DRC., katika mahojiano maalum na Vatican News anasema, changamoto za uchafuzi na uharibifu wa mazingira zinazoendelea kujitokeza Ukanda wa Amazoni zinakaribiana sana na zile zilizoko kwenye Bonde la Mto Congo. Mto Congo ni mmojawapo wa mito mirefu zaidi duniani.

Itakumbukwa kwamba, Mto Congo una urefu wa km 4,700 sawa na maili 2,920 kutoka kwenye kitovu cha Bara Afrika hadi Bahari ya Atlantiki. Kina cha maji ya Mto Congo kimeshuka sana kutokana na uhaba wa mvua katika bonde la mto huo, lenye ukubwa wa kilomita za mraba milioni nne unaosababishwa na uchafuzi mkubwa wa mazingira nyumba ya wote. Hali hii pia imepelekea kupungua kwa uzalishaji wa umeme kutoka mitambo ya Inga, na hivyo kusababisha uzalishaji na usambazaji wa umeme mjini Kinshasa na miji mikubwa inayotegemea nishati ya umeme wa maji kutoka kwenye mto huo na kuanza kupata kwa njia ya mgao. Bonde la Mto Congo lina ukubwa wa ekari milioni 300 na huu ni msitu wa pili kwa ukubwa duniani na pia eneo ambalo linaongoza kwa kuwa na biashara haramu ya mbao inayogharimu Serikali ya Congo Brazzaville takribani dola za Kimarekani bilioni 10 kila mwaka. Kardinali Fridolin Ambongo Besungu anakaza kusema, uharibifu wa mazingira nyumba ya wote una madhara makubwa katika maisha na maendeleo ya watu wanaoishi kuzunguka Bonde la Mto Congo.

Ikumbukwe kwamba, watu wote wanawajibika katika utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Kumbe, sera na mikakati ya kiuchumi lazima izingatie ekolojia fungamani. Kama ilivyo kwenye Ukanda wa Amazonia, kuna haja pia kwa familia ya Mungu Bonde la Mto Congo kujizatiti zaidi katika mchakato wa uinjilishaji na utamadunisho; kwa kuamsha ari na mwamko wa kimisionari kwa ajili ya shughuli za kichungaji katika eneo hili. Huu ni mwaliko wa Kanisa kujielekeza zaidi katika mchakato mzima wa uinjilishaji unaoifunda mihimili mikuu ya uinjilishaji na utamadunisho ili kweli Injili iweze kugusa, kuganga na kutakasa maisha ya watu mahalia, ili nao wakiisha kuimarishwa katika imani, matumaini na mapendo, wao pia waweze kuwa ni mashuhuda na vyombo vya Injili ya: uhai, matumaini na huruma ya Mungu kwa watu wake kwenye Bonde la Mto Congo. Makatekista bado wanayo nafasi kubwa sana katika maisha na utume wa Kanisa Barani Afrika. Umefika wakati kwa waamini walei kujishikamanisha na Kanisa, ili kushiriki kikamilifu katika mchakato wa kuyatakatifuza malimwengu kwa njia ya ushuhuda wa imani inayomwilishwa katika matendo! Wanawake wengi wamekuwa kweli ni vyombo na mashuhuda wa ujenzi wa misingi ya haki, amani na upatanisho kati ya watu wa Mataifa.

Kwa upande wake, Kardinali Luis Francisco Ladaria Ferrer, S.J., Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa anakazia kwa namna ya pekee kabisa umisionari wa Kanisa sanjari na mchakato wa utamadunisho unaosimikwa kwenye Katekesi makini na endelevu; Sakramenti na Maadhimisho ya Mafumbo ya Kanisa; Maisha adili kama ushuhuda wa sala inayomwilishwa katika uhalisia wa maisha ya watu. Mchakato wa utamadunisho ni changamoto endelevu ya Kanisa Katoliki inayopaswa kuvaliwa njuga kwa kuzingatia mambo msingi ya imani ya Kanisa Katoliki pamoja na Mapokeo yake. Huu ni wakati wa Kanisa kuwekeza katika tunu msingi za kimaadili na utu wema, ili ulimwengu uweze kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi.

Bonde la Mto Congo
24 October 2019, 14:59