Mtakatifu Gaspari del Bufalo: Mtume hodari wa Damu ya Yesu!
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Mama Kanisa kila mwaka ifikapo tarehe 21 Oktoba, anaadhimisha Kumbu kumbu ya Mtakatifu Gaspari del Bufalo mfano bora wa uinjilishaji wa kina unaojikita katika ushuhuda na utakatifu wa maisha. Mtakatifu Gaspari ni mtume hodari wa Damu Azizi ya Yesu, chemchemi ya huruma, upendo na ukombozi wa mwanadamu. Katika maisha na utume wake, alibahatika kusimama kidete na kwa ujasiri mkubwa, akapambana na madhulumu dhidi ya Kanisa wakati wake, huku akiwa amejiaminisha na kujikabidhi chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa. Alikuwa ni mhubiri maarufu wa Neno la Mungu lililoacha chapa ya kudumu katika maisha ya wale wote waliolisikiliza. Mtakatifu Gaspari del Bufalo alijisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya kutangaza Habari Njema ya Wokovu, akawa na ujasiri wa kuweza kusikiliza na kujibu kilio cha maskini na wale wote waliokuwa wametengwa na jamii kutokana na kukengeuka na hatimaye kutopea katika dhambi. Kwa watu wote hawa, Gaspari akajipambua kwao kuwa ni ndugu, rafiki na mlinzi mwaminifu katika hija ya maisha!
Kardinali Gianfranco Ravasi, Rais wa Baraza la Kipapa la Utamaduni, Jumapili jioni tarehe 20 Oktoba kwenye Kanisa la “Santa Maria in Trivio” mjini Roma, Kanisa linalohifadhi masalia ya Mtakatifu Gaspari del Bufalo ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwa heshima ya Mtakatifu Gaspari del Bufalo, muasisi wa Shirika la Wamisionari wa Damu Azizi ya Yesu, C.PP.S. Katika mahubiri yake amekazia umuhimu wa waamini kadiri ya karama, nafasi na uwezo wao, kuwa ni vyombo na wajumbe wa Habari Njema ya Wokovu katika ulimwengu mamboleo. Pili amesema, Mtakatifu Gaspari del Bufalo ni alama na kielelezo cha sadaka ya maisha yaliyomiminwa katika tamaduni za watu mbali mbali duniani, ili kusikiliza na kujibu kilio cha “Damu ya Kristo” inayoendelea kumwagika sehemu mbali mbali za dunia kutokana na umaskini, magonjwa, dhuluma na nyanyaso. Kardinali Gianfranco Ravasi anasema, Kristo Yesu katika mahubiri yake alitaka kuwahubiria maskini Habari Njema, kuwatangazia wafungwa kufunguliwa kwao na vipofu kupata kuona tena, kuwaacha huru waliosetwa na kutangaza mwaka wa Bwana uliokuwa.
Waamini wanapaswa kuwa kweli ni wajumbe, vyombo na mashuhuda wa Injili ya matumaini, upendo na mshikamano wa dhati kwa wale waliokata tamaa kutokana na sababu mbali mbali za maisha. Injili ya Kristo Mfufuka iwe ni chemchemi ya furaha, imani na faraja. Isaidie kuamsha dhamiri, ili kujikita katika toba na wongofu wa ndani. Kimsingi; imani, matumaini na mapendo ni tunu msingi za Kiinjili zinazopaswa kumwilishwa katika uhalisia wa hija ya maisha ya waamini. Kardinali Gianfranco Ravasi anaendelea kufafanua kwamba, Mtakatifu Gaspari del Bufalo kwa kuanzisha Shirika la Wamisionari wa Damu Azizi ya Yesu, C.PP.S. alikuwa ni kielelezo makini cha kujibu kilio cha “Damu Azizi ya Kristo”, kinachoendelea kusikika sehemu mbali mbali za dunia kutokana na umaskini, magonjwa, njaa na upweke hasi unaowanyemelea watu wengi kwa sasa. Mtakatifu Gaspari akafanikiwa kuyamimina maisha yake katika tamaduni mbali mbali duniani, leo hii Wamisionari wa Damu Azizi ya Yesu wako mstari wa mbele katika kusikiliza na kujibu kilio cha damu ya watu wa Mungu.
Huu ni utakatifu unaojikita katika sala na Neno la Mungu linalomwilishwa katika uhalisia wa maisha. Leo hii kuna watu wanaoteseka kutokana na sababu mbali mbali; watu wanao ogelea katika upweke hasi; wote hawa wanahitaji mtu wa kusikiliza na kujibu kilio chao. Damu Azizi ya Kristo, iwe ni chemchemi ya: imani, faraja na matumaini kwa wale wote wanaoteseka sehemu mbali mbali za dunia! Mheshimiwa Padre Emanuele Lupi hivi karibuni amechaguliwa kuwa Mkuu wa Shirika la Wamisionari wa Damu Azizi ya Yesu Ulimwenguni. Wengine waliochaguliwa ni pamoja na Padre Angelo Anthony, C.PP.S. Makamu mkuu wa Shirika, Padre Augusto Menichelli, C.PP.S., Mshauri; Bro. Juan Acuña, C.PP.S., Mshauri; pamoja na Padre Alois Schlachter, C.PP.S., Mshauri ambaao wamechaguliwa hivi karibuni na wataliongoza Shirika la Wamisionari wa Damu Azizi ya Yesu kwa kipindi cha miaka sita! Padre katika maadhimisho ya Siku kuu ya Mtakatifu Gaspar del Bufalo kwa Mwaka 2019 anawataka Wanashirika kuwa ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya haki na amani dhidi ya utamaduni wa chuki, uhasama na kifo. Wamisionari wajifunge kibwebwe ili kutoka na kuwaendea maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, kama ilivyokuwa kwa Kristo Yesu, alifia mlimani Kalvari, nje ya malango ya Mji wa Yerusalemu.
Wamisionari wa Damu Azizi ya Yesu wawe ni vyombo na mashuhuda wa huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake kama ilivyokuwa kwa Mtakatifu Gaspari katika maisha na utume wake. Baba Mtakatifu Francisko analitaka Kanisa kuwa kama Hospitali katika uwanja wa vita, ili kuwaganga na kuwaponya wale waliovunjika na kupondeka moyo, watu wanaoelemewa na mizigo ya maisha. Kimsingi, Wamisionari wa Damu Azizi ya Yesu wawe ni chemchemi ya matumaini kwa wale waliokata tamaa. Watambue kwamba, wameitwa na kutumwa sehemu mbali mbali za dunia ili kutangaza na kushuhudia huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake. Maisha ya Mtakatifu Gaspari ni kielelezo cha maisha yaliyosimikwa katika huruma na upendo wa Mungu unaojionesha kwa namna ya pekee kwa Kristo Yesu kumwaga Damu yake Azizi kwa ajili ya kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti. Maadhimisho ya Kumbu kumbu ya Mtakatifu Gaspari del Bufalo ni muda wa kumshukuru Mungu kwa zawadi ya utakatifu na ujasiri wa Padre Gaspari del Bufalo. Ikumbukwe kwamba, utakatifu wa maisha ni wto kwa kila mwamini; wito unaopaswa kumwilishwa katika uhalisia wa maisha ya kila mtu. Mtakatifu Gaspari anawahimiza wamisionari wake kuwa ni chemchemi ya utakatifu kama ushuhuda na utambulisho wao, changamoto inayopaswa kuvaliwa njuga, kila siku ya maisha!