Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia: Muswada wa Hati ya Sinodi
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia kuanzia tarehe 6-27 Oktoba, 2019 yanaongozwa na Kauli mbiu: “Amazonia: njia mpya ya Kanisa na kwa ajili ekolojia fungamani”. Lengo la Sinodi hii ni kubainisha njia mpya za uinjilishaji Ukanda wa Amazonia, kwa kusikiliza na kujibu kwa ufasaha kilio cha Dunia Mama na kilio cha maskini; kwa kupembua matatizo, changamoto na fursa zilizopo ili kutoa mapendekezo yatakayofanyiwa kazi na Khalifa wa Mtakatifu Petro. Kwa muhtasari haya ndiyo mawazo makuu yaliyowasilishwa na Mababa wa Sinodi katika tafakari, majadiliano na mang’amuzi yaliyoibuliwa kwenye majadiliano ya vikundi vidogo vidogo, “Circoli Minori” kwa uwepo na ushiriki wa Baba wa Mtakatifu Francisko. Mababa wa Sinodi wameonesha matumaini makubwa katika mchakato wa maendeleo fungamani Ukanda wa Amazonia kwa kuzingatia njia mpya ya Kanisa kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu huko Amazonia.
Nguzo msingi ya matumaini haya ni ari na mwamko mpya wa kimisionari unaolitaka Kanisa kutoka kifua mbele ili kutangaza na kushuhudia tunu msingi za Kiinjili, ili kuwajengea watu wa Mungu mazingira bora zaidi ya kuishi. Mababa wa Sinodi wameanza kuandaa muswada wa Hati ya Mababa wa Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia. Hati hii ni muhtasari wa mchango uliowasilishwa na Mababa wa Sinodi na kwa sasa kwa njia ya Vikao vya vikundi vidogo vidogo, mawazo haya yanapatiwa, yanahaririwa na kutolewa muhtasari. Hati hii pamoja na mambo mengine, itakuwa ni mkusanyo wa hotuba elekezi iliyotolewa na Katibu mkuu wa Sinodi za Maaskofu pamoja na zile za Makatibu maalum wa Sinodi. Kazi hii inatekelezwa kwa msaada wa wataalamu; itapitiwa na kuangaliwa tena na Kamati iliyoundwa ili kuhariri Hati hii na baadaye, itasomwa mbele ya Mababa wa Sinodi na hatimaye, Jumamosi jioni, kila kipengele kitapigiwa kura.
Askofu mkuu Miguel Cabrejos Vidarte wa Jimbo kuu la Trujillo ambaye pia ni Rais wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Amerika ya Kusini na Caribbean CELAM, katika mahubiri yake kabla ya kuanza kikao cha 14, Siku ya Jumatatu, tarehe 21 Oktoba 2019 amegusia wimbo wa Mtakatifu Francisko wa Assisi unaochota utajiri wake kutoka katika Maandiko Matakatifu kwa kukazia: uzuri na utakatifu wa kazi ya uumbaji; umuhimu wa ujenzi wa udugu wa kibinadamu kama njia ya kumwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa, utukufu na shukrani. Huu ni utajiri mkubwa unaobubujika kutoka katika tasaufi ya maisha ya Mtakatifu Francisko wa Assisi kwa ajili ya kulinda na kutunza mazingira nyumba ya wote. Askofu mkuu Miguel Cabrejos Vidarte amewataka Mababa wa Sinodi kwanza kabisa, kutambua ustawi na mafao ya wengi; hatua ya pili ni kurejesha mafao haya kwa wahusika kama kielelezo cha shukrani kwa Mwenyezi Mungu.
Hii inatokana na ukweli kwamba, dhambi imeacha madhara makubwa katika maisha ya mwanadamu na matokeo yake mwanadamu pia amekuwa ni mharibifu wa mazingira nyumba ya wote. Mwenyezi Mungu ambaye ni Baba wa vyote vilivyo hai, vinavyoonekana na visivyoonekana, anapaswa kupewa sifa, ukuu na utukufu, kwa kujikita katika mchakato wa utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Mtakatifu Francisko wa Assisi katika safari ya maisha yake ya kiroho, alimtambua Mwenyezi Mungu kuwa ndiye asili na hatima ya kazi ya uumbaji. Kumbe, mwanadamu anawajibika kumrudishi sifa, heshima na utukufu kwa kuendelea kulinda, kutunza na kuboresha mazingira ili yawe ni mahali pazuri zaidi pa watu wa Mungu kuweza kuishi. Ndio maana Mama Kanisa anawataka watu wa Mungu kujikita katika wongofu wa kiekolojia ili kujenga na kudumisha ekolojia fungamani kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu dhidi ya uharibifu wa mazingira nyumba ya wote ambao umekuwa ni chanzo cha maafa makubwa kwa watu na mali zao.