Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia: Wongofu na matumaini!
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia kuanzia tarehe 6 - 27 Oktoba, 2019 yameongozwa na Kauli mbiu: “Amazonia: njia mpya ya Kanisa na kwa ajili ekolojia fungamani”. Baba Mtakatifu Francisko, Jumapili tarehe 27 Oktoba 2019 amefunga rasmi maadhimisho kwa Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican kwa kuwataka watu wa Mungu kusikiliza na kujibu kilio cha maskini na Dunia Mama na hivyo kuanza kujikita katika mchakato wa wongofu kwa ajili ya maendeleo fungamani ya binadamu kama sehemu ya ushuhuda wa Injili ya matumaini kwa watu wa Mungu Ukanda wa Amazonia. Mababa wa Sinodi wamepitia, wakajadili na hatimaye, wakapigia kura vipengele vyote na kupitisha Hati ya Maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia kwa Mwaka 2019. Hati hii inaongozwa na kauli mbiu “Amazonia: njia mpya ya Kanisa na kwa ajili ya ekolojia fungamani”.
Hati ina jula ya kurasa 30 zenye sura tano pamoja na utangulizi unaobainisha hija ya maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia. Hatua ya kwanza ni kusikiliza na kuanza mchakato wa wongofu fungamani unaosikiliza na kujibu kwa makini kilio cha maskini wa Ukanda wa Amazonia pamoja na kilio cha Dunia Mama! Njia mpya za wongofu wa kichungaji zinalitaka Kanisa kujielekeza zaidi katika kukuza na kudumisha ari na mwamko wa kimisionari kwa kutambua kwamba, linapaswa kuwa ni kielelezo cha Msamaria mwema, chombo na huruma ya Mungu kinachokita maisha na utume wake katika mshikamano. Wongofu wa kichungaji unajielekeza zaidi katika majadiliano ya kidini, kiekumene na kitamaduni. Lengo ni kusikiliza na hatimaye, kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu inayokita mizizi yake katika uhalisia wa maisha ya watu mahalia!
Mababa wa Sinodi wanasema wongofu wa kitamaduni unapania kuziinjilisha tamaduni ili kuitamadunisha Injili; kwa kusimama kidete katika wongofu wa kitamaduni unaothamini tamaduni, mila na desturi njema za watu wa Mungu Ukanda wa Amazonia. Dhumuni kubwa ni kusimama kidete ili kulinda: utu, heshima na haki msingi za binadamu. Utamadunisho ni sehemu ya mchakato wa umwilisho wa tunu msingi za Kiinjili katika uhalisia wa maisha ya watu. Njia Mpya za Wongofu wa Kiekolojia ni kuwawezesha watu wa Mungu Ukanda wa Amazonia kupata utimilifu wa maisha kwa kusimama kidete kulinda, kutetea na kutunza mazingira nyumba ya wote. Kusikiliza na kujibu kilio cha Dunia Mama pamoja na Maskini wa Ukanda wa Amazonia ni sehemu ya mchakato wa uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Kanisa liko kwa ajili pamoja na maskini.
Njia Mpya za Wongofu wa Kisinodi, ni kutaka kujenga na kudumisha umoja unaofumbatwa katika dhana ya Sinodi, kama sehemu ya mchakato wa maisha na utume wa Kanisa. Mababa wa Sinodi wanawahimiza wakleri, watawa na waamini walei kushiriki kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa. Dhamana na nafasi ya wanawake, Mashemasi wa kudumu, malezi na majiundo ya wakleri na watawa pamoja na maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu ni changamoto kubwa katika Ukanda wa Amazonia. Mababa wa Sinodi wanaliomba Kanisa kutoa kibali cha kuwapatia Daraja Takatifu ya Upadre Mashemasi wa Kudumu walioshuhudia vyema wito na utume wao, ili kusaidia mchakato wa maadhimisho ya Mafumbo ya Kanisa Ukanda wa Amazonia.
Kardinali Michael Czerny, Katibu mkuu msaidizi, Idara ya Wahamiaji na Wakimbizi, Baraza ya Kipapa la Huduma ya Maendeleo Endelevu na Fungamani ya Binadamu, Askofu David Martìnez De Aguirre Guinea, wa Jimbo Katoliki la Puerto Maldonado, Perù, Dr. Paolo Ruffini, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Mawasiliano pamoja na Padre Giacomo Costa, S.I., Katibu wa Tume ya Mawasiliano ndio viongozi waliowasilisha mchakato mzima wa Hati ya Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia mwaka 2019. Dr. Matteo Bruni Msemaji mkuu wa Vatican ndiye aliyeratibu tukio la kuwasilisha Hati ya Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia Mwaka 2019 kwa wadau wa tasnia ya mawasiliano ya jamii mjini Vatican, Jumamosi, tarehe 26 Oktoba 2019.
Dr. Bruni anasema, hati hii ni muhtasari wa tafakari, mawazo na mang’amuzi ya Mababa wa Sinodi yanayokita mizizi yake katika utajiri wa maisha na utume wa Kanisa, Mapokeo na Mamlaka Funzi ya Kanisa. Ni Hati ambayo imesikiliza kwa makini na kujibu kilio cha watu wa Mungu Ukanda wa Amazonia. Hati pamoja na mambo mengine, inapembua kwa kina na mapana kuhusu hali ya halisi ya Ukanda wa Amazonia: kichungaji, kitamaduni, kisiasa na kiekolojia. Hati hii inaihusu familia ya Mungu katika ujumla wake. Baba Mtakatifu Francisko amewapongeza na kuwashukuru wadau wote wa tasnia ya mawasiliano ya jamii kwa mchango wao katika kuwafikishia watu wa Mungu yale mambo msingi yaliyokuwa yanajadiliwa wakati wa maadhimisho ya Sinodi.
Kwa upande wake, Dr. Paolo Ruffini amesema Hati hii ni sehemu ya mchakato wa Kanisa linalotembea kwa pamoja, ili kusoma alama za nyakati na kujibu kilio cha maskini Ukanda wa Amazonia, na kilio cha Dunia Mama, kwa kuonesha upendo kwa Mungu na jirani. Dr. Ruffini amewaangalisha wadau wa tasnia ya mawasiliano ya jamii kuwa makini zaidi, kwa sababu wanaweza kudhani kwamba, wanampenda na kumwamini Mungu, lakini katika ukweli wa mambo wako kinyume chake. Umefika wakati kwa wadau wa mawasiliano kujikita katika ukweli kwa kusoma alama za nyakati, mambo msingi yaliyozingatiwa wakati wa maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia.
Wakati huo huo, Padre Giacomo Costa, S.I., Katibu wa Tume ya Mawasiliano katika maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia amekazia zaidi mchakato wa Kanisa kutembea kwa pamoja na umuhimu wa dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa. Huu ni mchakato unaoliwezesha Kanisa: Kusikiliza, kutafakari, kung’amua na kutenda kwa umoja na mshikamano ili kukabiliana na changamoto, matatizo na fursa zilizopo Ukanda wa Amazonia. Utekelezaji wa Waraka wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko “Laudato si” yaani “Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote” ni sehemu ya mbinu mkakati wa utunzaji bora wa mazingira na kwamba, Jumuiya ya Kimataifa inapaswa kusikiliza na kujibu sauti ya vijana wanaotaka kuona sera na mikakati ya utunzaji bora wa mazingira. Mababa wa Sinodi wamewasha moto wa Injili Ukanda wa Amazonia, ili kusimama kidete, kulinda, kutetea na kudumisha Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo. Matunda ya Sinodi ni furaha kwa watu wa Mungu Ukanda wa Amazonia.
Naye Askofu David Martìnez De Aguirre Guinea, wa Jimbo Katoliki la Puerto Maldonado lililoko nchini Perù, amegusia changamoto, matatizo na fursa zilizoko Ukanda wa Amazonia kama sehemu ya mchakato wa utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Maisha na utume wa Kanisa Ukanda wa Amazonia unasimikwa katika mchakato wa uinjilishaji na utamadunisho sanjari na kuhakikisha kwamba, watu wa Mungu Ukanda wa Amazonia wanapata huduma msingi. Wananchi wa Ukanda wa Amazonia wanapaswa kushirikishwa kikamilifu kwa sababu wao ndio wadau wa mchakato mzima wa uinjilishaji na utamadunisho unaofumbatwa katika ushuhuda wa maisha yenye mvuto na mashiko!
Mwishoni, Kardinali Michael Czerny, Katibu mkuu msaidizi, Idara ya Wahamiaji na Wakimbizi, Baraza ya Kipapa la Huduma ya Maendeleo Endelevu na Fungamani ya Binadamu, kwa namna ya pekee, kwa niaba ya Baba Mtakatifu Francisko amewashukuru wadau wa tasnia ya mawasiliano walioliwezesha Kanisa kuwafikia watu wa Mungu sehemu mbali mbali za dunia. Wamewasaidia Mababa wa Sinodi kuzungumza na kusikilizwa. Tema kubwa inayobeba uzito mzima wa Hati ya Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia 2019 ni: Wongofu wa kiekolojia, kichungaji, kitamaduni na kisinodi, ili kusoma alama za nyakati na kutoa majibu muafaka kwa wakati huu. Wongofu huu unapaswa kujikita katika maisha ya mtu binafsi, jumuiya na watu wote wa Mungu katika ujumla wao. Wongofu wa kichungaji unapaswa kutoa kipaumbele cha kwanza katika maisha na utume wa Kanisa, ili kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa watu wote bila ubaguzi.
Watu wana kiu ya kusikiliza Injili ya matumaini. Wongofu wa kitamaduni unaweza kuwa na maana nyingi, lakini jambo la msingi ni upendo kwa Mungu na jirani unaokita mizizi yake katika maendeleo fungamani ya binadamu sanjari na utamadunisho, ili hatimaye, kudhibiti kinzani, migawanyiko na mipasuko inayoibuliwa kila kukicha kwenye ulimwengu utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia. Wongofu wa kiekolojia ni changamoto pevu inayopaswa kuvaliwa njuga na watu wote wa Mungu. Kwa bahati mbaya ugunduzi wa mafuta na gesi asili badala ya kuwa ni baraka kwa ustawi, maendeleo na mafao ya wengi, umekuwa ni chanzo cha vita, kinzani, uchu wa mali na madaraka. Ukanda wa Amazonia umetunukiwa utajiri na maliasili nyingi inayojumuisha ardhi ya kilimo, maji, mafuta, gesi asili, madini, misitu na wanyama pori. Amazonia ina kiwango kikubwa cha maliasili duniani, ikiwa ni pamoja na nishati jadidifu na nishati isiyokuwa jadidifu bila kusahau utajiri mkubwa wa watu na tamaduni zao. Utajiri huu uwe ni kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu Ukanda wa Amazonia.
Wongofu wa kisinodi anasema Kardinali Michael Czerny ni mchakato unaotekelezwa na Mama Kanisa kwa kuwahusisha watoto wake wote ili kujenga utamaduni wa kusikilizana katika ukweli na uwazi; kusoma alama za nyakati na kuzipatia tafakari makini kwa njia ya mang’amuzi; daima ustawi, mafao na maendeleo ya watu wa Mungu katika ujumla wake, yakipewa msukumo wa pekee. Hii ni safari inayosimikwa katika imani, sala na furaha ya Injili inayowagusa na kuwaambata wote. Mapokeo ya Kanisa, kwa kuendelea kusoma alama za nyakati, yameliwezesha Kanisa kuweza kufanya mageuzi makubwa katika maadhimisho ya Sinodi za Maaskofu, mageuzi ambayo yameanzishwa kunako mwaka 2015. Rasilimali kubwa ya Kanisa ni: Mapokeo, Injili na Imani inayomwilishwa katika ushuhuda kama kielelezo cha imani tendaji! Haya ndiyo ambayo Radio Vatican inapenda kukushirikisha wewe ndugu msikilizaji, ili nawe uweze kuwashirikisha pia jirani zako! Chema kula na ndugu yako!