Askofu mkuu Michael Francis Crotty: Balozi Mpya Nchini Niger
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko amemteua Askofu mkuu Michael Francis CROTTY kuwa Balozi mpya wa Vatican nchini Niger na ataendelea pia kuwa Balozi wa Vatican nchini Burkina Faso. Itakumbukwa kwamba, Askofu mkuu Michael Francis CROTTY alizaliwa tarehe 26 Machi 1970 huko Cloyne, nchini Ireland. Baada ya masomo na majiundo yake ya Kikasisi, tarehe 3 Julai 1994 akapewa Daraja Takatifu ya Upadre. Tarehe 1 Julai 2001 akaanza utume wake katika Diplomasia ya Kanisa na kupelekwa kutekeleza utume wake huko nchini: Kenya, Canada, Iraq, Yordan na Hispania.
Kati ya Mwaka 2009-2017 alipangiwa utume kwenye Idara ya Mambo ya nchi za Nje na Ushirikiano wa Kimataifa mjini Vatican. Kati ya Mwaka 2017 hadi Mwaka 2020 alikuwa ni Mshauri Ubalozi wa Vatican nchini Hispania. Tarehe 1 Februari 2020, Baba Mtakatifu Francisko akamteuwa kuwa Askofu mkuu. Tarehe 25 Aprili 2020, akateuliwa na Papa Francisko kuwa Balozi wa Vatican nchini Niger. Mama Kanisa anamtakia heri na baraka katika maisha na utume wake huko Niger ili aweze kuwa kweli ni shuhuda na chombo cha majadiliano ya kidini ili kukuza na kudumisha misingi ya haki, amani, upendo na maridhiano kati ya watu wa Mataifa.