Tafuta

Baraza la Kipapa la Kuhamasisha Umoja wa Wakristo  katika mwaka 2020 linaadhimisha kumbukumbu ya miaka 60 tangu kuanzishwa kwake kunako mwaka 1960. Baraza la Kipapa la Kuhamasisha Umoja wa Wakristo katika mwaka 2020 linaadhimisha kumbukumbu ya miaka 60 tangu kuanzishwa kwake kunako mwaka 1960. 

Miaka 60 ya Baraza la Kipapa la Kuhamasisha Umoja wa Wakristo!

Mambo makuu matatu yanaendelea kupewa kipaumbele cha kwanza: Uekumene wa Upendo; Uekumene wa Ukweli pamoja na Uekumene wa umoja, ili wote waweze kuwa wamoja chini ya Kristo Yesu! Haya ni mambo msingi ambayo viongozi wa Kanisa tangu baada ya maadhimisho ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wamejitahidi kuyavalia njuga katika maisha na utume wa Kanisa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Maadhimisho ya Kumbukumbu ya Miaka 60 tangu kuanzishwa kwa Baraza la Kipapa la Kuhamasisha Umoja wa Wakristo ni ushuhuda wa majadiliano ya kiekumene ambayo yamepewa kipaumbele cha pekee na Kanisa Katoliki kama sehemu vinasaba vya maisha na utume wake. Katika kipindi cha Miaka 60 kumekuwepo na mafanikio na maendeleo makubwa katika mchakato wa majadiliano ya kiekumene. Mambo makuu matatu yanaendelea kupewa kipaumbele cha kwanza: Uekumene wa Upendo; Uekumene wa Ukweli pamoja na Uekumene wa umoja, ili wote waweze kuwa wamoja chini ya Kristo Yesu! Haya ni mambo msingi ambayo viongozi wa Kanisa tangu baada ya maadhimisho ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wamejitahidi kuyavalia njuga katika maisha na utume wa Kanisa. Kardinali Kurt Koch, Rais wa Baraza la Kipapa la Kuhamasisha Umoja wa Wakristo katika mahojiano maalum na vyombo vya mawasiliano ya jamii mjini Vatican anasema, mwanzoni mwa mwaka 1960 dhana ya majadiliano ya kiekumene ilikuwa bado haijazama sana katika maisha na utume wa Kanisa Katoliki.

Lakini huo ulikuwa ni mwanzo wa mikutano na majadiliano ya kiekumene, ili kujeresha tena umoja wa Wakristo! Hata sasa, lengo hili bado halijaweza kufikiwa na Makanisa pamoja na madhehebu ya Kikristo. Ili kufikia lengo hili kuna haja ya kuwa na mwono sahihi kuhusu maana na umuhimu wa umoja wa Wakristo. Katika kipindi cha miaka 60 iliyopita, umekuwa ni muda muafaka kwa Makanisa na Madhehebu ya Kikristo kubadilishana amana na utajiri wa Makanisa haya kwa kujikita katika: Neno la Mungu, Maadhimisho ya Liturujia ya Kanisa pamoja na kuendeleza upembuzi yakinifu kuhusu mawazo ya kitaalimungu. Neno la Mungu na Injili ya Kristo lazima viwe ni kiini cha maisha na utume wa Kanisa. Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kukazia dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa, ili kujenga umoja na mshikamano kati ya watu wa Mungu kwa kutambua na kuheshimu umoja na tofauti zao msingi. Hii ni zawadi na amana kutoka kwa Kanisa la Kiorthodox. Kwa upande wake, Kanisa Katoliki linaendelea kukazia umuhimu wa Kanisa la Kiulimwengu linalojenga na kudumisha umoja na mshikamano na Makanisa mahalia, kwani yanategemeana na kukamilishana katika maisha na utume! Katika kipindi cha miaka 60 iliyopita, majadiliano ya kiekumene yamesaidia kuondokana na maamuzi mbele na hivyo kurahisisha maelewano miongoni mwa Wakristo.

Kumekuwepo na majadiliano ya kiekumene katika ukweli kwa kuangalia mambo yaliyosababisha Kanisa kumeguka na hatimaye, Wakristo kuanza kujitenga. Mkazo unaendelea kuwekwa kwenye mambo yanayowaunganisha Wakristo, kuliko yale yanayowagawa na kuwasambaratisha. Uekumene wa maisha ya kiroho na sala, umeendelezwa zaidi, kwa Wakristo kujizatiti zaidi katika ile Sala ya Yesu, ili wote wawe wamoja. Hii ni Sala ya Kikuhani inayoendelea kuwachangamotisha Wakristo kutekeleza mapenzi ya Yesu kwa kujenga na kudumisha umoja na mshikamano. Kardinali Kurt Koch anasema, Mama Kanisa anaadhimisha Jubilei ya Miaka 25 tangu Mtakatifu Yohane Paulo II alipochapisha Waraka wake wa Kitume “Ut unum sint” yaani “Ili wawe wamoja: Dhamana ya Kiekumene”. Ujumbe huu ulichapishwa hapo tarehe 25 Mei 1995. Mchakato wa majadiliano ya kiekumene ni dhamana inayoendelezwa mbele. Baba Mtakatifu Francisko anatambua fika kwamba, dhamana na utume wa Khalifa wa Mtakatifu Petro ni kati ya vikwazo vya mchakato wa ujenzi wa umoja wa Wakristo. Lakini pia anatambua fika kwamba, Kanisa Katoliki linao mchango wa pekee katika mchakato wa majadiliano ya kiekumene.

Ndiyo maana Mtakatifu Yohane Paulo II aliwataka Wakristo sehemu mbali mbali za dunia kujizatiti katika mchakato wa majadiliano ya kiekumene na kidugu; kwa kuongozwa na fadhila ya unyenyekevu. Kuna uwezekano wa kuwa mwono mpya wa maisha na utume wa Khalifa wa Mtakatifu Petro kwani hii inapaswa kuwa ni huduma ya upendo. Haya ni mawazo makuu yaliyofanyiwa kazi na Mtakatifu Yohane Paulo II na Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI. Mtakatifu Yohane XXIII alitambua fika umuhimu wa majadiliano ya kiekumene katika maisha na utume wa Kanisa. Huu ulikuwa ni mchakato pia wa kutaka kulipyaisha Kanisa Katoliki. Mtakatifu Paulo VI alijitahidi kumwilisha mafundisho ya Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican mintarafu majadiliano ya kiekumene. Akafanikiwa kuzungumza na wakuu wa Makanisa ya Kiorthodox na Kiangalikana na akabahatika kuwa Papa wa kwanza kutembea Makao Makuu ya Baraza la Makanisa Ulimwenguni, WCC.

Mtakatifu Yohane Paulo II aliona mapambazuko ya Millenia ya Tatu ya Ukristo kuwa ni muda muafaka wa kushuhudia uekumene wa damu na utakatifu wa maisha. Baba Mtakatifu Francisko anakazia umuhimu wa kujenga na kudumisha majadiliano ya kiekumene kwa kujenga madaraja yanayowakutanisha watu. Anakazia uekumene wa damu, maisha ya kiroho, sala na huduma ya upendo kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Kama sehemu ya kumbukumbu ya miaka 60 tangu kuanzishwa kwa Baraza la Kipapa la Kuhamasisha Umoja wa Wakristo sanjari na Jubilei ya Miaka 25 tangu Mtakatifu Yohane Paulo II alipochapisha Waraka wake wa Kitume “Ut unum sint” yaani “Ili wawe wamoja: Dhamana ya Kiekumene”, kunatarajiwa kuchapishwa kwa Mwongozo wa Kiekumene: “Vademecum Ecumenical”. Lengo ni kufafanua dhamana na utume wa Askofu katika mchakato wa majadiliano ya kiekumene.

Huu utakuwa pia msaada kwa Maaskofu wapya kama chachu ya kuwashirikisha katika majadiliano ya kiekumene. Kuna Jalida la “Information Service” ambalo limekuwa likichapishwa kwa takribani miaka 50 iliyopita ili kusaidia kusambaza habari za majadiliano ya kiekume zinazotekelezwa na Khalifa wa Mtakatifu Petro pamoja na Baraza hili la Kipapa. Kardinali Kurt Koch anaendelea kufafanua kwamba, majadiliano ya kiekumene yanatekelezwa kwa watu wa Mungu kujenga utamaduni wa kukutana na kujadiliana katika ukweli, haki, upendo na udugu. Baba Mtakatifu Francisko amekuwa mstaro wa mbele kuhamasisha sala ya kiekumene kama ilivyojitokeza tarehe 15 Mei 2020 pamoja na Sala ya Kiekumene ya Kuombea Waathirika wa Vita Mashariki ya Kati. Kardinali Koch anamshukuru Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI kwa kumteuwa kuwa Rais wa Baraza hili hapo tarehe 1 Julai 2010. Anamshukuru Mungu aliyemwezesha kulihudumia Kanisa chini ya Papa Francisko na Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI. Wakati wote huu, Roho Mtakatifu ameendelea kuliongoza Kanisa katika mchakato wa majadiliano ya kiekumene. Miaka kumi ya huduma ni nafasi ya kumshukuru Mungu katika mchakato wa majadiliano ya kiekumene, ili siku moja Wakristo waweze kuwa wamoja.

Kard. Kurt Koch
05 June 2020, 14:16