Katiba Mpya ya Kitume: Predicate evangelium: Hubirini Injili!
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Mkutano wa Baraza la Makardinali Washauri, umeadhimishwa siku ya Jumatano tarehe 14 Oktoba 2020 kwa njia ya mitandao ya kijamii. Makardinali walioshiriki ni pamoja na Kardinali Óscar A. Rodríguez Maradiaga, S.D.B., Kardinali Reinhard Marx, Kardinali Sean Patrick O’Malley, O.F.M. Cap., pamoja na Kardinali Oswald Gracias. Kutoka mjini Vatican walioshiriki ni pamoja na Kardinali Pietro Parolin, Kardinali Giuseppe Bertello, pamoja na Askofu Marcello Semeraro, Katibu mkuu wa Baraza la Makardinali Washauri pamoja na Katibu Mwambata Askofu Marco Mellino. Baba Mtakatifu Francisko ameungana na Baraza la Makardinali Washauri akiwa kwenye Hosteli ya Mtakatifu Martha, iliyoko mjini Vatican ambayo kwa sasa inatumika kama makazi yake ya muda!
Baraza la Makardinali katika kipindi cha likizo ya kiangazi wameendelea kupitia na kuchambua Muswada wa Katiba mpya ya Kitume inayojulikana kama “Predicate evangelium” yaani “Hubirini Injili” kwa kuuboresha zaidi na hatimaye, kuwasilishwa kwa Baba Mtakatifu Francisko. Muswada huu kwa sasa umeingia hatua ya pili, ili uwasilishwe kwenye Mabaraza ya Kipapa tayari kusomwa, kupembuliwa na kufanyiwa maboresho zaidi. Mkutano wa Baraza la Makardinali pamoja na mambo mengine, umeangalia jinsi ya kutekeleza Katiba Mpya ya Kitume: “Predicate evangelium” yaani “Hubirini Injili” baada ya kuidhinishwa na Baba Mtakatifu. Baba Mtakatifu amewashirikisha Makardinali washauri juu ya utekelezaji wa Katiba katika masuala ya uchumi na uongozi. Kutokana na janga la homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19 kuendelea kutishia usalama, amani na utulivu, mkutano ufuatao wa Baraza la Makardinali Washauri utafanyika mwezi Desemba 2020 kwa kutumia mitandao ya kijamii.