Baba Mtakatifu Francisko ameridhia ombi lililowasilishwa kwake na Askofu Telesphor Mkude wa Jimbo Katoliki Morogoro la kutaka kung'atuka kutoka madarakani. Baba Mtakatifu Francisko ameridhia ombi lililowasilishwa kwake na Askofu Telesphor Mkude wa Jimbo Katoliki Morogoro la kutaka kung'atuka kutoka madarakani. 

Askofu Telesphor Mkude wa Jimbo la Morogoro Ang'atuka Madarakani

Tangu tarehe 12 Februari 2019, majukumu yote ya: kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu Jimbo Katoliki Morogoro yamekuwa yakisimamiwa na Monsinyo Lazarus Vitalis Msimbe Msimamizi wa Kitume wa Jimbo Katoliki la Morogoro, ili kutoa nafasi kwa Askofu Telesphor Mkude kushughulikia zaidi afya yake ambayo kwa miaka ya hivi karibuni iliteteleka sana.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko ameridhia ombi lililowasilishwa kwake na Askofu Telesphor Mkude wa Jimbo Katoliki la Morogoro, Tanzania la kutaka kung’atuka kutoka madarakani. Itakumbukwa kwamba, tangu tarehe 12 Februari 2019, majukumu yote ya: kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu Jimbo Katoliki Morogoro yamekuwa yakisimamiwa na Monsinyo Lazarus Vitalis Msimbe, S.D.S ambaye aliteuliwa na Baba Mtakatifu Francisko kuwa Msimamizi wa Kitume wa Jimbo Katoliki la Morogoro, ili kutoa nafasi kwa Askofu Telesphor Mkude ambaye alikuwa bado ni Askofu wa Jimbo la Morogoro (Sede plena) kushughulikia zaidi afya yake ambayo kwa miaka ya hivi karibuni iliteteleka sana.

Itakumbukwa kwamba Askofu mstaafu Telesphor Mkude wa Jimbo Katoliki la Morogoro alizaliwa tarehe 30 Novemba 1945 huko Pinde, Wilaya ya Mvomero mkoani Morogoro. Baada ya masomo na majiundo yake ya Kikasisi, tarehe 16 Julai 1972 akapewa daraja Takatifu ya Upadre kwa ajili ya Jimbo Katoliki la Morogoro. Tarehe 18 Januari 1988, Mtakatifu Yohane Paulo II akamteuwa kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki la Tanga na kuwekwa wakfu tarehe 26 Aprili 1988 na Hayati Kardinali Laurean Rugambwa, Askofu mkuu mstaafu wa Jimbo kuu la Dar es Salaam. Ilipogota tarehe 5 Aprili 1993, tena Mtakatifu Yohane Paulo II akamteuwa kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki la Morogoro hadi tarehe 30 Desemba 2020, Baba Mtakatifu Francisko aliporidhia ombi la kung’atuka kwake kutoka madarakani.

Kati ya amana na utajiri mkubwa ambao Askofu mstaafu Telesphor Mkude wa Jimbo Katoliki la Morogoro ameliacha Kanisa la Afrika Mashariki na wale wote wanaozungumza lugha ya Kiswahili ni Tafsiri ya Katekisimu ya Kanisa Katoliki kwa lugha ya Kiswahili. Huu ni muhtasari wa kile ambacho Mama Kanisa anakiri na kuamini, anaadhimisha, anaishi na kusali. Yaani: Imani, Sakramenti za Kanisa, Amri za Mungu na Maisha ya Sala. Alitekeleza dhamana hii, kama Mwenyekiti wa Idara ya Katekesi ya Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, TEC. Aliwaalika watu wa Mungu ndani na nje ya Tanzania kuipokea, kuisoma na kuitafakari, ili umoja katika imani ambayo ni chemchemi na msingi wake ni Fumbo la Utatu Mtakatifu uimarishwe na kuenezwa hadi miisho ya dunia! Kwa ufupi kabisa, Askofu mstaafu Telesphor Mkude wa Jimbo Katoliki la Morogoro amewaongoza, amewatakatifuza na kuwafundisha watu wa Mungu kama Padre kwa muda wa miaka 48 hadi kufikia mwaka 2020 na Miaka 32 kama Askofu Jimbo.

Askofu Mkude

 

 

30 December 2020, 11:58