Papa Francisko na Uislamu katika ncha tatu za mafundisho yake
ANDREA TORNIELLI
Kuna ncha tatu ambazo zinaunganisha hotuba tatu muhimu za Papa Francisko kuhusu mazungumzo ya kidini kwa namna ya pekee na Uislamu. Ni magisterium ambayo inaonesha ramani ya barabara iliyo na alama tatu msingi za kumbukumbu: nafasi ya dini katika jamii zetu, kigezo cha udini wa kweli na njia thabiti ya kutembea kama ndugu na kujenga amani. Hayo yanapatikana katika hotuba ambazo Askofu wa Roma alitoa huko Azerbaijan mnamo 2016, huko Misri mnamo 2017 na sasa wakati wa safari yake ya kihistoria nchini Iraq, katika mkutano ambao hautasahaulika huko Uru ya Wakaldayo, mji wa Ibrahim. Hotuba ya kwanza ilikuwa kama vile Washia wa Kiazabajani ni wasikilizaji, lakini pia na jumuiya nyingine za kidini za nchi hiyo, ya pili ilielekezwa hasa kwa Waislamu wa Sunni wa Misri na mwishowe ile ya tatu ilihutubiwa kwa hadhira pana ya kidini pamoja na kuwa na Waislamu wengi, kwa kuongezea Wakristo na wawakilishi wa dini za zamani za Mesopotamia.
Kile ambacho Papa Francisko anapendekeza na kutekeleza sio njia inayosahau tofauti na utambulisho ili kuweka kila kitu sawia. Badala yake, ni wito wa kuwa waaminifu kwa utambulisho wao wa kidini ili kukataa kila aina ya unyonyaji wa dini na katika kuchochea chuki, mgawanyiko, ugaidi, ubaguzi na wakati huo huo washuhudie katika jamii zinazozidi kuwa za kidunia kuwa tunamhitaji Mungu. Huko Baku, mbele ya Sheikh wa Waislamu wa Caucasus na wawakilishi wa jamuiya nyingine za kidini nchini humo, Papa Francisko alikumbuka “kazi kubwa” ya dini, ile ya “kusindikiza watu kutafuta maana ya maisha, kusaidia wao kuelewa kwamba uwezo mdogo wa mwanadamu na mali za ulimwengu huu hazipaswi kuwa ndizo za kipekee kabisa”.
Huko Cairo, akizungumza katika Mkutano wa Kimataifa wa Amani uliohamasishwa na Imam Mkuu wa Al Azhar Al Tayyeb, Papa Francisko alikuwa amesema kwamba Mlima Sinai “unatukumbusha kwanza kabisa kuwa agano halisi duniani haliwezi kupuuza Mbingu, kwamba ubinadamu hauwezi kupendekeza kukutana kwa amani ukiondoa Mungu kwenye upeo na hata hauwezi kupanda mlima ili kumiliki Mungu”. Ni ujmbe wa maana sana wa sasa mbele ya kile ambacho Papa aliita “kitendawili hatari”, kwa maana ya kusema kwamba: kwa upande mmoja, tabia ya kuachia dini tu katika nyanja ya kibinafsi, bila kuitambua kama mwelekeo wa kibinadamu na wa kijamii "; na kwa upande mwingine, machafuko yasiyofaa kati ya nyanja za kidini na kisiasa.
Huko Uru, mnamo Jumamosi tarehe 6 Machi 2021 , Papa Francisko alikumbusha kwamba ikiwa mtu “atamfukuza Mungu, anaishia kuabudu vitu vya kidunia”, akitoa mwaliko wa kuinua “macho Mbinguni” na kufafanua kama “dini ya kweli” ile ya kumpenda Mungu na kumpenda jirani. Huko Cairo, Papa alielezea kuwa viongozi wa kidini wameitwa kufunua vurugu zinazojifanya kuvaa utakatifu, wakiegemea kwenye ubinafsi tu badala ya uwazi halisi na “kukemea ukiukwaji wa hadhi ya binadamu na dhidi ya binadamu. Kupeleka mwanga na kujaribu kukemea aina zote za chuki kwa jina la dini na kulaani kama uwongo wa ibada ya sanamu ya Mungu”.
Huko Baku, Papa aliangazia nafasi ya kusaidia “kugundua mema na kujikita katika matendo ya dhati, kwa sala na kwa ugumu wa kazi ya undani; walialikwa kujenga utamaduni wa kukutana na amani, inayoundwa na uvumilivu, uelewa, unyenyekevu na hatua thabiti”. Wakati wa mzozo, dini alisema mfuasi wa Petro huko Azabajani, “inawezekana kuwa asubuhi ya amani, mbegu za kuzaliwa upya katikati ya mauti, mwangwi wa mazungumzo ambayo yanasikika bila kuchoka, njia za kukutana na upatanisho kufika huko pia, ambapo majaribio ya upatanisho rasmi yanaonekana hayana matokeo”.
Akiwa huko Misri Papa alielezea kwamba hakuna uchochezi wa vurugu utakaohakikishia amani” na kwamba “ili kuzuia mizozo na kujenga amani ni muhimu kufanya kazi ili kuondoa hali za umaskini na unyonyaji, mahali ambapo msimamo mkali una uwezekano mkubwa wa kuota mizizi”. Ni maneno pia ambayo yamesikika katika hotuba huko Uru kwamba: “Hakutakuwa na amani bila kushirikishana na kukaribisha, bila haki ambayo inahakikisha usawa na kuhamasisha wote, kuanzia na wadhaifu zaidi. Hakutakuwa na amani bila watu kunyosha mikono yao kuwasaidia watu wengine”.
Katika hotuba tatu za kipapa kwa maana hiyo zinaonesha jukumu ambalo udini unao leo hii katika ulimwengu ambao matumizi ya watu na kukataliwa kwa utakatifu kunatawala na ambapo imani inaelekea kuwa suala la kibinafsi. Lakini pia kuna haja, ambapo Papa Francisko anaelezea, dini halisi, ambayo haitenganishi ibada ya Mungu na upendo kwa kaka na dada. Na hatimaye Papa anaonesha njia ya kuhakikisha kuwa dini zinachangia wema wa jamii zetu, akikumbusha hitaji la kujitoa kwa sababu ya amani na kujibu shida na mahitaji halisi ya wachache, maskini, na wasio na ulinzi.
Ni pendekezo la kutembea bega kwa bega, “ndugu wote”, yaani “wote ni ndugu ili kuwa mafundi wa kweli wa amani na haki, zaidi ya tofauti na kwa utambulisho wao. Mfano wa njia hii ulinukuliwa na Papa Francisko, akikumbuka msaada wa vijana Waislamu kwa ndugu zao Wakristo katika utetezi wa makanisa huko Baghdad. Mfano mwingine ulitolewa na ushuhuda huko Uru na Rafah Hussein Baher, mwanamke wa Iraq wa dini ya Saba-Mandean, ambaye katika ushuhuda wake alitaka kukumbusha sadaka ya Najay, mtu wa dini ya Saba-Mandean kutoka Basra, ambaye alipoteza maisha kwa sababu ya kuokoa maisha ya jirani yake Mwislamu.