Viongozi wa San Marino Wakutana na Papa Francisko mjini Vatican!
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko, Jumatatu tarehe 15 Machi 2021 amekutana na kuzungumza na viongozi wakuu wa Jamhuri ya Watu wa San Marino. Hawa ni Waheshimiwa Alessandro Cardelli na Mirko Dolcini pamoja na msafara wao ambao baadaye, wamekutana na kuzungumza na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican aliyekuwa ameambatana na Askofu mkuu Paul Richard Gallagher, Katibu mkuu wa mambo ya nchi za nje na ushirikiano wa Kimataifa mjini Vatican. Katika mazungumzo yao, viongozi hawa wameridhishwa na uhusiano mzuri wa kidiplomasia kati ya nchi hizi mbili.
Masuala ya Kimataifa yamegusiwa na viongozi hawa wakati wa mazungumzo yao, ikiwa ni pamoja na mahusiano kati ya Nchi za Umoja wa Ulaya, EU pamoja na masuala ya diplomasia ya Kimataifa. Kwa namna ya pekee kabisa, Baba Mtakatifu na viongozi wakuu wa San Marino wamejielekeza zaidi katika janga la Virusi vya Korona, UVIKO-19 pamoja na mchakato wa chanjo unaoendelea ndani na nje ya Jamhuri ya Watu wa San Marino. Wamegusia pia kuhusiana na Sera za familia pamoja na ruzuku inayotolewa na Serikali kwa watoto wachanga wanazozaliwa nchini humo. Wamezungumzia pia kuhusu masuala ya wakimbizi na wahamiaji pamoja na njia za kuweza kuwasaidia mintarafu sheria, kanuni na taratibu za Jumuiya ya Kimataifa.